loader
Hali ya kimbunga Kenneth yawa tete

Hali ya kimbunga Kenneth yawa tete

KUTOKANA na tahadhari ya kimbunga Kenneth kupiga katika pwani ya mikoa ya Mtwara na Lindi, serikali na taasisi zake zimechukua hatua za tahadhari katika kukabiliana na kimbunga hicho ili kuepuka maafa makubwa kwa wananchi wa mikoa hiyo na maeneo jirani.

Katika taarifa yake kwa umma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema kimbunga hicho kinatarajiwa kusababisha athari mbalimbali ikiwemo mtawanyiko mkubwa wa mafuriko na upepo mkali wa kasi ya kilomita 130 kwa saa katika uelekeo wa mashariki umbali wa kilomita 175 kutoka pwani ya Mtwara.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, kimbunga hicho pia kinatarajiwa kusogea na kuelekea katika pwani kusini mwa Tanzania na kitaambatana na mafuriko ikizingatiwa kuwa pwani ya mikoa ya Mtwara na Lindi ipo chini ya usawa wa bahari. Athari zingine ambazo kimbunga hicho kinaweza kusababisha zimetajwa kuwa ni maisha ya watu, uharibifu wa makazi, mali, mazao mashambani, miundombinu na mazingira, shughuli za usafirishaji kwa njia ya maji, anga na nchi kavu.

“Serikali inaelekeza shughuli mbalimbali zinazofanywa kandokando na ndani ya Bahari ya Hindi hususani uvuvi, biashara ndogondogo, usafirishaji majini na anga zisitishwe katika kipindi hiki kilichotabiriwa kuwa hatarishi ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza, kamati za maafa zifuatilie kwa kina jambo hili,” alieleza Mhagama. Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ilitabiri uwezekano wa kutokea kimbunga hicho na mafuriko katika maeneo ya pwani ya mikoa ya Mtwara na Lindi kuanzia Aprili 24-26, mwaka huu.

Taasisi zajiandaa Katika kuchukua tahadhari ya kuepuka maafa yanayoweza kusababishwa na kimbunga Kenneth, Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Godfrey Zambi, ameagiza shule zote kwenye mikoa hiyo kufungwa pamoja na taasisi za umma ikiwemo ofisi za mkoa, fedha na binafsi kwa siku mbili kuanzia jana na kuwataka watu wabaki majumbani mwao, wasitaharuki kwa kukimbia hovyo kwa sababu za kiusalama.

Alisema maeneo ambayo yanatakiwa kuendelea na kazi katika siku hizo mbili ni vituo vya afya, hospitali, polisi na magereza. Zambi alisema mkoa wake umetenga maeneo ya dharura ya milimani ambako wananchi wanaoishi mabondeni wanapaswa kwenda kuishi kwa muda, huku huduma za dharura za afya na zimamoto zikiwa zimewekwa katika hali ya utayari. Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, wananchi wanaoishi kando kando ya ukanda wa pwani wanatakiwa kuhamia katika Shule za Sekondari za Angaza, Mpilipili, Lindi Sekondari, Uwanja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Uwanja wa Mpira wa Mtanda.

“Tumesimamisha kwa tahadhari vyombo vya baharini pamoja na kivuko visifanye kazi, lakini pia maadhimisho ya siku ya malaria duniani nzilizopangwa kufanyika mkoani hapa kitaifa nazo tumezisitisha baada ya kushauriana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,”alisema Zambi. Naye Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Leonard Subi, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kutokaa kwenye madirisha, nyumba ziwe wazi, wakae ndani na chini ya meza.

Dk Subi alisema kuwa vituo vyote vya afya katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma vitakuwa wazi wakati wote kwa ajili ya kutoa huduma endapo kutatokea maafa. Kwa upande wake, Msajili wa Meli kutoka Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Japhet Loisimaye, alisema wamiliki wa vyombo vya majini katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Wilaya ya Mafia nao wanatakiwa kusitisha shughuli zao kwa muda mpaka itakapotolewa tena taarifa nyingine ya hali ya usalama baharini.

Loisimaye alisema japo kimbunga hicho kimeelezwa kupiga katika pwani ya Mkoa wa Mtwara kwa sehemu kubwa, lakini katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Wilaya ya Mafia kunaweza kuwa na upepo mkali unaoweza kusababisha maafa makubwa, hivyo ni vyema vyombo hivyo vidogo na vikubwa, vya abiria na mizigo visiingie majini katika siku hizo tatu za tahadhari.

Kauli ya Zimamoto Kwa kuzingatia madhara yanayoweza kusababishwa na kimbunga Kenneth, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini limetoa wito kwa wananchi waishio katika maeneo hatarishi, ikiwemo pembezoni mwa bahari na kandokando ya mito, kuyahama maeneo hayo haraka. Kamishna wa Operesheni wa Jeshi hilo, Billy Mwakatage, alisema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa pamoja na kusikiliza vyombo vya habari na kuzingatia tahadhari zinazotolewa.

Kwa kuwa kimbunga hicho kinaambatana na mvua kubwa, Mwakatage amewataka wananchi kuepuka kusimama au kuegesha magari yao chini ya miti mikubwa kwa kuwa kuna uwezekano wa miti mikubwa kuanguka, lakini pia mawe makubwa na udogo kuporomoka na kuziba barabara. Hali ya Zanzibar Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Usafiri baharini Zanzibar (ZMA), imesitisha shughuli za usafiri wa baharini kuanzia jana mchana kutokana na tahadhari ya Kimbunga Kenneth. Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, Ramadhan Hussein, alisema kuwa wamelazimika kusitisha shughuli za safari kwa vyombo vyote baharini hadi hapo taarifa zaidi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa zitakapotolewa.

Bunge latoa tahadhari Akiwa bungeni jana Waziri Mhagama aliwataka wananchi wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi kujiepusha kwa kuondoka maeneo hayo kabla ya hali hatarishi ya kimbunga na mafuriko kutokea.

Pia ilisema shughuli mbalimbali zinazofanywa kando na ndani ya Bahari ya Hindi zikiwemo za uvuvi, biashara ndogo na usafirishaji wa majini na anga, zinatakiwa kusimamishwa katika kipindi hicho ili kuepusha athari zinazoweza kutokea kwa wananchi. Alitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu (PM) na Idara ya Maafa. Alisema kimbunga hicho kitaendelea kusogea kuelekea hadi Pwani ya Kusini ya nchi na kitaandamana na mafuriko kwani Pwani ya mikoa ya Mtwara na Lindi kwani mikoa hiyo ipo chini ya Usawa wa Bahari (ASL).

Alisema hali hiyo inatarajiwa kuleta athari mbalimbali zikiwemo za mtawanyiko mkubwa wa mafuriko na upepo mkali ambavyo vinavyoweza kusababisha athati kwa maisha uharibifu wa makazi, mali, mazao shambani, miundombinu na mazingira kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya Bahari ya Hindi katika kipindi kifupi. Aidha alisema, shughuli za usafirishaji kwa njia wa anga na kwenye maji na nchi kavu zinaweza kuathirika katika mikoa hiyo kutokana na hali mbaya inayotabiriwa na TMA. “Tunaendelea kusisitiza kwamba Kamati za Maafa katika ngazi za vijiji hadi mikoa katika maeneo husika, kwa mujibu wa sheria tuliyonayo, kufuatilia kwa karibu na kwa kina jambo hilo ambalo limekwisha kutabiriwa,” alisema.

Taharuki Mtwara Wakati huo huo, Mwandishi Sijawa Omary anaripoti kutoka Mtwara kuwa wakazi wa mkoani humo walilazimika kukimbia makazi yao na kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kunusuru maisha yao baada ya kimbunga Kenneth kupita pembezoni mwa mkoa huu kuelekea nchi jirani ya Msumbiji. Gazeti hili lilishuhudia namna ambavyo wananchi wa mkoa huo walivyokuwa wakihangaika huku na kule kufuata sehemu za kunusuru maisha yao juu ya tukio hilo.

 

Baadhi ya maeneo ambayo wakazi hao walikusanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa na serikali ya mkoa huu kuwa wananchi waishio kando kando ya bahari wahamie kwenye maeneo ambayo yatakuwa salama kwao na hata likitokea tukio hilo madhara hayatakuwa makubwa kwao. Maeneo hayo ya muda ambayo wakazi hao walikusanyika ilikuwa ni pamoja na shule za msingi na sekondari, Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Naliendele, Mangamba, Shule ya Sekondari ya Mustafa Sabodo na maeneo mengine.

Mkazi eneo la Shule ya Msingi Tandika, Majengo Manispaa ya Mtwara Mikindani, Amina Abdul alisema kuwa, tukio hilo ilikuwa wakiona tu katika nchi za wenzao na madhara yake huwa ni makubwa na mkoa huu ni mara ya kwanza kuripotiwa kutokea kwa tukio hili. Mustafa Joki, mkazi wa Chuno alisema, mara baada ya serikali kutangaza janga hilo, yeye na familia yake wakafanya maamuzi ya kuchukua tahadhari ya kuhama makazi yao na kuhamia katika vituo ambayo wameelekezwa ili kunusuru maisha yao na kuomba tukio hilo lisitokee.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa wakati akizungumza na wananchi hao walioko katika maeneo hayo alisema waendelea kuwa na subira kwa kubaki katika maeneo hayo ambayo ni salama kwao huku serikali ikiendelea kufuatilia zaidi hatua na hali inayoendelea kadiri muda unavyoendelea juu ya tukio hilo na kisha kuwapatia taarifa. Hata hivyo, mkuu huyo alikanusha uvumi uliosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa hali Mtwara siyo shwari kwani mpaka sasa hali ni shwari na hakuna madhara yoyote ambayo yameweza kutokea hadi sasa kutokana watu wameweza kuchukua tahadhari.

Meneja wa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Kusini, Daudi Amasi alisema, kuanzia majira ya asubuhi jana hii hali ya upepo ilianza na kilometa 20 ikaja hadi 30 ikafikia 40 ambapo hadi kufikia majira ya mchana hali ya upepo ilifikia kilometa 60 kwa saa. “Tunaendelea kusisitiza kwa wananchi wa maeneo hayo na maeneo mengine hapa nchini kuendelea kuchukua tahadhari pale panapotokea matukio kama haya na tunapotoa taarifa kama hizi basi wananchi uchukuwe tahadhari ili kuepeusha madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Amasi.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa huyo amevunja kambi zote sita ambazo wakazi hao walikimbilia kwa ajili ya kunusuru maisha makambi ambayo serikali ya Mtwara ilitangaza. Alisema, endapo kutatokea mabadiliko yoyote juu ya tukio hilo watapatiwa taarifa kupitia vyombo vya habari ambavyo viko rasmi ambapo hadi hivi sasa mkoani hapa hali imekuwa shwari na hakujatokea tatizo lolote.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/326a1ad95d295158d9e5d02eba04d37c.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi