loader
Picha

Sheikh Thabit Kombo: Nyerere hakulazimisha Muungano

KWENYE kitabu cha masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha ambacho utangulizi wake umeandikwa na Mwalimu Julius Nyerere, kwenye Sura ya 10, ameeleza kwa undani sababu za kuunganika kwa Tanganyika na Unguja na kuzaliwa Tanzania.

Aidha, ameandika namna mafi sadi wa Muungano wanavyousimanga Muungano huu na kuufanyia kila hila ili ubomoke nao wajipatie wanachotaka ambacho kinazuiwa na Muungano, ubinafsi. Katika maandiko hayo, Sheikh Thabit anasema: “Mafisadi wanalalamika, kwanini Muungano umefanyika harakaharaka; mapinduzi Januari na Muungano Aprili, miezi mitatu tu!” Anasema, wapo wanaodhani kuwa Mwalimu Nyerere ndiye aliyelazimisha Muungano. Kwa mujibu wa maandiko yake, Sheikh Kombo anasema wazo la Muungano ni wazo la chama cha Afro Shirazi tangu mwanzo.

Anasema katika ilani yao, walisema kwa wakipata uhuru azima ya ASP (Afro Shiraz Party) ni kuona kuwa, Afrika yote inakuwa moja yenye nguvu. Kutokana na kauli hiyo thabiti iliyokuwa katika maandiko, ASP ilikuwa inashiriki katika mazungumzo ya Pafmeca na Pafmecsa. Anasema pamoja na mambo hayo Tanganyika na Zanzibar, ahadi ya Muungano ilikuwa ni ahadi ya wanachama wenyewe waliokuwa wanaitoa katika mikutano yao yote wakisisitiza kuwa, pindi watakapopata uhuru, wataungana na wenzao wa Tanganyika.

Muungano kwa wanachama wa ASP ilikuwa ni mwanzo wa kujenga Afrika moja. “Na kweli katika historia zetu wote. Watu wa Tanganyika na Watu wa Zanzibar ni wale wale, tofauti na sisi wa Zanzibar kutawaliwa na Sultani,” anasema Sheikh Thabit. Sheikh Thabit anasema kauli ya Muungano ilikuwa kauli ya umma wa Zanzibar ni kauli ya Afro Shirazi iliyokuwa ikitawala wakati huo, ni ridhaa ya watu wenyewe wa Tanganyika na Zanzibar.

Anasema baada ya mafani-kio katika mapinduzi kilichobaki kilikuwa ni kuungana na Tanganyika na Sheikh Karume anaelezwa kuwa hodari kwa kupima mahitaji ya wananchi na kuamua kukamilisha muungano kwa niaba yao. Sheikh Thabiti anasema wananchi wa visiwa walifurahia kuungana na wenzao kwani walijuana wakiwa katika unyonge na sasa wakataka kujuana katika heshima ya uhuru na nguvu ya kushiriki serikali.

Anasema: “Ni kama ndugu waliopoteana siku nyingi, sasa wakawa wameonana tena!” Moja la msingi ambalo limo katika kitabu hicho kuhusu Muungano ni maslahi ndani ya Muungano ambapo Sheikh Thabiti anasema yaliwezesha na kuzimwa kwa vitimbi vya wapinga mapinduzi. “Kusingekuwepo Muungano tungekuwa na hasara kubwa, kwa Tanganyika na kwa Zanzibar pia.

Zanzibar pamoja na mapinduzi yake, ingedumu katika wasiwasi kwamba mbinu zingeweza kutumika kumrudisha Sultani. Na Tanganyika, pamoja na ukubwa wake, isingekuwa salama kabisa kama kungekuwepo na vurugu visiwani hapa,” anaandika Sheikh Thabit. Anasema maadui wangeweza kuitumia Zanzibar kuihujumu Tanganyika kwa urahisi sana. Kuna mambo mengi ambayo Sheikh Thabiti aligusa usalama wa Tanganyika na Zanzibar na hasa alizungumzia hofu ya fitina na usalama unaoweza kuibuliwa na wanaotaka kuhujumu mataifa haya mawili.

Ndani ya Muungano, haikuwa rahisi kwa mahasimu wa pande zote mbili kutumia eneo moja kupanga machafuko kwa upande mwingine na hasa mwanya wa waliopinduliwa kutumia Tanganyika kurejea Zanzibar au Marekani waliotimuliwa kufanya mpango wa kurejea kiurafiki au kwa hila. Marekani walikuwa na kituo cha kijasusi katika eneo la Tunguu na baada ya mapinduzi, Serikali ya Zanzibar ilikataa uwapo wao wakafunga virago na kuondoka. Marekani katika hili, hawakufurahi hata chembe na kulikuwa na kila dalili ya kutumia mabavu kubakia Zanzibar.

Imeelezwa kuwa, baada ya mapinduzi, mazungumzo yalifuata ili kuukamilisha muungano uliotenganishwa na wakoloni. Sheikh Abeid Amani Karume aliongoza viongozi wa Zanzibar katika mazungumzo ya siku moja jijini Dar es Salaam na upande wa Tanganyika ukiongozwa na Mwalimu Nyerere. Anasema hoja haikuwa muungano, bali muungano uwe wa sura gani.

Mazungumzo yaliyafanyika na maelekezo na kisha wataalamu wakaenda kuyaandika kwa ufasaha. Katika kitabu chake, Sheikh Thabit anasema Aprili 22, 1964 Mwalimu Nyerere, Rais wa Tanganyika alifika Unguja kukamilisha mazungumzo yake na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mpaka yakafikiwa makubaliano kamili.

“Kuja kwa Mwalimu Nyerere kulikuwa kama kugonga muhuri katika maafikiano yaliyokuwapo tangu zamani,” anaandika Sheikh Thabit. Katika masimulizi yake, inaonekana dhahiri kwamba taratibu zilifuatwa na kiu za wananchi wa pande hizi mbili zilisikika na kutekelezwa. Baada ya mazungumzo na kufikiwa kwa mwafaka Visiwani, Mwalimu Nyerere Aprili 25,1964 aliitisha kikao cha dharura cha Bunge la Tanganyika ili kuthibitisha makubaliano ya msingi ya muungano yaliyofikiwa katika mazungumzo baina ya viongozi wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika hotuba yake, Mwalimu Nyerere anasema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano wa azma ya Afrika nzima kuwa nchi moja yenye nguvu. “Tunashirikiana kwa mila, kwa lugha, kwa tabia na hata kwa siasa…” anasema Mwalimu Nyerere na Aprili 26 Sheikh Abeid Amani Karume akifuatana na mawaziri na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi walikwenda Dar es Salaam kusaini hati ya Muungano. Baada ya tukio hilo, Mwalimu Nyerere aliteua watu 6 kutoka Zanzibar kuingia katika Bunge la Afrika Mashariki na watu 47 kuingia katika Bunge la Muungano.

Katika orodha hiyo, wajumbe wote 23 wa Baraza la Mapinduzi waliteuliwa kuwa wabunge na miongoni mwa wale 14 waliozidi, Thabit Kombo Jecha alikuwa mmojawapo. Kiukweli Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania Aprili 26, 1964 ni matokeo ya kihistoria zaidi kwa kuwa kabla ya kuja wakoloni, pande hizi mbili zilikuwa na uhusiano mkubwa kibiashara, kidamu, kiutamaduni na kisiasa.

Uhusiano wa vyama vya ASP na TANU ulifanya kuwepo nia ya dhati ya kuunganisha pande hizo mbili. Hata hivyo, licha ya changamoto kadhaa zinazoweza kuwapo au kujitokeza, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeendelea kuimarika siku hadi siku kwa kusimamiwa na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuungwa mkono na wananchi wanaoitakia mema Tanzania.

Mashauriano na mijadala imeokoa hekaheka nyingi ambazo zilizokuwa zinasukumwa katika Jamhuri ya Muungano ili kuwagawa wananchi. Pia, mpangilio mzuri wa namna ya kutatua matatizo ya Muungano umeufanya muungano huu kuwa wa aina yake na wa kipekeee barani Afrika na duniani kote. Imeandikwa na Beda Msimbe kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

ELIMU ya msingi ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya mtoto ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi