loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchafu mitaani uwatumbue maofisa afya

SUALA la uchafu wa mazingira ni jipu linalohitaji kutumbuliwa kuanzia ngazi ya jamii hadi watendaji. Uchafu wa mazingira unahusisha vyoo, mitaro kufurika uchafu, taka kukusanywa na kuacha kwenye maeneo muda mrefu kiasi cha kusababisha harufu na utupaji taka hovyo kuanzia majumbani hadi mitaani.

Kwa upande wa vyoo, hili ni tatizo kubwa ambalo natamani mamlaka zinazohusika na usimamizi kuandaa kampeni maalumu siyo tu ya kuhamasisha, bali pia kuwajibisha wale wote watakaokutwa wanatumia vyoo vichafu.

Kama hujawahi kushuhudia choo kichafu, basi omba Mungu usikutane nacho! Yupo mwingine anaweza kudhani vyoo vichafu ni kwa vijijini tu. La hasha! Hata mijini, yapo maeneo/ familia zinaoishi kwa kutumia vyoo ambavyo ni hatarishi kwa afya.

Si tu kwa familia, bali pia unakuta taasisi, wafanyakazi wanatumia vyoo vya ajabu ambavyo inakulazimu ujiulize mara mbili mbili kabla ya kwenda kukidhi haja.

Nakumbuka mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliwahi kueleza namna anavyokerwa na uchafu wa vyoo katika ofisi na taasisi za serikali na akataka suala hilo liangaliwe kwa umakini kuepusha mlipuko wa maradhi yatokanayo na uchafu.

Ilikuwa Agosti mwaka jana alipokuwa akitangaza shindano la kitaifa la usafi wa mazingira ambalo lilihusisha vipengele kadhaa kikiwamo cha matumizi ya vyoo bora.

Alisema licha ya kwamba watendaji wa serikali ndiyo wanapaswa kuwa wahamasishaji wa usafi kwa kiwango kikubwa, lakini wamekuwa wakitumia vyoo vichafu. Kwa upande wa shule, aliagiza zishindanishwe kupata choo bora na safi.

Namnukuu: “Kuna ofisi za umma ukienda chooni unaweza kutamani ukajisaidie barabarani kutokana na uchafu, tatizo kubwa naliona Watanzania hawazingatii mazingira na usafi wa vyoo.”

Nikirejelea kwenye kwenye jamii, ukiacha suala zima la utupaji taka hovyo, zipo kaya nyingi zinaishi kwa kutumia vyoo vya ‘ajabu’. Hilo halihitaji utafiti wa kina, bali ni suala linalojidhihirisha.

Tena katika jiji kama Dar es Salaam, unakuta familia inatumia choo ambacho ukikishuhudia unabaki kujiuliza ni tatizo ni nini?.

Tena unakuta vyoo vya namna hiyo (vichafu), vinatumika hata kwenye mighahawa, baa na maeneo mengine nyeti ambako wahusika wanakusanya fedha za mauzo, lakini hawawezi kuboresha miundombinu ya vyoo vyao.

Unakuta nyumba yenye wapangaji ‘kibao’ lakini choo kinachotumiwa ni duni na kichafu. Unabaki kujiuliza, inawezekanaje mwenye nyumba anapokea kodi lakini bado hawezi kuboresha mazingira ya eneo hilo nyeti?.

Katika mitaa tunayoishi, tunashuhudia baadhi ya familia zenye vyoo duni, zikidiriki kutiririsha maji machafu barabarani.

Wakati mwingine, majirani huingia migogoro kutokana na mmoja kutiririsha maji machafu kwake au choo kuleta usumbufu wa harufu kwa mwingine.

Laiti kama mamlaka za ukaguzi zingekuwa zikionekana, ina maana kero hizo zingezungumzwa na hatua zikachukuliwa kwani mambo haya yapo wakati wote na hayana udhibiti wala ufuatiliaji wa kutosha. Hapo ndipo huwa najiuliza, ziko wapi mamlaka na hasa Maofisa Afya?.

Mathalani, katika eneo ninaloishi, sijawahi kuona ofisa afya wala kushuhudia mamlaka za ukaguzi kwa ajili ya kushauri au kuchukua hatua kwa wanaochafua mazingira.

Matokeo yake, licha ya baadhi ya wananchi kukerwa na uchafu unaofanywa na baadhi, hushindwa kwenda kuripoti wenzao kwa kuogopa kuingia migogoro.

Kwa muktadha huu, agizo la Waziri Mwalimu alilolitoa hivi karibuni kwa maofisa afya ni muafaka.

Amewaagiza maofisa hao kusimamia kwa ukamilifu usafi wa mazingira katika jamii kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Alikuwa akizindua taarifa ya Utafiti wa Viashiria vya Ugonjwa wa Malaria wa mwaka 2017 jijini Dar es Salaam.

Namnukuu: “Nawaagiza Maofisa Afya, badala ya kupoteza muda mwingi wa kukagua migahawa, bucha za nyama na sehemu ambazo wanajua zinaleta fedha, tunataka pia wajikite katika kusimamia usafi wa mazingira katika Kata, Vijiji na Mitaa yetu.”

Kutokana na agizo hili, ni wakati wa maofisa afya kujitafakari na kujitathimini kama kweli wanaingia mitaani kutekeleza wajibu huo au ni maofisa wa ofisini pekee?.

Inawezekana kama alivyosema Waziri Mwalimu, wao mitaa wanayoifahamu ni kwenye maeneo ya biashara pekee lakini katika maeneo ya makazi wameyakinga kisogo wakiacha watu wajiendeshe watakavyo.

Katika hilo la kutembelea maeneo pasiwapo sababu zozote za kuhalalisha vitendo vya maofisa afya kukaa ofisini au kuchagua baadhi ya maeneo ya kukagua. Iwe ni uhaba wa vitendea kazi au ukubwa wa maeneo, hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha uchafu kwenye maeneo na baadaye kuingiza jamii na taifa kwa ujumla kwenye hasara ya kutibu magonjwa yatokanayo na uchafu.

Inafahamika wazi kuwa magonjwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, kutapika, maambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI) na hata magonjwa ya ngozi huchangiwa na uchafu wa mtu binafsi na mazingira.

Matokeo yake, watu hutumia fedha nyingi na muda kuyatibu badala ya kufanya shughuli za maendeleo. Naunga mkono na kupongeza agizo la Waziri Mwalimu kwamba mabaraza yote ya halmashauri nchini yaweke sheria na adhabu kali kwa wote ambao wamekuwa wagumu kushiriki usafi wa mazingira.

Sambamba na sheria na adhabu kali, pia maofisa afya wazembe, wanaofanya kazi kwa mazoea wamulikwe na kuchukuliwa hatua.

Natamani kuona uchafu mitaani ikiwamo vyoo duni, wanaotiririsha maji machafu mitaani, unageuka jipu la kuwatumbua maofisa afya wasiotimiza wajibu kuukomesha.

Maofisa afya wanapaswa waonekane mitaani kukagua na kuchukua hatua dhidi ya wachafuzi wa mazingira na si kukaa ofisini au kuchagua maeneo fulani ya ukaguzi yenye ‘maslahi’ wanayoyajua wao.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi