loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bunge laomboleza kifo cha Dk Mengi

BUNGE limeomboleza kifo cha mmiliki wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi kilichotokea juzi likimkumbuka kwa mambo mengi aliyofanya ikiwamo msaada wa Sh milioni 50 aliotoa hivi karibuni kwa wabunge.

Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwasilisha salamu jana bungeni kabla ya kuanza kipindi cha maswali na majibu katika kikao cha 20 cha mkutano wa 15 unaoendelea mjini hapa. Miongoni mwa mambo ambayo mfanyabiashara huyu maarufu nchini anakumbukwa kuyafanya, ni pamoja na moyo wake wa utoaji wa misaada ya kijamii ikiwamo hivi karibuni alipochangia Sh milioni 50 kuunga mkono mradi uliobuniwa na wabunge wanawake (TWPG) wa kujenga vyoo vya mfano kwa mtoto wa kike katika majimbo.

“Katika kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa, sisi bunge tunaungana na mheshimiwa Rais John Magufuli, familia ya marehemu na watanzania wote tukimshukuru Mwenyezi Mungu na tuki mshukuru Mengi kwa mchango wake mkubwa usiopimika kwa watanzania,” alisema Ndugai.

Alisema kwa miaka mingi, Mengi alijulikana kwa utoaji mkubwa wa misaada ya kijamii ikiwamo ujenzi wa misikiti, makanisa, kwa masikini na wasiojiweza, wanyonge na wenye ulemavu. Vile vile alisaidia katika matibabu kwa magonjwa mbalimbali ikiwamo magonjwa ya moyo. Alisema Mengi alikuwa ni Mtanzania ambaye kwa bidii, juhudi na maarifa aliweza kukua kiuchumi kutoka maisha duni ya kijijini hadi kufikia kuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini, Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Ndugai aliendelea: “Tutamkumbuka daima kwa jinsi alivyosaidia hifadhi ya mazingira hasa maeneo yanayozunguka mlima Kilimanjaro kwa kupanda miti mingi sana kwa mabilioni bila kuchoka.”

Alikuwa mmiliki wa vyombo mbalimbali vya habari vikiwamo redio, televisheni na magazeti kadhaa; alikuwa mmiliki wa viwanda”. Alimtaja Mengi alikuwa kiongozi wa umma kwa kuwa kiongozi wa bodi mbalimbali na taasisi nyingine nyingi binafsi na za umma.

Aliwahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Mazingira (NEMC), mwenye kiti wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA); Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids); Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) na nyadhifa nyingine nyingi. Mengi ambaye alizaliwa mwaka 1942 mkoani Kilimanjaro, alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa Dubai katika Falme za Kiarabu.

MGOMBEA urais  wa Zanzibar aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi