loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mengi anaendelea kuishi

VYOMBO vya habari vimetawaliwa na habari kuhusu kifo mfanyabiashara maarufu nchini, Dk Reginald Mengi.

Sauti za maombolezo zinasikika kila pembe ya nchi.

Zinamlilia mmiliki huyu wa Makampuni ya IPP. Taasisi na makundi mbalimbali ya watu yanakumbuka mema na mchango wake.

Wanatasnia ya habari ni miongoni mwa waombolezaji wake wanaoshuhudia mchango wake katika kusimamia maendeleo ya tasnia.

Ni mwandishi gani asiyetambua nafasi na mchango wa Dk Mengi katika tasnia? Sidhani kama yupo asiyefahamu kwamba alikuwa miongoni mwa waajiri wakubwa katika sekta ya habari. Licha ya kwamba Mengi alikuwa mwekezaji katika maeneo mengine tofauti tofauti, kwa upande wa sekta ya habari ameacha pengo kubwa.

Jukwaa la Wahariri (TEF) kupitia kwa Katibu wake, Neville Meena linakiri kifo cha Mengi ni pigo kwa tasnia. Ni pigo ambalo naamini wapo (wengi) wanaojiuliza kama vyombo vyake vya habari vitaendelea kusimama, kuajiri na kutoa huduma iliyotukuka?

Dua na maombi ni kuona televisheni, redio na magazeti yake yakiendelea kufanya kazi. Hata hivyo, waandishi wa habari ni sehemu ndogo ya watu wa kada tofauti wanaomlilia mfanyabiashara huyu.

Hata Rais John Magufuli anakiri kwamba Mengi alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Ubalozi wa Marekani katika taarifa yake, unakumbuka mchango wake katika ukuaji wa muda mrefu wa uchumi na maendeleo ya Tanzania.

Waliowahi kunufaika na misaada mbalimbali ni kundi lingine lenye ushuhuda wa matendo makuu aliowafanyia katika maisha yao. Wanamlilia ‘msamaria’ wao.

Ni nani hakuwahi kushuhudia Dk Mengi akikabidhi misaada mbalimbali ikiwamo utaratibu aliokuwa amejiwekea wa kukutana na watu wenye ulemavu na kupata chakula nao?

Hata Bunge kupitia kwa Spika Job Ndugai , linakiri Mengi alikuwa na moyo wa utoaji. Wabunge wanakumbuka Sh milioni 50 walizopewa na mfanyabiashara huyu kuunga mkono mradi uliobuniwa na wabunge wanawake (TWPG) wa kujenga vyoo vya mfano kwa mtoto wa kike katika majimbo. Ndugai alisema mchango wa Mengi haupimiki kwa Watanzania.

Alijulikana kwa utoaji mkubwa wa misaada ya kijamii kwa masikini na wasiojiweza, wanyonge na wenye ulemavu hata ujenzi wa misikiti na makanisa.

Aidha, Mengi alikuwa kioo na mfano wa kuigwa katika suala zima la mapambano dhidi ya umasikini.

Spika Ndugai anamwelezea kwamba ni Mtanzania ambaye kwa bidii, juhudi na maarifa alikua kiuchumi kutoka maisha duni ya kijijini hadi kufikia kuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini, Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla. Kwa ujumla, watu wa kada mbalimbali wanaendelea kuibua mambo mengi mema ambayo Dk Mengi ameyatekeleza katika kipindi chote ambacho Mungu alimjalia kuishi hapa duniani.

Miaka 77 aliyoishi hapa duniani kabla ya kukumbwa na mauti kwa kiwango kikubwa ameitendea haki kwa kuacha alama. Katika kurejelea salamu za rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali, salamu za Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas zinakumbushia kauli aliyowahi kutoa Mengi. Kupitia ukurasa wake wa twitter, Dk Abbas anasema Mengi aliwahi kusema watu wanaoacha alama hawafi.

Kwa hiyo kulingana na vilio kutoka kila kona vinavyoshuhudia juu ya mambo mengi aliyofanya Mengi, ni dhahiri kwamba hajafa.

Kimwili ameondoka duniani lakini alama alizoacha kwa taifa na watu mbalimbali, zinaendelea kuishi.

Walionufaika, wakiwamo waliopewa misaada, ajira, hawataweza kusimulia maendeleo yao bila kutaja jila la Mengi. Hata taifa litaendelea kumkumbuka mfanyabiashara huyu kwa mchango wake katika uchumi.

Hata hivyo, Mengi ambaye taifa linaendelea kuomboleza kifo chake; ikumbukwe ni binadamu mwenye upungufu kama ilivyo kwa binadamu yeyote.

Baadhi ya maandiko matakatifu yanaweka bayana kwamba hakuna hata mmoja aliye mkamilifu. Sisi sote ni wenye upungufu (unaotofautiana).

Kwa muktadha huo, kila mtu kwa nafasi yake, atumie mema ya Mengi kama somo la kuandika alama katika maisha ya watu wengine.

Kwa kufanya hivyo, kifo kitakapofika, ataendelea kuishi mioyoni mwa walinufaika. stella.nyemenohi@tsn. go.tz

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi