loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jifunze kwa aliyoacha Dk Mengi

LEO ndio siku ya maziko ya bilionea mzalendo nchini na Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi, aliyefariki dunia Mei 2 mwaka huu, baada ya kuugua muda mfupi akiwa nchini Dubai.

Ukweli ni kwamba tangu kutokea kwa msiba huo, Tanzania imezizima kwa simanzi kutokana na nafasi kubwa aliyokuwa nayo mfanyabiashara huyo, ambaye pamoja na kuchangia uchumi wa taifa, lakini pia alitoa ajira na kusaidia wengi waliokuwa na shida.

Msiba huo kwa siku kadhaa sasa, umekuwa gumzo, si kwenye vyombo vya habari vya magazeti, televisheni na redio pekee, lakini hata vyombo vya habari vya kisasa kama blogu, televisheni za mtandao na mitandao mingi ya kijamii.

Kupitia vyombo hivyo, kila kona ya nchi watu wameonesha kuguswa na msiba huo. Viongozi mbalimbali wamejitokeza kila mmoja kwa nafasi yake akielezea namna nchi imepata pigo na pengo kutokana na kifo cha Dk Mengi.

Wapo viongozi waliotoa ushuhuda wa namna walivyosaidiwa na mfanyabiashara huyo hadi kufika hapo walipofika.

Wapo walioelezea namna alivyojitoa kusaidia wenye mahitaji na hata alivyochangia katika shughuli za maendeleo.

Ni wazi kuwa Dk Mengi pamoja na kwamba alikuwa ni mchapakazi katika kjitafutia riziki hadi kufikia hatua ya kuitwa bilionea, lakini pia alifahamu umuhimu wa kujitoa kwa jamii iliyomzunguka.

Na hilo limejihidhirisha katika msiba wake huu, ambao kila mwili wake unapopitishwa kuanzia Dar es Salaam, ulipotua kutoa Dubai, Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro ulipowasili kwa ajili ya mazishi, watu wengi wamejitokeza bila kuficha hisia zao na kumlilia.

Katika maeneo yote mwili huo ulikopita, wananchi walijaribu kuonesha hisia zao ikiwemo kumwagia maua gari lililobeba mwili wa mfanyabiashara huyo, kutandika kanga barabarani na hata kufagia njia.

Mengi ameacha simanzi kubwa kwa watanzania kutokana na mchango wake katika jamii. Kusema ukweli ameacha alama kubwa, inayoendelea kukumbukwa.

Hivyo basi, wakati leo bilionea huyo akienda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele, watanzania wasikubali sifa zote na yale yote mema aliyoyafanya na kujenga jina lake katika jamii, azikwe nayo.

Ni wakati sasa wa wale walio karibu naye, wananchi, viongozi na wafanyabiashara wakiwemo mabilionea waliopo nchini, kuyaishi kwa vitendo matendo mema ya mfanyabiashara huyo.

Jambo kubwa analoliliwa na ataendelea kuliliwa bilionea huyo ni namna alivyokuwa mstari wa mbele, kushiriki katika masuala ya maendeleo ya nchi yake, kupenda kujaribu na pia kusaidia wale wenye mahitaji wakiwemo watu wenye ulemavu.

Hata kitabu chake cha I CAN, I MUST na I WILL, kimeacha funzo kubwa kwa watanzania, kujifunza kwa yale aliyopitia hadi kumfikisha hapo alipofikia hadi kifo chake.

Kitabu kile kinapambanua wazi kuwa kila mtu anaweza kufanikiwa, kama tu atajituma, atathubutu na pia kuwa karibu na watu wa aina zote, bila kubagua hali zao za kipato, itikadi, dini wala kabila.

Dk Mengi amefariki na kuacha majonzi makubwa nyuma na pengo ambalo halitazibika, isipokuwa tu pale nyendo na matendo yake zitakapoenziwa na kila mpenda maendeleo yake binafsi na taifa kwa ujumla.

Nenda mzee Mengi nenda. Nenda Mwenyekiti wa IPP, umemaliza mwendo wako na kutuachia mambo mengi.

Ni wakati wetu sasa kuenzi uliyotuachia na sisi kutengeneza historia yetu, kama yako uliyoatuachia. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake Mzee Mengi mahali pema peponi Ameni.

SERIKALI ya Rais John Magufuli tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi