loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tupaze sauti kuzuia ajali

UZI Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu ni ‘Paza Sauti, Zuia Ajali, Okoa Maisha’.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika mikoa tofauti huku kukiwa na makongamano mbalimbali yaliyoshirikisha wadau wa masuala ya usalama barabarani ambayo yote yalikuwa yakiendana na kaulimbiu hii mpya pamoja na kujadiliana mikakati mipya ya kukabiliana na janga la ajali.

Kaulimbiu hii ni jumuishi kwa kuwa inatoa jukumu kwa kila mwanajamii kuchukua hatua katika kuzuia ajali hasa inaposema paza sauti inagusa kila mtu kuzungumza, kukemea, kukaripia na hata kupiga kelele zitakazosaidia kukabiliana na ajali.

Sauti hizo zikipazwa zinaweza kwa kiasi kikubwa kuzuia ajali na mwishowe kuokoa maisha.

Binafsi nimeguswa na kaulimbiu hii na pia nia dhahiri iliyooneshwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyolenga kuitekeleza kaulimbiu hii kwa vitendo.

Hii ni hatua kubwa na inatoa mwanga mpya zaidi katika uwepo wa mazingira bora ya usalama barabarani kwa kuwa utaleta sheria mpya zinazoendana na na wakati dhidi ya zile za zilizopo kwenye Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ambazo zimepitwa na wakati.

Baadhi ya mambo yaliyopo kwenye sheria hiyo ni pamoja na mwendeshaji wa pikipiki ndiye anapaswa kuvaa kofia ngumu wakati wa matumizi ya chombo hicho huku abiria yeye hajatajwa.

Lakini pia hata kwenye watumiaji wa magari hasa yale binafsi abiria anayekaa kiti cha mbele na dereva ndio wametajwa kuwa wanapaswa kuvalia mikanda ya gari lakini abiria wa viti vya nyuma hawajatajwa kuwa wanapaswa kuvaa mikanda hiyo.

Hizo ni baadhi ya sheria za kizamani zisizoendana na mazingira ya sasa ambazo zimekuwa ni kero hasa kwa wasimamia sheria ambao wanashauri kuwapo kwa sheria ambazo zinawawezesha kuzisimamia na kukabiliana na kila kisababishi cha ajali.

Ninasema kuwa nia ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya kuingiza muswada huo kwenye bunge lijalo inaashiria nia ya dhati ya serikali katika kukabiliana na janga hili.

Ni imani yangu kuwa muswada huo utaingizwa na kujadiliwa na kisha mapendekezo husika yaliyotolewa na wadau kufanyiwa kazi hasa kwa yale ambayo hayakuguswa kabisa kwenye sheria hiyo mfu lakini kwa mazingira ya sasa ni muhimu kuingizwa.

Nitafurahi zaidi kuona muswada huo umejadiliwa hadi kufikia hatua ya kupelekwa kwa Rais John Magufuli na kisha kusainiwa na kuwa sheria mojawapo kati ya mambo hayo ni adhabu kuwa sheria.

Naamini sheria hii mpya za kuwabana watu wanaosababisha ajali ili kutokomeza uzembe na pia kuacha tabia kuendesha vyombo vya moto wakiwa wanazungumza na simu za mkononi.

Kwa kuwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau ambayo yatakuwapo kwenye muswada huo yamependekeza na adhabu kwa watakaokutwa na makosa, basi ni hakika kuwa dawa na ajali za barabarani inakuja kupatikana.

Kama kuanzia Januari mosi hadi Machi mwaka huu waliopoteza maisha kutokana na ajali za barabarani ni 335 huku majeruhi wakiwa 735 hiyo ni idadi kubwa ya vifo ambavyo vimeondoa nguvu kazi kubwa ya watu huku wengi wakiachwa kuwa majeruhi.

Ifahamike kuwa wakati ajali nyingine zikiwa zimetokea kwa bahati mbaya ila kuna ambazo zinatokana na uzembe ambazo hakika sheria hii mpya itadhibiti uzembe wa aina hiyo kutokana na adhabu kali zitakazotolewa. Mungu bariki mchakato mzima wa upatikanaji wa sheria mpya ya usalama

SERIKALI ya Rais John Magufuli tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi