loader
Picha

Waziri apongeza ushirikiano wa TSN na GSI Tanzania

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ameipongeza kampuni inayojihusisha na utoaji wa huduma za msimbomilia (barcodes) GS 1 Tanzania kwa kuwezesha bidhaa nchini kutambulika kimataifa na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa taasisi zote zinasimamia ubora na viwango wa bidhaa nchini.

Katika hatua nyingine, Kakunda amepongeza makubaliano yaliyoingiwa baina ya kampuni hiyo na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo ambayo yatawezesha kupeleka elimu ya msimbomilia kwa wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya kampuni hiyo pamoja na utiaji saini wa makubalino na TSN, Waziri Kakunda alisema kuanzishwa kwa Kampuni ya GS 1 Tanzania kumesaidia kuleta mafanikio makubwa kwa Taifa hususani katika jumuiya ya wafanyabiashara.

Alisema awali kabla ya ujio wa kampuni hiyo, wafanyabiashara walilazimika kwenda hadi nje ya nchi hususani katika mataifa ya Kenya, Afrika Kusini na Ubelgiji ili kupata huduma hiyo, suala alilosema kuwa lilikuwa likiwasababishia usumbufu kwa kiwango kikubwa.

Alisema pamoja na changamoto iliyokuwa ikiwakuta wao na bidhaa wanazozizalisha kukosa kutambulika katika mifumo ya kimataifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), pia ilichangia kutokukua kwa makampuni madogo na ya kati hatua iliyosababisha bidhaa zinazozalishwa na kampuni hizo kushindwa kuingia katika maduka makubwa ya kisasa sanjari na serikali kukosa mapato.

“Ni jambo la kujivunia kwa sasa kuona Tanzania ni miongoni mwa nchi Barani Afrika iliyoingia katika utaratibu huu wa Barcodes na kuungana na nchi zingine za Algeria, Misri, Ivory Coast, Kenya, Libya, Mauritius, Morocco, Nigeria na Afrika Kusini, hatua hii ni muhimu kwa maendeleo katika Sekta ya Biashara na Taifa kwa ujumla,” alisema Kakunda.

Pia aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kote kuhakikisha wanaongeza thamani kwa kusajili bidhaa zao na huduma hiyo ili kujitanua kimataifa sambamba na kujiongezea kipato.

Kuhusu ushirikiano na wa GS 1 na TSN, Waziri Kakunda alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuwasambazia elimu wananchi nchini kote juu ya umuhimu wa kuwa na alama za msimbomilia katika bidhaa zao tofauti na ilivyo sasa ambapo wananchi wengi bado hawana uelewa juu ya suala hilo.

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa kujengwa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi