loader
Rais aidhinisha hifadhi mpya tatu

Rais aidhinisha hifadhi mpya tatu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Rais ameridhia hifadhi tatu mpya kuingizwa katika orodha ya Hifadhi za Taifa.

Alibainisha hayo jana wakati akihitimisha na kujibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika hotuba yake ya makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

“Hapa nina hati kutoka kwa Rais, ameridhia hifadhi mpya tatu kuingia katika orodha ya hifadhi za taifa,” alisema na kuzitaja hifadhi hizo mpya kuwa ni Hifadhi ya Burigi Chato, Hifadhi ya Rumanyika Karagwe na Ibanda Kyerwa. Katika hatua nyingine, Waziri Kigwangalla amesema biashara ya kuuza wanyama hai nje imefungwa na haitafanyika tena hata awe mnyama mdogo wa aina gani.

“Biashara hii ya kuuza wanyamapori hai nje ya nchini haitafanyika tena, imefungwa, kama bado mimi ni waziri katika wizara hii nimeifunga na sitaifungua na haitafanyika kamwe, hata awe chawa…haijalishi mnyama ana ukubwa gani,” alisema. Alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Mbunge wa Muheza Adadi Rajabu.

Akichangia mada Msigwa aliomba biashara ya kuuza wanyamapori hai irejeshwe kwa kile alichodai waliokuwa wakifanyabiashara hiyo wameingia katika umasikini na wengine kupoteza maisha kutokana na kukosa biashara wakati Adadi akichangia hoja alitaka biashara ya kuuza vipepeo nje ya nchi iruhusiwe.

“Hakuna mnyama hai akayetoka na kuuzwa nje ya nchi iwe kwa njia halali au la…naona Msigwa ananiangalia uniangalie tu vizuri, biashara hii imefungwa, hata Adadi pia alichangia lakini uamuzi ndio huo hakuna kipepeo au mnayama hai atatoka nje… kuna vipepeo wanapatikana msitu wa Amani, ni wa kipekee hakuna sehemu wengine tunaendelea kuboresha ili watalii wazaidi wafike kuangalia lakini pia kwenye maporomoko yaliyopo karibu na pale,” alisema.

Waziri Kigwangalla alisema kama kuna mtu anafuga wanyamapori wake basi afungue ‘Zoo’ watu waende wakaangalie kwenye hifadhi hizo binafsi, lakini hakuna biashara ya kununua wanyama hapa nchini na kuuzwa nje ya chini hata awe mdogo kiasi gani. Awali wakichangia hoja ya wizara hiyo wabunge walisema utalii ni biashara kubwa, hivyo serikali inatakiwa kutafuta namna ya kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo badala ya kupoteza muda katika kutatua migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.

Pia wameitaka serikali kujipanga na kuangalia namna ya kupunguza tozo nyingi ambazo walieleza zimekuwa kikwazo katika sekta hiyo muhimu nchini ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya kigeni kwa asilimia 25.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ni nyeti na inahitaji uwekezaji mkubwa, lakini imekuwa ikicheleweshwa na migogoro ya muda mrefu kati ya mamlaka ya hifadhi na wananchi. “Tumekuwa badala ya kufanya biashara ya utalii ni kutatua migogoro tu, tuseme sasa inatosha tufanye biashara kwa kupata suluhisho la kudumu... tuichukulie biashara ya utalii kwa upeo wa kibiashara zaidi kama wenzetu katika nchi nyingine wanavyofanya na tutajiingizia mapato zaidi ya tunayopata sasa,” alisema Msigwa na kuongeza kuwa serikali iangalie haraka mipaka na kumaliza kabisa suala la migogoro ya ardhi.

Msigwa pia alizungumzia kukinzana kwa sheria mbali mbali na kusababisha utekelezaji wake kuwa mgumu na kukwamisha mazingira ya kuvutia biashara ya utalii. “Wizara hii inategemewa kuleata mapato, acheni urithi, tunaona kuna sehemu ya kazi inafanyika na mawaziri waliopo sasa... mkiendelea kazi hii nzuri, tutaondokana na hali ya kufukuzana fukuzana katika wizara hii nyeti,” alisema mbunge huyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema), alisema sekta ya utalii imekuwa ikichangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa, lakini imekuwa haichukuliwi kwa umakini na kutaka serikali kujipanga kwa kutegemea fedha zake za ndani badala ya wadau wa nje ili kuiingua sekta hiyo.

Owenya pia alizungumzia kodi ambazo alizielezea kuwa ni nyingi na kutoa mfano kwenye hoteli wamekuwa wakitozwa kodi na Osha Sh milioni 1.5, Cosota kodi sh milioni 1.5, Nemc Sh milioni 1.5 na taasisi zingine na kuhoji tozo hizo zote fedha zake zinapelekwa wapi na zinafanyia kazi gani ya kumfaidisha mfanyabiashara wa hoteli. Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema anaona kodi ya wizara hiyo ni ndogo na kupendekeza serikali iache maduhuli ya wizara hiyo angalau kwa miaka mitano ili watumie kuendelea kuboreshea wizara ili iweze kufikia mafanikio makubwa zaidi na kuliingizia taifa kipato. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alichangia alisema tozo zimekuwa nyingi kwa wadau wa utalii na kuwa sekta hiyo haiwezi kuendelea kwa kujaza matozo kwenye biashara ndio maana hazikui. Aliitaka wizara hiyo kuwa na mbinu za kuutangaza utalii wa Tanzania na kutoa mfano wa Malaysia imekuwa ikipata watalii milioni 25 kwa mwaka na kuwa wamekuwa wakitumia vitu vya kawaida tu kutangaza utalii wao. Wizara ya Maliasili na Utalii imeomba iidhinishiwe na Bunge Sh 120, 202,638, 734 kwa matumizi ya wizara, na kati ya fedha hizo, Sh 71,312, 649,000 ni matumizi ya kawaida na Sh 48,889,988, 734 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ad0255ac8103536cc8237a8094082098.png

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi