loader
Picha

Wabunge; sheria kuzuia simu barabarani inahitajika

SHIRIKA la Afya Dunia (WHO) linasema, kila sekunde 24 duniani, mtu mmoja hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani. Idadi ya vifo vitokanavyo na ajali kila mwaka vimeongezeka kutoka watu milioni 1.24 mwaka 2016 hadi watu milioni 1.35 mwaka 2018.

Ripoti iliyotolewa na WHO hivi karibuni kuhusu Hali ya Usalama Barabarani Duniani, inasema kuna vifo 27 kwa kila watu 1,000. Hata hivyo, vinatajwa visababishi vikuu vitano vya ajali duniani kuwa ni pamoja na makosa ya kibinadamu, sababu za kimazingira, ubovu wa miundombinu na vyombo vya moto.

Vipo viashiria kadhaa vya ajali na ongezeko la madhara ya ajali za barabarani ambavyo ni pamoja na mwendo wa kasi, ulevi kwa madereva, matumizi duni ya mikanda kwa abiria na vizuizi kwa watoto, ukosefu wa matumizi sahihi ya kofia ngumu na zenye viwango. Hata hivyo, kiashiria na kisababishi kingine cha ajali kinachopigiwa kelele ili kiingie katika marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani yanayopendekezwa ni matumizi ya simu barabarani kwa madereva na waenda kwa miguu hasa wanapovuka barabara.

Wadau wa Mtandao wa Wadau kutoka Asasi za Kiraia unaotetea Marekebisho ya Sheria na Sera ihusuyo Usalama Barabarani nchini wanasisitiza jamii kuungana na watunga sera na sheria kujua na kuzingatia umuhimu wa kurekebisha Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 ili itamke kuwa, ni kosa kwa dereva au mwenda kwa miguu kuvuka barabara huku akitumia simu.

Kwa mujibu wa Ofisa Programu wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) ambao ni taasisi wadau wa mtandao huo, Mackphason Buberwa, endapo mapendekezo waliyotoa baada ya uchambuzi wa sheria na kuyakabidhi kwa Serikali na Bunge yatafanyiwa kazi ipasavyo na kwa haraka, ajali hazitatokea na hata Rais Magufuli atapumzika kutuma salamu za rambirambi kutokana na vifo vya ajali.

Hata hivyo anasema, mapendekezo hayo mintarafu sheria kuzuia matumizi ya simu kwa madereva na waenda kwa miguu wanapovuka barabara, yanaonesha dalili nzuri kwani yamepokelewa vizuri na Serikali na Bunge. Anasema kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polosi, miongoni mwa sababu za ajali kwa waenda kwa miguu ni matumizi ya simu za mkononi ama kwa kujipiga picha, kutuma na kusoma meseji, au kutafuta namba za mtu wakati anavuka barabara.

“Tunatambua juhudi za Jeshi la Polisi katika kupambana na ajali na kwamba, wamekuwa wakijitahidi kuelimisha umma dhidi ya matumizi ya simu barabarani kwa madereva na wanaovuka barabara,” anasema Markphason. Hata hivyo anasema ipo changamoto kwamba, vyombo vingine hasa magari vina teknolojia ya simu kuingia na kusikika kupitia redio bila dereva kushikilia simu hivyo, siyo rahisi kubaini kama kweli dereva ametumia simu au la.

Anatoa suluhisho akisema: “Ukifika wakati, tunaweza kutumia kamera kama za kupima spidi, zikaboreshwa na kuwekewa teknolojia ya kubaini kama dereva anatumia simu…” Kwa mujibu chapisho liitwalo, ‘Road Safety in the African Region, 2015’ la WHO lililotolewa mwaka 2016, nchi nyingi za Afrika zikiwamo za Algeria, Chad, Congo, Ethiopia, Gabon, Ghana, Togo, Senegal na Uganda zinayo sheria maalumu dhidi ya matumizi ya simu kwa madereva.

Katika nchi hizo, sheria hiyo inazuia matumizi ya simu kwa madereva wanapoendesha gari ama kwa kushikilia simu, au kwa sauti ya juu bila kushika simu yaani ‘hands free phones.’ Anasema: “Wananchi wanapaswa kutambua jukumu lao kujilinda na kwamba, ni kosa na hatari kubwa kutumia simu wakati unavuka barabara…” Anaongeza: “Ndiyo maana wakati mwingine mtu anatembea huku anachati matokeo yake, watu wanagongana barabarani au mwingine anaacha njia yake na kwenda upande wa magari na matokeo yake, inakuwa ni ajali… hata katika vivuko vya waenda kwa miguu umakini unahitajika sana.”

HALI ILIVYO

Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, matumizi ya simu za mkononi yanazidi kuongezeka nchini na duniani kote. Simu zinatajwa kuchangia kuwapo kwa ajali za barabarani.

Ripoti ya robo ya nne ya mwaka inayoishia Desemba 2017 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaelezwa idadi ya wamiliki wa simu za mkononi nchini imeongezeka maradufu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imeongezeka kutoka milioni 27.62 mwaka 2012 hadi takriban milioni 40 sasa samaba.

Ongezeko la watumiaji wa simu hizo limeteka akili za watumiaji wengine kiasi cha wengine kuvuka barabara huku wakitumia simu zao hali iliyowafanya wengi kugongwa na gari, pikipiki au baiskeli na kufa au kupata majeraha. Hata katika nchi nyingine duniani ikiwamo Marekani, vyanzo mbalimbali vinasema kuna ongezeko kubwa la vifo vya watembea kwa miguu kutokana na ajali za barabarani, simu za mkononi zikitajwa kuwa chanzo.

Chapisho moja linasema: “Watu hupata ajali kutokana na kutumia simu zao wakati wakitembea pembezoni au wakivuka barabara na huku madereva nao husababisha ajali kutokana na matumizi ya simu zao wakiwa wanaendesha.”

Mmoja amenukuu mtandao wa Edgarsnyder.com unaonukuu ripoti ya Baraza la Usalama la Taifa nchini Marekani linalosema kuwa, matumizi ya simu ya mkononi barabarani husababisha ajali zipatazo milioni 1.6 kila mwaka, watu 390,000 hujeruhiwa.

“Ajali moja kati ya nne nchini humo husababishwa na madereva wanaochati wakiwa wanaendesha magari yao,” anasema. Inaelezwa kuwa, matumizi ya simu barabarani huongeza uwezekano wa dereva kusababisha ajali mara sita zaidi, kwani kuchati huhamisha mawazo ya mhusika. Kwa mujibu wa mtandao huo, madereva wapatao 660,000 hutumia simu za mkononi wakiwa wanaendesha barabarani, kusoma ujumbe mfupi wa maandishi, barua pepe, simu au maombi mengine ya simu, hivyo kuongeza hatari ya uwezekano wa kusababisha ajali.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma katika Kitengo cha Usalama Barabarani katika makao makuu ya Polisi, Mrakibu wa Polisi (SP), Abel Swai anasema, matumizi ya simu za yanaweza kuathiri tabia ya dereva, hususani kuhusu kazi za mikono yake hisia pamoja na maamuzi barabarani. Anasema: “Kitendo cha kupiga simu kinaathiri uwezo wa dereva kuendelea kubaki barabarani inavyotakiwa… Simu zinapokonya maamuzi ya busara ya dereva hasa anapopata habari mbaya au njema zaidi kwake.”

SP Swai anasema: “Chukulia dereva upo kwenye mteremko simu inaingia, na wewe unapokea au kusoma sms unakuta taarifa kama vile timu yako imefunga timu pinzani; Simba au Yanga, magoli saba, kwa wale mashabiki damudamu atakuwa wapi?” Anaongeza: “Au unaambiwa mama, baba, mtoto, mume au mke amefariki hali itakuwaje! Hapo ni rahisi kushituka na kujikuta mguu umeachia breki na pengine, bila kutarajia ukakanyaga zaidi mafuta sehemu unayopaswa kukanyaga breki.”

Swai anasema utafiti katika maeneo mbalimbali unaonesha kuwa, matumizi ya simu kwa dereva au mwendesha pikipiki, huathiri ufanisi wa dereva na kuupunguza kwa kiasi kikubwa hasa katika kuendesha kwa spidi inayotakiwa sambamba na kufanya maamuzi sahihi kama kuweka umbali sahihi kati ya gari lake la mbele au la nyuma.

Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Morogoro, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Michael Deleli anasema: “Dereva yeyote makini hawezi kutumia simu wakati anaendesha chombo cha moto na roho za watu ama awe kwenye gari, au pikipiki.” SSP Deleli anasema: “Ingawa yote ni makosa yanayohatarisha maisha ya watu, ni afadhali dereva anayepokea simu iliyoita na kuzungumza huku anaendesha, kuliko anayechati au kutafuta jina na namba wakati anaendesha japo wote wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ajali.”

Wataalamu hao wa usalama barabarani wanasema, matumizi ya simu huharibu umakini na uzingatiaji (concentration) wa madereva katika kazi yao na hupunguza uoni kwa kuwa mara nyingi macho ya dereva yatakuwa kwenye kioo cha simu na siyo barabarani. Inaelezwa kuwa, dereva anayetumia simu wakati anaendesha anakuwa katika hatari ya kupata ajali mara nne zaidi ya dereva asiyetumia simu wakati anaendesha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amewahi kunukuliwa akikiri kuwa, matumizi ya simu za mkononi barabarani hasa kwa waenda kwa miguu na madereva wa magari na pikipiki wanapokuwa barabarani. Kamanda Muroto anasema: “Kuchati kunawaponza wengi, unakuta mtu anatembea barabarani, anavuka huku akiwa anaendelea ku-chart’ au unakuta ni dereva anaendesha na wakati huo huo ana-chart, matokeo yake ni ajali.” Kwa mujibu wa Chama cha Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) Tanzania, kila mtu ajiulize kuna sababu gani kutumia simu huku unaendesha.

Ajiulize je, facebook, meseji, instagram, twiiter, na whatsapp haziwezi kusubiri hadi usimame!

MAREKEBISHO YA SHERIA YANAHITAJIKA

Ripoti ya Masuala ya Usalama Barabarani iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2018, inaeleza Tanzania haijaweka sheria madhubuti kudhibiti matumizi ya simu za mkononi barabarani.

Wadau mbalimbali wa usalama barabarani ukiwamo Mtandao wa Wadau kutoka Asasi za Kiraia unaotetea Marekebisho ya Sheria na Sera ihusuyo Usalama Barabarani nchini wakiwamo wabunge ambao ndio watunga sheria pamoja na watunga sera, hawana budi kuuona umuhimu wa haraka wa kurekebisha Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 ili itamke katazo la dereva yeyote ama awe wa gari la abiria, au gari la binafsi, mwendesha pikipiki, mpanda baiskeli au mwenda kwa miguu anayevuka barabara kutumia simu ama kwa kuzungumza, kutafuta namba au jina, kuchati au kujipiga au kutazama picha hadi mhusika anaposimama na kutulia.

Mratibu Mradi wa Usalama Barabarani wa Tamwa, Gladness Munuo, anasema sheria haisemi kitu kuhusu matumizi ya simu kwa madereva na japo ni miongoni mwa visababishi vya ajalli. Gladness anasema: “Kutumia simu wakati unaendesha ni hatari maana hujui ujumbe unaopewa utakupa tahadhari, au taharuki… Ni vema sheria iwe wazi ili mtu atumie simu kupiga au kupokea atakaposimama.”

Ifahamike kuwa, matumizi ya simu barabarani yanatufanya tusione alama za barabarani, tusione taa nyekundu, yanaufanya ubongo ulegeze mguu kwenye peda za breki au ukandamize zaidi peda za kuongeza mwendo na yanatufanya tujisahau tunapoendesha. Kadhalika, simu zinafanya tusione ishara za maelekezo kutoka kwa askari wa sulama barabarani.

jJukumu la kuelimisha umma mintarafu usalama barabarani dhidi ya matumizi ya simu na mengine muhimu lisiachwe kuwa sula la jeshi la polisi pekee, bali wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa kulifanya kuwa agenda ya kudumu katik kila mkusanyiko. Watunga sera na wanasiasa katika ngazi mbalimbali wajue kuwa, ni wajibu wao mkubwa kuhakikisha popote walipo, wananchi wanakuwa salama kwani mwananchi anapofariki dunia, anakuwa amefariki mpigakura.

“MKAKATI mzuri nilio nao kukabiliana na ugonjwa wa corona ni ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

2 Comments

 • avatar
  Hamadi Shomari
  30/05/2019

  0757566668

 • avatar
  Hamadi Shomari
  30/05/2019

  0757566668

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi