loader
Samatta apewa mtaa Temeke

Samatta apewa mtaa Temeke

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza moja ya mitaa ya Manispaa ya Temeke ipewe jina la nahodha wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Samatta anayecheza soka ya kulipwa KRC Genk ya Ubelgiji anakuwa mchezaji wa kwanza nchini kupewa jina la mtaa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Makonda alisema amelazimika kumpa mtaa Samatta kutokana na kuchambua mchango na juhudi zake katika soka.

Samatta amekuwa na msimu mzuri Ubelgiji ambapo mbali na timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya huko, ameibuka mchezaji bora wa Afrika katika ligi ya nchi hiyo na pia ameshika nafasi ya pili kwa ufungaji bora akipachika mabao 23, mabao mawili nyuma ya aliyetwaa kiatu cha dhahabu.

“Kwa kutambua mchango wa Samatta katika soka ya nchi hii tunampa mtaa kule kule kwao alipokulia Mbagala, ila kwa kutambua juhudi za Rais John Magufuli katika maendeleo anayoleta tunampa Samatta mtaa mzuri uliojengwa barabara ya lami, mitaro mizuri na taa za barabarani ili kuangaza dunia nzima ione kuwa Samatta ametoka wapi,” alisema.

Alisema mtaa huo utafunguliwa kabla Samatta hajaondoka na Stars kwenda kwenye michuano ya Afcon inayotarajiwa kufanyika Misri kuanzia Juni 21.

Alisema katika hafla ya kuutambulisha mtaa huo kutakuwa na viongozi mbalimbali na wachezaji wenzake wa Taifa Stars na wengineo atakaowaalika.

“Mchango wa Samatta katika Taifa hili kila mtu anautambua, hivyo nasi kama mkoa tumeona moja ya barabara kubwa zenye lami na taa itaitwa jina la Samatta,”alisema Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda jana alitimiza ahadi yake ya kutoa Sh milioni 10 kwa kipa wa Simba Aishi Manula na Sh milioni moja kwa wachezaji 10 waliong’ara kwenye tuzo za Mo Simba wiki iliyopita.

Makonda aliahidi kumpa fedha Manula kutokana na kufanya kazi nzuri kwenye mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Congo DR iliyofanyika Lubumbashi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f42ad73810632db55c5f33670e935a85.jpg

ZAIDI ya Vijana 25,000 kutoka ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi