loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mawasiliano watoa huduma, wagonjwa na ndugu yaboreshwe

TUNAKUBALIANA kwamba kuna maendeleo makubwa katika sekta ya afya nchini, kuanzia hospitali za chini hadi hospitali za rufaa.

Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma, kujenga vituo vya afya na kuweka vifaa mbalimbali vinavyohitajika maeneo muhimu kuanzia kwenye maabara hadi katika utabibu.

Kwa upande wa wataalamu, hatua kubwa imefikiwa ambapo kwa sasa idadi ya wataalamu wa afya, wakiwamo madaktari na wauguzi imeongezeka.

Hata hivyo, sekta ya afya bado ina changamoto nyingi hasa kwa upande wa watoa huduma hiyo binafsi.

Naamini serikali inalifanyia kazi suala hilo. Jambo lililonisukuma kuandika wazo hili ni changamoto ninayoiona kwa kipindi sasa katika mawasiliano kwenye hospitali nyingi kati ya watoa huduma, wagonjwa na ndugu wa wagonjwa.

Katika hospitali nyingi, bado wagonjwa na au ndugu zao wanajibiwa vibaya na baadhi ya watoa huduma, hawapewi maelekezo ya kutosha na wengine huishia kupotezewa muda wakitakiwa kusubiri visivyowezekana kusubiri, tena bila sababu za msingi.

Naishukuru serikali kwa sababu imefanya na inaendelea kufanya sehemu yake kwa kuboresha huduma lakini hilo la majibu yasiyostahili linalofanywa na baadhi ya wauguzi, madaktari na wahusika wengine katika hospitali mbalimbali ni la kitabia zaidi linalompasa kila mmoja wao kujitathmini, ikiwa anafanya kazi hiyo kwa wito au ilimradi.

Cha msingi ninachoshauri kwa upande wa serikali ni kuendelea kuwapa elimu ya namna ya kuwasiliana na wagonjwa wale wote wanaofahamika au wanaoweza kugundulika kuwa na tatizo hilo ili uboreshaji unaofanywa katika sekta ya afya ufanikiwe katika maeneo yote.

Ni vizuri wauguzi na madaktari wakakumbushwa mara kwa mara kuwa anayeugua tayari anakuwa na tatizo, hivyo kuhitaji faraja bila kujali ni wa kutibiwa na kuruhusiwa (OPD) au mgonjwa aliyelazwa.

Mawasiliano bora ni muhimu kati ya pande hizo tatu na haipendezi kuona daktari akiwasiliana na kompyuta iliyo mbele yake au karatasi na kumwambia mgonjwa ‘kamata hii uende maabara’ bila hata kumpa maelezo ya nini anadhani anapaswa kupimwa, huu ni mtihani katika hospitali nyingi. Wapo wagonjwa ambao wakiuliza ufafanuzi wa kilichoandikwa kwenye vyeti wanawaanzishia ugomvi, haipendezi.

Naamini mgonjwa ana haki ya kujua anachoumwa au ndugu yake kwa idhini ya mgonjwa ama kulingana na jinsi daktari anavyoona, lakini kama ni ugonjwa wa kawaida anaopaswa kuelezwa katika hali ya kawaida tu haifai kumzungusha au kumfanya ahisi ana ugonjwa ‘usiobebeka’ au kutibika, jambo linaloweza kumfanya akate tamaa.

Mawasiliano mengine yanayopuuzwa na madaktari au waandaaji wa wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji ni ya ama wale chakula baada ya muda wa kusubiri kufanyiwa operesheni kupita au la.

Imekwishatokea mara kadhaa wagonjwa waliolazwa wanaambiwa wasile kwa sababu muda wa operesheni umekaribia au siku ya operesheni iko karibu, lakini unashangaa zinapita siku hata mbili hakuna operesheni wala maelekezo kuhusu ruhusa au katazo jingine la kula.

Hii si sawa. Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Laurence Museru aliwahi kusema kuwa, pamoja na jitihada zinazofanywa kuboresha huduma za afya, watoa huduma wanarudisha nyuma jitihada hizo kwa kuwa na mawasiliano yasiyo mazuri na wagonjwa au ndugu wa wagonjwa.

WAKATI zikiwa zimebaki siku ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi