loader
Picha

Umeme wa Backbone unavyobadili hali ya viwanda mkoani Shinyanga

AZMA ya serikali ni kufi kia uchumi wa kati unaojengwa kwa kutumia viwanda ifi kapo mwaka 2025. Kutokana na hilo, serikali ikiongozwa na Rais John Magufuli imefanya juhudi kubwa kuweka mazingira mazuri yanayowapa wawekezaji fursa ya kusaidia nchi kufikia azma hiyo kupitia viwanda mbalimbali.

Moja ya fursa na nyenzo muhimu kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda, ni upatikanaji wa nishati ya uhakika ili kuwezesha viwanda hivyo kuzalisha katika mazingira wezeshi na rafiki ukiwamo upatikanaji wa nishati ya uhakika, imara na inayotosheleza. Katika msingi huo, serikali imekamilisha miradi kadhaa mikubwa ya umeme pamoja na kuendelea na miradi mingine mikubwa ya kuzalisha umeme.

Miradi hiyo ikikamilika, itaifanya Tanzania kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika ambao siyo tu utatumika nchini, bali pia utauzwa katika nchi nyingine hasa za jirani. Miongoni mwa miradi mikubwa iliyoanza utekelezaji, ni mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji wa megawati 2,115 utakaokamilika mwaka 2022.

Kukamilika kwa ujenzi wa bwawa hili na kuanza uzalishaji kutaifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu. Aidha, utaifanya Tanzania kuwa ya kwanza Afrika Mashariki kwa kuwa na bwawa kubwa, ya nne kwa Afrika na kuwa kati ya nchi 70 duniani zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme. Ipo pia miradi mikubwa iliyokamilika, ukiwamo wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako, Madaba hadi Songea, pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Madaba na Songea na upanuzi wa Kituo cha Makambako.

Kukamilika kwa njia hii ya kusafirisha umeme kumefanya mikoa ya Njombe na Ruvuma kuunganishwa katika Gridi ya Taifa na hivyo, kusitishwa kwa matumizi ya mitambo ya mafuta iliyokuwa ikiligharimu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Hali hiyo imeokoa wastani wa Sh bilioni 9.8 kwa mwaka zilizokuwa zikitumika kununua mafuta katika vituo vya Madaba, Ludewa, Songea, Mbinga na Namtumbo.

Siyo mradi huo tu uliokamilika, bali pia upo mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme (Backbone) ya msongo wa kilovolti 400 yenye urefu wa kilometa 670 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia mikoa ya Dodoma na Singida. Mradi huu umehusisha kukamilika kwa upanuzi wa vituo vinne vya kupoza na kusambaza umeme kwenye mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga, utawezesha kuvipatia umeme vijiji takriban 121 vinavyopitiwa na mradi.

Huu ni mradi muhimu katika Gridi ya Taifa kwa sababu umeongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Kanda ya Kusini Magharibi, ambako kuna vyanzo vingi vya umeme na kupeleka Kanda ya Kaskazini Magharibi na Kanda ya Ziwa ambako kuna shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo migodi ya madini. Mradi huo ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2015, ulikamilika mwaka 2017, na sasa mafanikio yake yanaonekana katika mikoa mbalimbali ukiwamo wa Shinyanga ambao licha ya kuwa na umeme wa uhakika kwa mahitaji ya wananchi wake, pia nishati hiyo imewezesha viwanda vingi kupiga hatua katika uzalishaji.

Katika mazungumzo yao na gazeti hili kwenye viwanda vyao hivi karibuni, wamiliki wa viwanda kadhaa vikiwamo vya Jambo Group, Fresho Investment Limited na Joc Textile (Tanzania) Co. Limited, wamekiri mradi wa Backbone umeleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji wao, kiasi kwamba kwa takriban mwaka sasa, hawana tatizo la kukatikatika kwa umeme au kuwa na umeme usio imara. Meneja wa Fedha wa Kampuni ya Jambo Group, Ally Khalfan Nguzo anasema kwa miaka miwili sasa, hali ya umeme katika viwanda vyao imekuwa imara na ya uhakika.

“Tofauti na miaka miwili iliyopita, sasa hivi upatikanaji wa umeme ni mzuri na wa uhakika. Umeme ni stable (imara), haukatiki tena, hali hii imesaidia kuepusha hasara zilizokuwapo awali kutokana na katikatika ya umeme,” anasema Nguzo. Naye Mhandisi Mkuu wa Jambo Food, Tom Mboya anasema kuna mabadiliko makubwa katika huduma za umeme mkoani Shinyanga yaliyowasaidia wenye viwanda kutekeleza azma ya serikali ya uchumi wa viwanda. “Tunapenda kuishukuru serikali kwa mradi huu mkubwa ambao umetusaidia sana katika uzalishaji wetu.

Umeme ni wa uhakika, hatuna tena shida. Tumeokoa fedha nyingi za kuendesha mitambo kwa kutumia jenereta maana huko nyuma tulikuwa tunaingia gharama kubwa kutokana umeme kutokuwa wa uhakika,” anasema Mboya. Anaongeza kuwa kwa mwezi wanatumia umeme wenye kati ya Sh milioni 430 hadi 450, hivyo wanaishukuru Tanesco kwa kuviwezesha viwanda vyao kufanya biashara ya uhakika. Kundi la Kampuni za Jambo linamiliki kampuni za kuuza mafuta ya dizeli na petroli, vinu za kuchakata mafuta ya kula, kampuni ya kusaga unga na ya vinywaji baridi yakiwamo maji, juisi na vifungashio.

Kwa upande wake, Meneja Rasilimaliwatu wa Kiwanda cha Nyuzi cha Joc Textile (Tanzania) Co. Limited, Marco Kyaruzi anasema Mradi wa Backbone umeleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa nyuzi kiwandani kwao. Anasema kati ya mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa umeme ilikuwa mbaya, lakini tangu mwaka jana, umeme unapatikana kwa wingi na kwa uhakika.

Kyaryuzi anasema awali walikuwa wanapata shida ya umeme na kulazimika kuingia gharama kwa kusimamisha uzalishaji huku wakiendelea kulipa wafanyakazi, jambo ambalo kwa sasa ni historia kutokana na kukamilika mradi huo. “Miaka ya nyuma wafanyakazi walikuwa wanakuja na kukaa bila kufanya kazi kutokana na kukosekana kwa umeme kwa siku nzima.

Hivi sasa umeme haukatiki ovyo, na kama kuna tatizo tunapewa taarifa mapema na wenzetu wa Tanesco. Hali ya uzalishaji sasa ni nzuri kwani umeme siyo tatizo tena,” anasema Kyaruzi. Kwa mujibu wa Kyaruzi, kwa mwaka kiwanda hicho kinapokea tani 800 hadi 1,000 za pamba iliyokwisha chambuliwa, na asilimia 90 ya nyuzi zao wanauza nje kwa sababu kiwanda hicho kimesajiliwa chini ya Ukanda wa Biashara za Nje (EPZ).

Akizungumzia mafanikio ya Mradi wa Backbone kwa kiwanda chao, Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Fresho Investment, Othman Rajab alnasema hali ya upatikanaji umeme imesaidia kampuni kufanya uzalishaji wa uhakika. Anaishukuru serikali kupitia Tanesco kwa kutekeleza mradi huo anaosema umekuwa mkombozi wa viwanda vingi mkoani Shinyanga, kwani awali walikuwa wakiteseka kwa huduma isiyokuwa na uhakika.

Meneja wa kiwanda cha vifungashio wa kampuni hiyo, Charles Otwere naye anaipongeza Serikali ya Rais John Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo azima ya Tanzania ya viwanda kwa kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana kwa uhakika. Anasema umeme ni bidhaa muhimu kwa wenye viwanda, na kupatikana kwa uhakika na imara kutachochea mapinduzi makubwa katika Tanzania ya viwanda kwa kuongeza uzalishaji hivyo kuongeza mapato ya serikali na pia kusaidia katika kuongeza ajira nchini.

Mbali ya kutengeneza vifungashio vya bidhaa ambavyo ni rafiki wa mazingira, Fresho Investment pia inajihusisha na kinu cha kuchambua pamba na kukamua mafuta ya kula. Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Fedgrace Shuma anasema Mradi wa Backbone uliogharimiwa na Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umesaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme mkoani Shinyanga na katika mikoa ya jirani.

Anabainisha kuwa, mahitaji ya umeme mkoani kwake ni megawati 68.2, wakati kiwango walicho nacho ni megawati 162, hivyo wana ziada kubwa ya umeme inayowafanya watoe mwito kwa wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika mkoa huo wenye fursa nyingi za kiuchumi. “Baada ya Backbone kukamilika, umeme wetu ni wa uhakika, imara na upo mwingi.

Wawekezaji waje tu kuwekeza, tunao umeme wa kutosheleza mahitaji yao hasa wakati huo wa Tanzania ya viwanda,” anasema. Mbali ya kuupatia umeme wa uhakika Mkoa wa Shinyanga, Mradi wa Backbone umewezesha kuimarika umeme katika mikoa ya Tabora, Arusha, Mara, Simiyu, Mwanza na Kagera. Umeme huo pia unalisha katika migodi mikubwa ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi pamoja na ule wa almasi wa Mwadui Williamson Diamond wa wilayani Kishapu.

SERIKALI imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu zaidi mashirika na taasisi zake ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi