loader
Usajili wa Bocco zogo

Usajili wa Bocco zogo

SIKU moja baada ya klabu ya Simba kutangaza kumuongezea mkataba wa miaka miwili nahodha wake John Bocco, timu ya Polokwane City SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) imeibuka na kudai mchezaji huyo amesaini mkataba wa awali kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao.

Taarifa kutoka uongozi wa Polokwane zinadai mchezaji huyo walijua alikuwa huru ndipo walipoanza kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kusaini mkataba wa awali tangu Aprili kuitumikia timu hiyo na kwamba hadi sasa PSLS kwa wasimamizi wakuu nchini humo wanajua kwamba mchezaji huyo watakuwa naye msimu ujao.

Hata hivyo, mkataba wa awali wa Bocco Simba unatarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu, hivyo alifanya mazungumzo na kuingia mkataba wa Polakwame akiwa ndani ya mkataba mwingine, kinyume na sheria za Fifa.

Taarifa ya Simba kwa vyombo vya habari jana iliwataka Wanasimba kufahamu kuwa Bocco ni mchezaji wao halali. “Tunapenda kuwajulisha umma wa Wanasimba kupitia vyombo vya habari kuwa suala hili lilizungumzwa baina ya viongozi wa Simba na Polokwane juu ya utata huo na likamalizwa kwa maelewano ya pande zote mbili,” ilisema taarifa ya Simba iliyosainiwa na Ofisa habari wake, Haji Manara.

“Ifahamike kuwa kwa mujibu wa Fifa, mchezaji akiwa amebakiza miezi sita kabla ya mkataba wake kumalizika na kama kuna klabu nyingine inayotaka kumsajili inabidi iwape taarifa klabu husika inayommiliki kabla ya kuzungumza na mchezaji, kwenye suala hili la Bocco, Polokwame hawakutoa taarifa kwa Simba juu ya kutaka kufanya mazungumzo na nahodha wetu,” alisema Manara kwenye taarifa yake.

“Kwa muktadha huo, tunawajulisha Wanasimba na Watanzania wote kwa ujumla kwamba John Bocco bado ni mchezaji wetu halali wa Simba na ameshaongeza mkataba na klabu yetu kama tulivyowaarifu jana (juzi) kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii,” alisema Manara.

Bocco aliyesajiliwa kutoka Azam misimu miwili iliyopita amekuwa na mchango mkubwa kwa Simba kwenye michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Kwa sasa yupo Misri kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachotarajiwa kushiriki fainali za Afrika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bc6c8050afd0a42e1df9b62c5e579a3c.jpg

TAMASHA la muziki wa dansi ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi