loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wabunge wamlaumu Amunike

WABUNGE wa Bunge la Tanzania wadai kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike kukosa mbinu ndiko kumechangia timu hiyo kufanya vibaya katika mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, dhidi ya Senegal juzi.

Taifa Stars juzi ilianza vibaya kampeni zake katika mashindano hayo Cairo, Misri baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Senegal katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa June 30.

Wabunge hao, Juma Nkamia wa Jimbo la Chemba mkoani Dodoma na Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo waliyasema hayo jana kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wakati wakirejea nchini pamoja na Spika Job Ndugai baada ya kushuhudia mechi ya ufunguzi Misri kati ya Taifa Stars na Senegal.

Nkamia ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa wizara inayoshughulikia michezo wakati wa uongozi wa awamu ya nne, alisema Amunike kukosa mbinu ni sababu iliyosababisha kikosi hicho kufanya vibaya kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Senegal.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Bulembo, ambaye kwa miaka mingi huko nyuma aliwahi kuwa kiongozi wa soka ndani ya kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (Fat) kabla ya kuwa Shirikisho la Soka (TFF).

Bulembo alisema mbali na kukosa mbinu pia kocha huyo hadi sasa hana kikosi chake cha kwanza, ambacho anaamini ni chanzo cha timu hiyo kukosa muunganiko kutoka sehemu ya ulinzi hadi ushambuliaji, hali iliyowafanya wapinzani wao kutumia makosa hayo na kuwazidi kila idara.

Nkamia alisema Stars ni timu ya serikali, lakini muda wote walikuwa wanacheza kwenye eneo lao hali iliyowafanya kushambuliwa wakati wote na kufanya makosa ambayo yaliwagharimu na kupoteza mchezo huo.

“Kama kocha Amunike angekuwa na mbinu, basi tulipaswa kupata ushindi, kukosa mipango ya kuwafanya wachezaji wa kikosi hicho kuwa wajanja kuwazidi wapinzani wetu tuliendelea kubaki kulinda lango, jambo ambalo ni hatari pale unapocheza na timu iliyotuzidi ubora kama Senegal,” alisema Nkamia.

“Niwaombe Watanzania tusirudi nyuma tuendelee kuisapoti timu yetu, ingawa ili tuweze kufanya vizuri lazima kocha awe na kikosi cha kwanza, Samatta ni mchezaji mmoja, lakini hapati ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji wengine,” alisema.

Bulembo alisema wakati wanaachana na wachezaji hao Misri walikuwa wanaendelea vyema na wana morali kubwa ya kuendelea kupambana hadi mwisho.

Naye Ndugai amesema ili kikosi hicho kiweze kuwa na nguvu na ari ya kushindana na timu zilizoendelea kama Senegal, kama nchi tunatakiwa kuwekeza kwenye miundombinu itakayozalisha wachezaji watakao kuwa na hazina kwa taifa.

“Kama taifa tunatakiwa kuwekeza kwenye kujenga viwanja bora na vya kisasa, kuwa na vituo vya kuvumbua vipaji na kulea watoto wenye vipaji na kuwa na Ligi bora, na kupinga vitendo visivyokuwa vya kiungwana kwenye mchezo huo kama rushwa,” alisema Ndugai aliyekuwa kiongozi wa msafara huo wa wabunge.

STAA wa Bongo Fleva, Rajab Kahali au Harmonize, ametoa ushauri ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi