loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tundu Lissu apoteza ubunge, nafasi iko wazi

SPIKA wa Bunge Job Ndugai ametangaza ukomo wa kiti cha ubunge cha Tundu Lissu kupitia jimbo la Singida Mashariki (Chadema) na amemuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwa jimbo hilo sasa liko wazi.

Ndugai alitoa taarifa ya ukomo wa ubunge wa Lissu, bungeni Dodoma jana mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasilisha hoja yake ya kuahirisha Bunge hilo hadi Septemba 3, mwaka huu. Kwa mujibu wa Spika huyo alitaja sababu mbili za ukomo wa ubunge wa Lissu ufikie ukomo, kuwa ni kutoonekana bungeni kwa muda mrefu bila taarifa lakini pia kutowasilisha kwa kipindi kirefu tamko la mali zake kwa Tume ya Maadili ya Viongozi kwa mujibu wa Katiba.

“Nimeshamuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi (NEC) na kumtaarifu kuwa jimbo la uchaguzi la Singida Mashariki lililokuwa chini ya Tundu Lissu, liko wazi,” alieleza. Alisema Lissu hakuwepo bungeni tangu Septemba mwaka 2017, baada ya kuondoka nchini kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu nchini Kenya.

“Zaidi ya mwaka mmoja uliopita hadi sasa amekuwa akionekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari duniani, akitembelea nchi na kushiriki mikutano na mihadhara. Kwa muda wote huo hajafika hapa bungeni na wala hajawahi kutoa taarifa yeyote kwa spika kuhusu alipo na anaendeleaje wala hajawahi kuleta taarifa yeyote kupitia kwa uongozi wake wa kambi au bungeni,” alieleza Ndugai.

Alisema Katiba iko wazi katika mambo ya aina hiyo, na baadhi ya wabunge wameshapata matatizo kutokana na utoro na kushindwa hata kumuambia spika mahali walipo. “Yaani mtu ana disregard tu. Pamoja na hilo lakini pia wabunge wote humu tunatakiwa tujaze taarifa kila mwaka mara moja zenye maelezo ya mali na madeni kama Katiba inavyotaka,” alisema Alisema utaratibu unataka zijazwe nakala mbili zote ziende Ofisi ya Spika, na baada ya hapo nakala moja ipelekwe kwa Tume ya Maadili ya Umma.

Ndugai alisema akiwa kama Spika baada ya kuona hakuna fomu zozote za Lissu, aliamua kupata uhakika kutoka kwa Kamishna wa Maadili ambaye alithibitisha kuwa mbunge huyo hajawasilisha tamko lake la mali na madeni kama inavyotakiwa. “Sasa mimi sina fomu za tamko lake wala maadili hawana.

Nawasisitiza wabunge tuishi kwa Katiba tuliyopa kwayo, Katiba inaeleza wazi nini kinakupata usipoitekeleza kama mbunge,” alifafanua. Kutokana na masuala hayo, kifungu cha 37 (3) kinataka Spika amtaarifu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi hivyo amemuandikia tayari barua kuwa kiti cha Singida Mashariki kiko wazi na mwenyekiti huyo aendelee na hatua ya kukijaza kwa mujibu wa sheria.

Alieleza kuwa Katiba inasema katika mazingira hayo yote mawili ubunge wake unakoma na ataacha kiti chake. Tangu Septemba mwaka 2017, Lissu aliposhambuliwa kwa kupigwa risasi, alienda nje ya nchi nchini Kenya na baadaye nchi nyingine ikiwemo Ubelgiji kufanyiwa matibabu ikiwemo kutolewa risasi.

Hata hivyo, amekuwa akionekana akifanyiwa mahojiano na vyombo mbalimbali vya kimataifa na kitaifa na kuelezea masuala mbalimbali yanayoendelea ya kisiasa ikiwemo tuhuma dhidi ya anaodai wameshambulia. Mbali na Lissu, Joshua Nassari (Chadema), ni mbunge mwingine ambaye nafasi yake ya ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki ilifikia ukomo kutokana na kutoonekana bungeni kwa muda mrefu bila taarifa.

UZALISHAJI wa chakula umeimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi