loader
Dstv Habarileo  Mobile
Binti yupo juu na brandi ya ubuyu

Binti yupo juu na brandi ya ubuyu

“NINATEGEMEA kujikuza zaidi kuhakikisha kwamba naondoka hapa nilipo ili niweze kuwa na eneo langu mwenyewe na kubwa zaidi,” anasema Asha Kasiliwa maarufu Atasha, jina la nembo yake ya bidhaa.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 24 hivi karibuni alipata tuzo ya wakfu wa Citi kwa kuwa mjasiriamali kijana katika hafla iliyoendeshwa na Shirikisho la Asasi zinazotoa huduma za fedha kwa wajasiriamali wadogo (TAMFI) katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro.

Akizungumza kutoka eneo lake la uzalishaji linalomilikiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lililopo Vingunguti, Asha anasema kwa sasa anaona eneo hilo kuwa dogo na tayari ameshatafuta eneo lake ambalo anataka kulifanyia kazi ili aweze kuajiri watu zaidi na kutanua biashara yake ya ubuyu na mazao yake na kuingiza bidhaa nyingine sokoni.

Anasema wakati anatazama mafanikio yake anakumbuka namna alivyoangalia fursa za ubuyu na kuanza kuufanyia kazi hasa baada ya kujifunza kuhusu ubuyu na namna ya kuuweka katika namna tofauti.

Alianza kwa mtaji wa Sh 200,000. Baada ya kupata mafanikio na kuona haja ya kuongeza mtaji, alijiunga na vikoba na kukopa Sh 500,000 ambazo imefanikisha kupandisha mtaji wake.

“Kwa sasa naona changamoto kubwa katika kazi hii. Mahitaji yamekuwa makubwa na bidhaa zimekuwa chache sokoni. Watu wameikubali brandi sasa ni kazi yangu kukidhi mahitaji,” anasema Asha.

Pamoja na kufanya shughuli zake za uzalishaji katika eneo hilo la SIDO Vingunguti, ofisi yake ipo nyumbani kwao Yombo Vituka Magogoni na sehemu kubwa ya bidhaa zake zinapatikana katika mtandao wa maduka ya Royals.

Bidhaa za ubuyu ambazo zinafanyiwa kazi kwa sasa ni matunda ya ubuyu, unga, mafuta na bidhaa za chai ya ubuyu na biskuti zake.

Kwa mujibu wa binti huyo, chai ya ubuyu ina faida mbalimbali kiafa, ikiwa ni pamoja na kusaidia kuimarisha viungo na kusaidia kumbukumbu (brain feed).

Akiwa katika kiwanda kidogo anachozalisha mafuta ya ubuyu, unga wa ubuyu na ubuyu wa kula kama tunda, anasema kwamba shughuli zake zote zinafanywa katika eneo ambalo limepata baraka za Shirika la Viwango nchini (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na pia anatumia mitambo ya kisasa zaidi kwa ajili ya kufanyia kazi ya kuchakata ubuyu huo.

Anasema alianza kazi ya kuchakata ubuyu mwaka 2017 baada ya kumaliza shahada yake ya Sayansi ya Kompyuta katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kwa mtaji kidogo sana kiasi cha Sh 200,000.

“Niliingia katika kazi hii ya ujasiriamali kwa kuwa naipenda. Nilienda kusoma shahada ya sayansi ya kompyuta kujipatia elimu ambayo natumaini itanisaidia katika safari yangu. Mama alinitaka nisome, nimesoma nina shahada, lakini napenda ujasiriamali na naona naenda vyema," anasema Asha ambaye asili yao ni Namanyere, Ufipani, mkoa wa Rukwa.

Asha anasema yeye alitamani tangu awali kusomea masuala ya biashara, lakini aliingia katika kozi ya sayansi ya kompyuta na alipomaliza aliona hamu yake ya kufanya ujasiriamali ikiwa imepanda sana.

Akiwa amezaliwa hospitali ya Tumaini, mkoa wa Dar es Salaam, Februari 17, 1994, amesoma shule ya msingi ya Kigilagila kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 na kujiunga na shule ya sekondari Kibasila kuanzia 2007 na kumaliza ngwe mwaka 2010.

Baada ya kumaliza sekondari aliingia katika Chuo cha Techno Brain ambapo alichukua stashahada kabla ya kuingia IFM kwa ajili ya shahada ya sayansi.

Binti huyu wa Alfred Kasililwa mwenyeji wa Namanyere na Tausi Selemani wa Tabora anasema alianza rasmi ujasiriamali mwaka 2017 baada ya kumaliza mafunzo katika taasisi ijulikanayo kama Tanzania Entrepreneurship and Competitiveness Center (TECC) ambako alichukua kozi ya wiki sita ya mambo mbalimbali.

Aliingia katika mafunzo hayo akitaka kuwa mtengeneza mikate, lakini kutokana na maelekezo ya mafunzo aliona kitu cha kufanya ni zao la ubuyu.

“Utengenezaji wa mikate unahitaji mtaji mkubwa na wakanisaidia kuona jambo jingine,” anasema Asha.

TECC ambao hufundisha wajasiriamali vijana kuanzia miaka 18 hado 24 ndio waliombeba Asha katika kujitambua na kufanya maamuzi ya kuendelea na wazo lake la ujasiriamali.

Ukiangalia hali aliyonayo sasa, Asha anasema yupo katika hali bora zaidi kuliko wakati wote na kwamba sasa anafikiria kupanua uwezo wake kufikia hatua ya kutoa ajira zaidi.

Kujituma kwake katika shughuli ya ujasiriamali kumeonwa na ndio maana TAMFI waliona haja ya kumpitisha katika kinyang'anyiro cha kuwania Tuzo za Wajasiriamali ya wakfu wa Citi na akiwa kijana aliibuka na tuzo na fedha za kuambatana kama kichocheo cha kazi zake anazofanya za kujiajiri na maono yake ya baadaye ya kuajiri vijana.

Pamoja na kushughulika na uchakataji wa zao la ubuyu, Asha pia ni mratibu wa matukio na majukwaa mbalimbali na mwalimu katika masuala mengi yakiwemo ya ujasiriamali. Asha anasema kwamba amefurahishwa sana na yeye kumzaa Asha mwingine ambaye watu wanapenda kumwangalia. “

Bidhaa hizi ni Asha mwingine kwani sasa wananchi wengi zaidi wanakutana na Asha katika bidhaa zenye brandi yangu."

Akiwa na vifungashio vinavyovutia, Asha ametoka katika hali ya kutumia vifungashio visivyokuwa na hadhi katika kuuza ubuyu wake kama tunda na kama unga na hivyo kuweka nakshi yenye mvuto mkubwa katika biashara.

Ukiangalia brandi ya Atasha utaona kwamba kwa umri wake na kupata tuzo za Citi kwa wajasiriamali wadogo, amepata msukumo mkubwa katika kazi yake ya ujasiriamali ambayo pia hufundisha wenzake.

Heshima ya tuzo ya Citi, ambayo hapa nchini inaratibiwa kwa pamoja kati ya TAMFI na Citibank ni kubwa kiasi ya kwamba Asha anasema hatakaa asahau kwa kuwa ni kubwa kwake na ni ya mara ya kwanza.

Benki ya Citi inayoongoza duniani na hufanya biashara katika nchi na mamlaka zaidi ya 160. Katika nchi Kusini mwa Jangwa la Sahara na hasa Tanzania, Citibank imejikita zaidi katika kutoa huduma za biashara na uwekezaji kwa makampuni makubwa, taasisi za serikali na za kifedha, wakiwa wanawezesha fedha na utoaji mitaji kwa uwekezaji mkubwa na kwa kutumia wakfu wa Citi wawekezaji wadogo.

Akiwa kama mwekezaji mdogo anasema wazi kwamba tuzo yake ambayo iliambatana na fedha ni msukumo mkubwa katika mpango wake wa kuwa na eneo lake na kutanua wigo wa bidhaa zake ifikapo 2020.

“Nataka kutanua wigo wa uzalishaji na kuingia katika soko la maduka makuu yaani supermarket,” anasema Asha ambaye anashukuru serikali kwa kutoa maelekezo mapya kwa Mamlaka ya Chakula TFDA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhusu muda wa kukaguliwa na kupata vibali.

Anasema vibali hivyo ni muhimu kuingia katika soko la maduka makuu.

Akiwa kijana ambaye bado hajawa na familia anasema kwamba ana mpango huo mara tu mambo yakikaa sawa ila kwa sasa anachangamkia zaidi ujasiriamali.

“Nina mchumba ambaye ananisapoti sana, amenikuta katika ujasiriamali na ananiambia nikazane nitafika mbali,” anasema.

Akiwa bado kijana anasema ni matumaini yake kuona kwamba anakuwa mjasiriamali mkubwa, mwenye familia yenye furaha.

Asha anasema ikiwa hayupo katika shughuli zake za ujasiriamali hupendelea kusoma vitabu, kuangalia filamu na anapenda kupitia mitandao kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa.

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi