loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wizara yafuata kodi ya pango GGM

OPERESHENI maalumu inayofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula kupita ofisi moja hadi nyingine kuzibana taasisi na kampuni zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi, imeuangukia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) mkoani Geita.

Imebainika kuwa mgodi huo hauna hatimiliki ya eneo hilo, lenye ukubwa wa kilomita za mraba 196.27 sawa na takriban hekta 19,927 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, hivyo kushindwa kulipa kodi ya pango la ardhi.

Juzi Dk Mabula alitembelea mgodi huo wa dhahabu wa Geita, kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi sambamba na kuangalia iwapo mgodi huo una hatimiliki ya ardhi katika eneo hilo.

Pamoja na kuipongeza GGM kwa kuwa mlipaji mzuri wa kodi ya serikali, Dk Mabula alisema eneo la mgodi huo linapaswa kupimwa, kutokana na kuwa katika mipango miji na sheria yake inaelekeza maeneo yote ya mipango miji, kupimwa na kupangiwa matumizi.

“Eneo la mgodi GGM lazima lipimwe na kupangwa kwa kuwa ndani ya mgodi kuna maeneo ya makazi, ofisi na matumizi mengine na vyote hivyo lazima vioneshwe katika ramani,” alisema Mabula.

Alisema upimaji katika mgodi wa GGM ni muhimu, kwani utaondoa migogoro ya ardhi, ambayo baadhi husababishwa na wananchi kuingia maeneo ya mgodi.

Alitoa mfano wa mgodi wa Nyamongo uliopo Tarime mkoani Mara, akisema baada ya kupimwa, umeepusha migogoro iliyokuwa ikitokea sambamba na kulipa kodi ya pango la ardhi.

Mshauri wa Masuala ya Sheria ya Mgodi huo, Elizabeth Karua alimweleza Dk Mabula kuwa GGM imekuwa ikilipa kodi mbalimbali serikalini, lakini haijawahi kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa ina leseni maalumu ya uchimbaji madini.

Kwa mujibu wa Karua, Mgodi wa Dhahabu wa Geita ulio chini ya kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afrika Kusini, katika kipindi chote cha shughuli zake, haujawahi kupewa wito wa kutakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi na umekuwa ukizingatia Mkataba wa Uendelezaji Uchimbaji Madini.

Aliomba mgodi huo kupewa wiki mbili, kushauriana na uongozi wa juu kuhusu suala hilo kwa kuwa ujio huo ulikuwa wa kushtukiza. Mabula aliupa mgodi huo hadi Julai 29 mwaka huu, kuja na majibu kuhusu suala hilo.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami alisema kodi ya pango la ardhi, inapaswa kulipwa na haina uhusiano wowote na leseni za uchimbaji madini, kwa kuwa mmiliki wake anakuwa kama amepangishwa eneo. Alieleza kuwa sheria ya Tanzania imetamka bayana kuwa ardhi itakuwa chini ya Rais.

Alisisitiza kuwa kodi ya pango la ardhi inalipwa, kama zinavyolipwa ankara za umeme na maji.

Kwa mujibu wa Masami, cha muhimu katika suala la kodi ya pango la ardhi ni umilikishwaji ambapo Mgodi wa Dhahabu wa Geita unatakiwa kutambulika, kwa kuwa na nyaraka sahihi za umiliki na kusisitiza tafsiri ya sheria ya madini siyo sehemu ya ardhi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita, Richard Jordison alieleza kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuhakikisha suala hilo linapata mwafaka ili kuondoa migogoro.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi