loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rwanda kutengeneza dawa za saratani

KAMPUNI ya LEAF Rwanda imesaini mkataba utakaoiwezesha kutengeneza dawa za saratani, LEAF- 1404 kuanzia mwaka kesho. Hatua hiyo itazifanya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nyingine barani Afrika, kupata ahueni kubwa ya tiba ya ugonjwa wa saratani.

Mbali ya uhakika wa upatikanaji wa dawa hizo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, imeelezwa kuwa, zitakuwa na ubora na unafuu wa bei tofauti na hali ilivyo sasa, kwani dawa ni ghali na huagizwa kutoka nje ya Afrika.

Kampuni mama, LEAF Pharmaceuticals ya Marekani imeridhia kampuni mshirika ya Rwanda itengeneze dawa hizo. Makubaliano hayo yameshuhudia na taasisi ya Contract Manufacturing Organisation (CMO). CMO imetajwa kuwa na mitambo ya kisasa ya uzalishaji bidhaa husika iliyohakikiwa na Mamlaka inayosimamia Chakula la Dawa Marekani (FDA).

Dk Clet Niyikiza, Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa LEAF Pharmaceuticals, anasema uzalishaji wa LEAF-1404 utawasogeza karibu na upatikanaji wa dawa bora, salama na ya bei nafuu kwa tiba ya kansa hasa ya matiti, kizazi na Kaposi Sarcoma. Kaposi sarcoma ni aina ya kansa inayojenga au kuleta mabadiliko kwenye viungo vya ngozi, utando laini wa kwenye midomo, pua na koo na maeneo mengine ya mwili. Inaelezwa kuwa, asilimia 90 ya wagonjwa wa Kaposi Sarcoma duniani wapo katika bara la Afrika.

Dk Victor Moyo, Makamu Rais Mtendaji, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo ambaye pia ni Mganga Mkuu wa LEAF Pharmaceuticals, amesisitiza kuwa, idadi kubwa ya vifo zinavyotokana na matumizi ya dawa zisizo na ubora au bandia haikubaliki.

“LEAF Rwanda inafanya juhudi hili ili kusaidia kusambaza dawa zenye ubora ziweze kutiba kansa katika bara la Afrika,” anasema.

“Kwa kuzalisha LEAF- 1404, tunakuwa na uhakika wa kupata dawa muhimu na salama na muhimu kwa ajili ya wagonjwa wa kansa ya matiti, kizazi na Kaposi Sarcoma,” anasema Dk Diane Gashumba, Waziri wa Afya wa Rwanda. Aliongeza kuwa, kwa mara ya kwanza Rwanda itakuwa na dawa bora, salama na zitakazopatikana kwa bei nafuu kwa ajili ya nchi nyingine za Afrika. Dawa kwa ajili ya kansa ni nadra kupatikana kwa wagonjwa wengi wa kawaida barani Afrika, sababu kubwa ikiwa ni ughali.

Hata hivyo, hatua zinazochukuliwa na nchi nyingi katika kuhakikisha zinakuwa na viwanda vya kutosha vya dawa ndani ya bara badala ya kuagiza kutoka nje ya Afrika, huenda zikarahisisha upatikanaji wa dawa nyingi ambazo ni adimu.

Tatizo nchi za EAC LICHA ya ukubwa wa tatizo hilo duniani kama ilivyoelezwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kansa Februari 4, mwaka huu, nchi za EAC zimeonekana kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo, kwa kuanzisha kampeni mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali za kisasa karibu katika kila nchi mwanachama.

Kwa mujibu wa Wakala wa Kimataifa wa Utafiti wa Kansa, takribani wagonjwa wapya takribani milioni 22 wanatarajiwa kubainika kila mwaka ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na milioni 14 waliobainika kuanzia mwaka 2012, huku vifo vikitarajiwa kuongezeka kutoka milioni 8.2 hadi milioni 13 ifikapo mwaka 2030.

Na katika kukabiliana na ugonjwa huo, Rwanda licha ya LEAF Pharmaceuticals kufikiria kujenga kiwanda cha dawa, hivi karibuni iliungana na nchi nyingine za EAC kuzindua kituo chake cha kisasa cha tiba ya kansa kinachomilikiwa na Hospitali ya Jeshi la Rwanda. Pia imelenga kutumia Dola milioni 3.4 kwa mafunzo ya madaktari bingwa wa kansa 21, wataalamu wa mionzi, ngozi na wauguzi.

Nchini Rwanda, ugonjwa huo umetajwa kusababisha vifo 5,000 kila mwaka, sawa na asilimia 7 ya vifo vyote, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Katika ukanda wa EAC, Kenya ndiyo inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya vifo kwa mwaka, kiasi cha 33,000 zikiwa ni takwimu kutoka WHO. Kenya iliripotiwa kuwa na wagonjwa 47,887 wa kansa mwaka 2018, wa kansa ya matiti wakiwa asilimia 13, kansa ya kizazi asilimia 11 na waliogua kansa ya koo wakiwa asilimia 9.

Kulikuwa na vifo 15,762 mwaka 2016 na viliongezeka na kufikia 16,953 mwaka 2017. Na katika kukabiliana na kasi ya ugonjwa huo, Kenya imepanga kuwa kitovu cha tiba ya saratani katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na tayari imeanza mikakati ya kuanza na vituo vikubwa vinane vitakavyotoa matibabu ya kina ya ugonjwa huo.

Pia katika mpango wake wa miaka mitano, Kenya inakusudia kusambaza tiba ya kansa katika Kaunti zake 47. Waziri wa Afya, Sicily Kariuki alikaririwa akisema mpango huo unatarajiwa kuanza haraka lengo likiwa si kuwahudumia Wakenya kwa kiwango cha hali ya juu tu, bali wakazi wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania Wakati Kenya ikiwa ya kwanza kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na kansa, Tanzania imetajwa kuwa ya pili kwa vifo 28,000 kwa mwaka, ikifuatiwa na Uganda yenye vifo 21,000 kwa mwaka.

Takwimu za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam zinaonesha kuwa, kwa ujumla kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa kansa. Mwaka 2015, kulikuwa na wagonjwa wapya 5,764 na mwaka 2016 waligundulika wagonjwa 6,338 idadi iliyoendelea kukua na kufikia 7,091 mwaka 2017 na mwaka jana wagonjwa 7,649.

Hata hivyo, aina ya kansa inayotajwa kusababisha vifo zaidi ni ya kizazi inayochangia asilimia 31.2 ya vifo, ikifuatiwa na kansa ya matiti (asilimia 12), kansa ya koo (asilimia 9.8), tezi dume 3.9, kansa ya sehemu ya kichwa na shingo (asilimia 6.8), kansa ya kibofu cha mkojo (asilimia 2.8) na kansa ya ngozi, asilimia 2.6. Aprili mwaka jana, Tanzania lilikuwa taifa la saba Afrika kuanzishwa chanjo ya shingo ya kizazi ambayo husababisha vifo vya wanawake wengi kwa mwaka.

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu alisema Desemba mwaka jana kuwa, katika kila wagonjwa 100 wa kansa, 34 huugua kansa ya mlango wa kizazi na 12 kansa ya matiti. Na katika kukabiliana zaidi ya ugonjwa huo, Serikali ya Tanzania mwaka jana ilitoa Sh bilioni 7 ili kuiongezea uwezo wa kutibu Taasisi ya Kansa Ocean Road (ORCI).

Dk Crispin Kahesa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba katika ORCI alikaririwa akisema kuwa, gharama za tiba ya kansa zimepanda kutoka Sh milioni 400 mwaka jana hadi Sh bilioni 9 kwa sasa. Aliongeza kuwa, ugonjwa huo ni changamoto kubwa katika sekta ya afya Tanzania. ORCI inapokea takribani wagonjwa 50,000 kwa mwaka, huku 29,000 wakitajwa kupoteza maisha.

Uganda Nchini Uganda, wagonjwa 32,617 waligundulika kuwa na kansa mwaka 2018 ikilinganishwa na 5,000 mwaka 5,000 na 4,000 mwaka 2016. Kati ya wagonjwa hao wa mwaka 2018, wagonjwa 21,829 waliaga dunia. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Afya ya Msingi, Joyce Aducu na kuonesha kuguswa na takwimu za Taasisi ya Kansa Uganda (UCI).

Alisema wagonjwa wengi hujitokeza wakati kuchunguzwa wakati tayari ugonjwa ukiwa umeshasambaa mwilini, hivyo kufanya kazi ya kutibu kuwa ngumu. Machi mwaka 2017, Uganda iliteuliwa na nchi wanachama wa EAC kuwa na hospitali ya kisasa ya magonjwa ya kansa iliyotengewa Dola za Kimarekani milioni 34 kwa ajili ya kuhudumia nchi wanachama.

EAC inaundwa na nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Aidha, EAC ambayo imeorodheshwa na WHO, kama moja ya eneo lenye hatari ya saratani ya mlango wa uzazi, ilianzisha kampeni ya kutoa chanjo katika kila taifa ili kudhibiti ugonjwa huo ambao hukumba wanawake. Kampeni hiyo iliyoanza Aprili, imekuwa ikiwapa chanjo wasichana kuanzia miaka 14.

Kauli ya EAC Kutokana na wimbi la ongezeko la wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, uongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki kupitia Katibu Mtendaji wa Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (EAHRC), Profesa Gibson Kibiki, ulielezea kusikitishwa na idadi kubwa ya wananchi ndani ya jumuiya kukumbilia tiba nje ya nje, akisema kuna tiba bora na nafuu katika hospitali zilizopo ndani ya jumuiya kwa sasa.

Alisema baadhi ya huduma zinazofuatwa nje kama tiba ya saratani, figo, moyo na kadhalika, sasa zinapatikana ndani ya Afrika Mashariki. Alisema kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaweza kutibiwa Kenya ambako huduma hiyo inatolewa kwa viwango vya juu; wenye magonjwa ya moyo wanaweza kutibiwa kwenye Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Muhimbili, Dar es Salaam, nchini Tanzania ambayo inatoa matibabu ya kibingwa kiasi cha kuwa gumzo ndani na nje ya jumuiya.

Aliongeza kuwa kwa wenye matatizo ya saratani wanaweza kwenda kutibiwa nchini Uganda ambako matibabu yanayotolewa ni ya kiwango cha juu, wakati matibabu kwa njia ya mtandao, Uhandisi tabibu pamoja na ukarabati wa kiafya yanapatikana kwa ubora nchini Rwanda.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: KIGALI, Rwanda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi