loader
Picha

Wadau waonya Afcon 2021

WADAU mbalimbali wa soka nchini wamesema Tanzania inaweza kufuzu fainali zijazo za Afrika, Afcon iwapo hakutakuwa na ubabaishaji wa maandalizi ya kikosi hicho mapema.

Katika ratiba iliyotolewa juzi na Shirikisho la soka Afrika (CAF), Tanzania imepangwa kundi J, lenye timu za Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta. Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wadau hao walisema kinachohitajika kwa sasa ni maandalizi mazuri na kuwa makini kwa kuweka mipango mapema.

“Tukifanya maandalizi mazuri tutakuwa na nafasi lakini tukiendelea na ubabaishaji hatuwezi kufika popote. Wahusika wanatakiwa kuandaa utaratibu mzuri na yote yanawezekana,”alisema mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga Zamoyoni Mogella.

Mogella alisema kunahitajika mechi zenye nguvu za kujipima nguvu, uchaguzi bora wa wachezaji na benchi la ufundi na mipango. Mchambuzi wa soka Ally Mayay alisema kundi la Tanzania sio jepesi kwasababu Tunisia na Libya ni timu nzuri ambazo kama hakuna maandalizi bora ya kuwakabili zinaweza kuwa ngumu.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema kinachohitajika ni kampeni za hamasa kuanza mapema za kushinda angalau mechi mbili za nyumbani kutoka kwa Libya na Guinea ya Ikweta na kugawana pointi na Tunisia.

Kingine alisema ni lazima mipango ianze sasa kwa maana ya kuwepo na kikosi kipana chenye nguvu kitakachomsaidia kocha kuelekea kwenye michuano hiyo sambamba na ile ya CHAN (Kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani).

Mchambuzi mwingine wa soka, Dominiki Salamba alisema kundi sio jepesi na kwamba anaona changamoto kubwa itakuwepo zaidi katika michezo ya ugenini na kutaka mipango na umakini uwepo katika maandalizi.

Alisema wachaguliwe wachezaji wanaostahili bila kuangalia watu, lakini kingine akisisitiza litafutwe benchi la ufundi ambalo litakaa na wachezaji kwa muda mrefu na kuwasoma.

Salamba alisisitiza pia, vijana wanaocheza ligi za ndani waendelee kuaminiwa na kupewa nafasi kwenye kikosi hicho ili kujiuza na kupata nafasi ya kucheza soka nje ya nchi.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars Charles Mkwasa alisema kundi ni gumu kulingana na wapinzani waliopo kwa kuwa, Taifa Stars hutegemea zaidi wachezaji wa ndani ukilinganisha na wengine huku akihimiza ligi zitengeneze mfumo utakaowezesha kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kushindana.

TIMU ya Taifa ya soka ya wanawake chini ya umri ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi