loader
Picha

Wasafiri bodaboda watumia helmeti feki

IMEBAINIKA kuwa asilimia kubwa ya kofi a ngumu (helmet) zinazotumiwa na watumiaji wa usafiri wa bodaboda nchini zinaingizwa kiholela huku pia zikiwa hazikidhi ubora unaotakiwa na viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), HabariLeo imebaini.

Kiutaratibu helmeti zinapoingia nchini ni lazima kwanza zikifika bandarini zikaguliwe na TBS ambayo inachukua kofia kadhaa kama sampuli na kwenda kuzipima kwenye maabara yake ili kubainisha kama zinaendana na ubora unaotakiwa ambao ni TZS 1478:2013.

Licha ya TBS kuwa na kiwango hicho kinaelekeza malighafi za kutumika kwenye utengenezaji wa helmet hizo kwa kuzingatia ugumu wa gamba la kofia husika, uimara, ukubwa wa ndani wa kofia lakini gazeti hili limebaini kuwa zipo njia za panya zinazotumiwa kuingiza helmeti zisizokuwa na viwango.

Ufuatiliaji wa kina uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam, umebainisha uwepo wa kofia zisizo na viwango ambazo kimsingi ndio zimeingizwa kwa njia hizo zisizosahihi.

Kofia hizo zinawahi kupasuka pindi zikipata msukosuko ambapo kama ikirushwa kutokea juu inapasuka haraka kutokana na utengenezwaji wake kuwa usio wa viwango ili hali inayokidhi viwango inapaswa kudunda na si kupasuka.

Kingine kinachothibitisha uwepo wa kofia zenye viwango na zile za kawaida ni tofauti ya bei ambapo kofia zenye viwango bora huuzwa kwa Sh 30,000 huku zile zenye viwango duni huuzwa hadi Sh 10,000, hali ambayo inawavutia wamiliki au waendesha wa bodaboda kupendelea kutumia zisizokuwa na viwango za Sh 10,000.

HabariLeo limefuatilia kwa undani na kubainisha kuwa hata hao wanaouza za bei ndogo tofauti na wa bei kubwa ni kwamba wakiulizwa kwa undani zaidi kuhusiana mahala walipozitoa hushindwa kuwa na majibu yanayoeleweka.

Mwathirika wa ajali ya bodaboda, mkazi wa Temeke Stereo, Mwavua Khamis aliyejeruhiwa kichwani katika ajali iliyotokea Februari mwaka huu huku akiwa amevaa helmeti bila kujua kuwa ni moja ya zisizo na ubora, aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kuwa alikuwa amevaa helmeti wakati ajali hiyo ikitokea lakini alikumbwa na jeraha kubwa kichwani.

Anasema imemchukua takribani miezi mitatu kutibiwa sehemu za kichwa huku akibainisha kuwa pia aliumia mguu wa kulia na bega katika ajali hiyo ambayo iliua mwendesha bodaboda papo hapo (jina limehifadhiwa).

Alisema,”siku hiyo nakumbuka dereva alivaa helmet na mie pia nilivaa ila sikuifunga kwa kuwa kwanza haikuwa na kifungio, sasa ninachokumbuka ni kuwa dereva alikuwa anakwepa daladala akaingia nyuma ya lori, ila nimeambiwa kuwa huenda hata helmet niliyotumia ni zile zisizokuwa na viwango ndio maana kichwa kikaumia.”

Mwendesha bodaboda, Haruna Shaban wa Tabata Kimanga amesema, waendesha bodaboda wamejikuta wakiwa njia panda kwa kuwa wanachojua ni kuwa helmet zote ni sawa na kuwa wanapouziwa za bei ndogo ndio kwao za maana.

Anasema,”kuna mwenzetu nakumbuka mwaka juzi alikufa kutokana na ajali ambapo alipatwa majeraha kichwani na hata pale Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Moi walishindwa kumtibu na akafa, alikuwa akipenda kuvaa helmeti na hata ajali ilipotokea alikuwa kaivaa sasa huenda ndio hizo za kiwango bora hazipasuki ajali ikitokea na zinazuia madhara.”

TBS wanena

Mkaguzi wa Ubora wa Bidhaa wa TBS, Yona Afrika alibainisha uwepo wa changamoto katika kukabiliana na uingizwaji wa helmeti nchini huku akigusia bandari bubu zinavyoshiriki katika hujuma hizo.

Alitaja moja kati ya changamoto hizo ni ubadilishwaji wa mara kwa mara wa njia zinazotumika kuziingiza nchini kofia hizo ambapo maofisa wa TBS wanaweza kukaa bandarini au mpaka mmoja kwa muda mrefu wakisubiri ziingizwe lakini waingizaji huwasiliana na kubadilisha njia.

Alisema kuwa hali hiyo imepelekea kuingizwa kwa kofia ngumu nyingi nchini na kuuzwa huku zikihatarisha usalama wa waendeshaji wa bodaboda hizo pamoja na abiria wake.

Alisema kwa upande wa TBS imekuwa ikiongeza umakini katika kuzikagua zile zinazopitia njia zinazotambulika ambapo pindi zikiingia nchini huchukua sampuli kadhaa na kisha kuyafunga kwa alama maalumu makontena yenye mzigo husika na kuyaruhusu kuondolewa kwenye bandari husika kuepuka gharama ambazo wanaweza kutozwa.

Alisema, TBS ndani ya siku tatu hutoa majibu kama helmeti walizokamata zinaendana na viwango vyao huku akibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 TBS iliziteketeza helmet zaidi ya 2,000 baada ya kubaini kutokuwa na ubora.

Alisema kiwango cha ubora za TBS kwa kofia ngumu cha 1478:2013 kimewekwa wazi wa wadau wote wanaoagiza bidhaa hizo na kuwa kwa wale ambao wanaziingiza tu nchini bila ya kuzingatia ndio wanaokumbana na adhabu husika.

Alisema kuwa ukaguzi wa TBS imeingia makubaliano na kampuni nne za kimataifa kufanya ukaguzi wa bidhaa zake zikiwamo helmet ambazo ni SGS, CCIS, Bureau Veritas na Intertek ambazo zimesambaa duniani kote na kati ya majukumu yake ni kufuatilia viwanda vinavyotengeneza helmet za kuja hapa nchini.

Wasemavyo wadau wa helmeti Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Helmet Vaccine Initiative Tanzania, Alpherio Nchimbi anaishauri TBS kukagua na kuteketeza helmeti feki zilizopo mitaani kama inavyofanya kwa bidhaa feki nyingine.

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamewasilisha mapendekezo kwenye Kamati ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi