loader
Picha

'Afrika iache ukoloni kuharakisha maendeleo'

NCHI za Afrika zimetakiwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwao ili kufi kia malengo kwa ustawi wa bara zima na watu wake.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, alipokutana na wakuu wa vyombo vya habari nchini humo.

Wakuu hao wa vyombo vya habari wanatoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Zimbabwe, Malawi, Namibia, Afrika Kusini, Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Ethiopia, Togo, Burkina Faso, Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Angola, Gabon, Guinea, Mauritania, Senegal, Sierra Leone, Chad na Djibouti.

Amesema Bara la Afrika lina fursa nyingi za kuziwezesha nchi zake kunufaika pamoja na wananchi wake. Shoukry alisema nchi za Afrika zinahitaji kujenga ushirikiano baina yao na kuachana na mtindo wa ushirikiano wa kikoloni ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Kwa njia ya ushirikiano, Afrika inaweza kutatua matatizo yake yenyewe. Tunaweza kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwamo kubadilishana teknolojia, maendeleo ya viwanda, elimu, afya, biashara na maeneo mengine mengi,” amesema Shoukry.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Misri, aliwaeleza wakuu hao wa vyombo vya habari wapatao 30 kuwa nchi hiyo imejipanga kushirikiana na nchi nyingine za Afrika na imeanzisha nafasi ya naibu waziri wa mambo ya nje inayohusika na mambo ya Afrika ikiwa ni mkakati wake wa kuimarisha ushirikiano huo.

Aliwataka waandishi wa habari wa Afrika kufanya kazi zao kama mabalozi kwa kuripoti habari nzuri na chanya kuhusu bara lao pamoja na kukuza ushirikiano kati ya nchi na nchi.

“Afrika imepata mafanikio makubwa katika sayansi, teknolojia, elimu na afya, hivyo lazima tujiendeleze wenyewe na kuuonesha ulimwengu kuhusu mafanikio yetu,” alisema.

Akijibu maswali kuhusu mambo ya usalama barani humo hususan mwelekeo wa vijana kujihusisha na makundi ya kigaidi na yenye msimamo mkali, Shoukry alisema Misri inafahamu uwapo wa makundi hayo na imejipanga kuhakikisha kunakuwapo amani na utulivu barani Afrika.

Alisema jambo hilo ni gumu hivyo Afrika ni lazima ibadili mtazamo wake kuhusu tatizo hilo kwa kuzuia mawazo yanayochochea kuanzishwa kwa makundi ya kigaidi na yenye msimamo mkali pamoja na kuzifanyia kazi sababu zinazowafanya vijana kujiunga na makundi hayo.

Shoukry alisema vijana ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na bara zima, hivyo kuna haja ya kuwaendeleza kielimu na kuwafanya wawe na manufaa.

Kwa mujibu wa Shoukry, Umoja wa Afrika (AU) mpango wake maalumu wa mwaka 2023 unalenga kuijenga Afrika yenye mafanikio.

Mpango huo uliopitishwa kwenye mkutano mkuu wa AU mwaka 2015, una malengo saba na mengine 20 yanayohusiana kwa ajili ya kufikia mageuzi katika maeneo matano ya msingi ikiwamo kuboresha hali za maisha ya watu.

Maeneo mengine ni kuwa na uchumi jumuishi na endelevu, Afrika iliyoungana, kuwawezesha wanawake, vijana na watoto pamoja na kuwa na Afrika inayojitawala vizuri, yenye amani na utamaduni wa kipekee katika muktadha wa kimataifa.

Imeelezwa kuwa mpango huo wa miaka kumi (2014- 2023) ni awamu ya kwanza ya ajenda ya AU ya miaka 50 ya ajenda ya 2063 katika kufikia maono ya kuwa na Afrika yenye ushirikiano, ustawi na amani inayoongozwa na watu yenyewe.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Cairo

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi