loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM: Ukombozi wa uchumi umetimia

“LEO ni siku ya kwanza ya safari ya ukombozi wa kiuchumi kwa Tanzania.” Hiyo ilikuwa kauli ya Rais John Magufuli muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Rufiji wa megawati 2,115.

Aliweka jiwe hilo jana katika Pori la Akiba la Selous wilayani Rufiji mkoani Pwani, kuendeleza safari ya ujenzi ya miaka mitatu iliyoanza Juni 15, 2019. Mradi huo wa kihistoria wazo lake liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1976, na kufanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 1980 na kampuni ya Norway.

Kampuni hiyo iligundua kuwa eneo hilo linafaa kwa mradi huo, lakini ndoto hiyo haikutimizwa kwa sababu mbili, mahitaji madogo ya umeme wakati huo megawati 100 na gharama kubwa wakati huo dola za Marekani bilioni 1.380.

Lakini jana Rais Magufuli alisema ana furaha kubwa kwa sababu ameanza safari ya mwanzo ya ukombozi wa kiuchumi kwa Watanzania. Rais Magufuli alisema pia ana sababu tatu za kuwa na furaha kubwa jana.

Aliitaja ya kwanza kuwa ni kutekeleza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya kuendeleza mradi huo wa kihistoria utakaofungua sekta nyingine. “Ya pili ni kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa kati unaojengwa kwa viwanda, hivyo bila umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, hilo haliwezekani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema zipo nchi ambazo gharama zao za umeme ziko chini hivyo Tanzania inalenga kufikia huko ili kujenga uchumi wa viwanda kufikia maendeleo. Aliitaja sababu ya tatu kuwa ni kupitia mradi huo Tanzania imedhihirisha kuwa ni Taifa huru linalojiamulia mambo yake wenyewe.

“Mwaka 2017 tulipoanza mradi huu tulipata upinzani mkali kutoka ndani na nje ya nchi. Hakuna mtu mmoja aliyejitokeza kutaka kutusaidia hata zikipojitokeza kampuni hizi za Misri.

Sisi ni taifa huru na siyo masikini. Tunajenga mradi huu kwa fedha zetu Sh trilioni 6.5, fedha zetu za ndani kupitia kodi zenu ninyi wananchi wa Tanzania,” alisema Rais Magufuli.

Alisema jambo jingine la kujivunia ni kwamba mradi huo unajengwa na Waafrika wenyewe, kampuni za Misri, nchi yenye uhusiano wa kindugu wa muda mrefu na Tanzania na kuwa kwa msingi huo sio vema kusubiri kupangiwa miradi ya kufanya na watu wengine.

“Hivi mnajua kwamba hapa Selous kuna hoteli chumba cha kulala unalipa dola za Marekani 3,000? Mimi niliamua makusudi kulala hapo ili nijue haya mambo. Sijui kama watu wa Maliasili wanajua. Sijui kama wanajua tunapokea ‘percentage’ ngapi. Sijui kama watu wa Ulinzi na Usalama wanajua kinachoendelea. “Ukiona nyuki wa mahali wako wakali sana ujue kuna asali, ukiona mahali nyuki hawahangaiki nawe ujue hapo hakuna asali. Eneo hili ni asali kwa Watanzania. Eneo hili ni asali ndio maana wanapiga kelele,” alisema.

Aliwataka Watanzania kutokubali kulaliwa akisema ya kuwa wamelaliwa muda mrefu kwa maslahi ya baadhi ya watu. “Tumelaliwa muda mrefu sana na ndio maana watu wanapiga kelele sana. Wana interest zao.

Tumelaliwa mpaka tutapasuka, msikubali kulaliwa tena,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa umeme na kufikia megawati nyingi zaidi kuliko wakati wowote ule na hasa nchi inapolenga kufikia megawati 10,000 kufikia mwaka 2025. Mbali na hilo, Rais Magufuli alisema mradi huo ni wenye manufaa kwani bwawa litadumu kwa zaidi ya miaka 60 na uwekezaji ukiwa wa gharama nafuu.

Pia alisema jingine ni Watanzania kufaidi uchumi wa kati kwani kutakuwa na umeme wa uhakika, wa kuaminika na wa gharama nafuu, hivyo kuongeza uzalishaji kwa wajasiriamali. “Biashara na uwekezaji pia utaongezeka kwani kutakuwa na nishati ya uhakika ya kuvutia wawekezaji kuja nchini,” alisema.

Rais Magufuli aliongeza kuwa mradi huu utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira kwani hekta 400,000 za miti zinateketezwa kila mwaka, zikiwamo hekta 150,000 za miti za Morogoro.

Alisema hili litasaidia kuhifadhi misitu ya nchi, hivyo maneno kuwa mradi huo utaharibu sio kweli kwani eneo la mradi ni asilimia 2 tu ya eneo lote la Pori la Akiba la Selous lenye kilometa za mraba 50,000 (zitatumika kilometa 914).

“Katika suala la uhifadhi wa mazingira sisi wa Tanzania hatuna mtu wa kutufundisha. Sisi katika Afrika ndio tumetenga eneo kubwa la uhifadhi karibu asilimia 32.2 ya ardhi yote ya Tanzania ,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa katika mabwawa mawili ya kufua umeme ya Mtera na Nyumba ya Mungu yamethibitisha kuna faida kubwa licha ya kufua umeme, ipo pia ya uvuvi ambako wananchi wanavua samaki kwa wingi.

Aliongeza kuwa pia wananchi watafaidika kwa utalii kwa kutembelea mandhari mazuri ya bwawa na michezo mbali mbali, hivyo kuongeza mapato. Kwa heshima ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alitoa pendekezo ambalo limeridhiwa na wizara, la bwawa hili kuitwa Bwawa la Nyerere. Bwawa hilo litakuwa na utefu wa kilometa 100, na litakuwa la nne kwa ukubwa Afrika, la kwanza kubwa Afrika Mashariki na la 17 duniani.

Aliipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kusimamia mradi huo na pia kufanikisha miradi mingine nchini. “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Tanesco wanafanya kazi nzuri, nawapongeza sana. Hivi sasa hakuna mgawo wala katikakatika ya Umeme… Tanesco wamepunguza gharama za uendeshaji, miradi wa Makambako wameokoa bilioni 9.8, Liwale - Tunduma bilioni 7.3, sasa hivi hakuna kuagiza nyaya, transfoma, Luku nje ya nchi. Kuna viwanda 15,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema Tanesco sasa hawapati ruzuku kutoka serikali, na viwanda hivyo 15 vimetoa ajira ya watu 3,520. Aliipongeza Tanesco kwa kupeleka Umeme vijiji katika vijiji 7,419 kote nchini kutoka vijiji 254 miaka minne iliyopita.

Aidha, wameongeza wateja wao kutoka milioni 1.4 mwaka 2015 kufikia wateja 2, 442,648 Mei mwaka huu. Maagizo mahsusi Rais Magufuli aliagiza mkandarasi Kampuni ya Arab Contractors na Elsewedy Electric zote za Misri kukamilisha mradi huo kwa wakati. Pia aliagiza bima ya mradi huo ikatwe kwa Shirika la Bima la Taifa (NIC) na vinginevyo.

Aliagiza hilo kwa wizara, Tanesco, Hazina na wakandarasi. Jingine ni kuwa vibali vya wafanyakazi wa kigeni viharakishwe na mamlaka husika, lakini visitolewe holela. “Wananchi wa Rufiji wapewe kipaumbele katika mradi huu kwa sababu wao ndio wamelitunza pori hili, kama sio wao basi ni baba zao, babu zao, au baba wa babu zao,” alisema. Aliwataka Watanzania zaidi ya 6,000 watakaojiriwa katika mradi huo kuwa waaminifu kwani wakihujumu mradi huu watakuwa wanatenda dhambi kwao wenyewe na kwa serikali.

Aliziagiza kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Pwani na Morogoro kuulinda mradi huo kama mboni ya serikali wakati wote na ikiwezekana JkT wapewe fursa ya kufanya kazi. Aliwataka wakazi wa mikoa hiyo miwili kuchangamkia fursa ya mradi huo kwani hakuna serikali inayojazwa watu fedha mfukoni, isipokuwa kwa kuchapa kazi. Aliwahimiza kulinda vyanzo vya maji na miradi mingine ya maendeleo na kuongeza kuwa mradi ukikamilika utoa ajira za kudumu 300 hadi 500.

Majaliwa Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema ndoto za Rais Magufuli za kuwapatia Watanzania wote umeme zimeanza kuleta mafanikio. Aliwataka Watanzania waendelee kumuombea rais pamoja na pacha wake, Rais Abdellah Fattah Al Sisi wa Misri. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema Bunge linamuelewa sana Rais Magufuli na serikali yake na kusema wale wanaodai hawaielewi “hii serikali, wataielewa tu.”

Kalemani Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema kazi kubwa ya mradi zitakuwa kujenga bwawa lenye kubeba maji mita za ujazo bilioni 35.2, nyumba ya mashine yenye mashine tisa kila moja ikifua megawati 235 na kituo cha Umeme cha kilovolti 440. Waziri wa Misri Waziri wa Nishati na Umeme wa Misri, Dk Mohamedi Shaker alitoa salamu za Rais All Sisi ambaye alisema anaufuatilia mradi huo kwa karibu.

Alisema Misri itasimama bega kwa bega na Tanzania katika mradi huo, ikiwamo kuwajengea uwezo wa kuzalisha, kubadilishana uzoefu na kuhuisha teknolojia. Dk Shakar alisema Misri itawapa mafunzo vijana 50 wa Kitanzania, huku alisema mradi huo sio ndoto tena, bali sasa ni uhalisia. Mwinuka wa Tanesco Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka aliahidi kuwa watausimamia mradi huo kwa weledi na kwamba kati ya fedha Sh trilioni 6.5, tayari Sh trilioni 1.007 zimelipwa.

Wakuu wa mikoa ya Pwani, Moro Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema mradi utakuwa na manufaa makubwa na tayari watu 558 wamepata ajira, na wataulinda mradi huo. Dk Stephen Kebwe wa Morogoro alisema mkoa wao utanufaika na tayari kuna ajira 1,884 za watu wa wake. Salma Kikwete Akizungumza baada ya kupewa nafasi na Rais Magufuli alipomaliza hotuba yake, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Salma alisema rais ameandika historia itakayokumbukwa.

Mbunge huyo wa kuteuliwa alisema Taifa na dunia inatambua kazi hiyo kubwa inayofanywa na mradi huo utaipeleka Tanzania katika uchumi wa kati unaojengwa kwa viwanda. Mawaziri 12, mabalozi 16 Shughuli za jana zilitia fora kwa kuhudhuriwa na mawaziri 12 wakiongozwa na Waziri mwenyeji Dk Kalemani.

Wengine ni mawaziri wa Madini, Muungano na Mazingira, Habari, Mambo ya Nje, Maliasili, Ofisi ya Waziri Mkuu, Maji, Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia Tamisemi, Utumishi pamoja na Ardhi, huku naibu mawaziri wakiwa wanne wa Nishati, Ujenzi, Maliasili na Mifugo. Wakuu wa mikoa walikuwa nane pamoja na wakuu wote wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mabalozi 16 na wawakilishi wa mashirika matatu ya kimataifa walihudhuria. Wananchi zaidi ya 1,500 kutoka sehemu mbalimbali walihudhuria katika sherehe zilizohanikizwa na ngoma ya Mganda, bendi ya JKT Ruvu na msanii Peter Msechu.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba, Rufiji

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi