loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kiswahili kitumike mkutano wa SADC

SIKU chache zimebaki kabla mkutano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, watu zaidi ya 900 kutoka sekta binafsi, wamejisajili kushiriki maonesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC yaliyoanza jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye maandalizi yanaendelea vizuri kuhakikisha washiriki wanapata nafasi nzuri ya kuonesha teknolojia na ubunifu wao katika viwanda.

Simbeye alimweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Dk John Kijazi alipotembelea maeneo ya maonesho jana kuwa maonesho hayo yatashirikisha watu kutoka Tanzania na nchi nyingine za SADC. Rais John Magufuli alifungua maonesho hayo.

Hata hivyo, zipo changamoto kadhaa zinazokabili ushirikiano baina ya nchi za SADC.

Kwa mfano, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu anataja changamoto inayoikabili MSD katika kununua dawa na vifaatiba miongoni mwa nchi wanachama wa SADC kuwa ni lugha.

Anaeleza kuwa Tanzania kupitia MSD, imekuwa imechukua hatua kukabiliana na tatizo hilo, hasa kutokana na Tanzania kutekeleza jukumu ililopewa mwaka jana la kuwa mnunuzi mkuu wa dawa kupitia mfumo wa ununuzi shirikishi.

Kwa mujibu wa Bwanakunu, lugha zinazotumika katika SADC ni tatu za Kiingereza, Kifaransa na Kireno, hivyo itawalazimu kutafuta wakalimani, kwa ajili ya kupeleka taarifa katika nchi wanachama kulingana na lugha wanazotumia.

Lugha hizi ni za kigeni na zinatokana na historia ya mataifa yaliyotawala katika nchi husika. Tatizo ni kwamba kwanini tuendelee kutumia lugha za mataifa yaliyotutawala wakati tupo huru? Na asili ya lugha hizo siyo bara la Afrika bali Ulaya. Kwa nini tunazitumia katika SADC ambayo inahusu nchi za Afrika?.

Ni kweli lugha za wakolonizimeenea kutokana na wao kutumia juhudi kubwa kuzieneza katika mataifa wanayoyatawala. Lakini, kwa nini waafrika tushindwe kueneza lugha zetu ambazo zitatuunganisha wote kwa pamoja? Kwa Waafrika lugha ambayo asili yake ni Afrika ni Kiswahili, lakini lugha hiyo haitumiki katika SADC.

Hivyo, zinatakiwa juhudi za makusudi, kueneza Kiswahili katika nchi za wanachama wa SADC, kwani ndiyo lugha pekee inayoweza kuwaunganisha haraka wanachama wa SADC na mataifa mengine barani Afrika.

Kwa hakika, kama nchi za SADC zitatumia lugha moja ambayo ni Kiswahili, zitarahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.

Kiswahili kinatakiwa kipendekezwe kuwa lugha mojawapo itakayotumika katika mkutano wa SADC na pia zifanyike juhudi za kukisambaza Kiswahili katika nchi za wanachama wa SADC. Kazi ya kusambaza Kiswahili katika nchi za wanachama wa SADC, haiwezi kuwa ngumu kwa sababu nchi nyingi zinafahamu lugha hiyo na chacheambazo hazifahamu lugha hiyo.

Lugha zenye ufahamu fulani kuhusu lugha ya Kiswahili na zinazotumia lugha ya Kiswahili ni Tanzania, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nchi ambazo watu wake hawajui Kiswahili ni rahisi kupata wakufunzi au wataalamu kutoka nchi za Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda ili baada ya miaka 10 Kiswahili kiwe lugha pekee itakayotumika katika mikutano ya SADC.

Waafrika tutukuze vya kwetu. Tuitukuze lugha yetu yenye asili ya Afrika. Tuamini katika Kiswahili chetu kwa maendeleo ya SADC na Afrika kwa ujumla. Pia tutumie lugha yetu adhimu ya Kiswahili, kujikomboa katika minyororo ya ukoloni mamboleo.

WAKATI zikiwa zimebaki siku ...

foto
Mwandishi: SALIM AREY, UDSM

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi