loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndugai aomba Bunge la SADC

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameuomba Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kulipa kipaumbele Jukwaa la Wabunge wa SADC kuwa Bunge kamili.

Ndugai amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na Serikali za SADC ikiwamo ya Tanzania, kutetea jukwaa hilo kuwa Bunge kamili na kuomba msukumo zaidi uwekwe katika mkutano huo rasmi, utakaofanyika Agosti 17 na 18 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unawahusu wakuu wa nchi na serikali wa nchi 16 wanachama wa SADC. Unatanguliwa na Maonesho ya Wiki ya Viwanda, yaliofunguliwa juzi na Rais John Magufuli, yanayoendelea hadi Agosti 8 na kisha vikao vya wataalamu na mawaziri wa jumuiya hiyo.

Akizungumza katika tafrija ya chakula cha jioni, iliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwa kushirikiana na kamati ya SADC na wadau wengine, Ndugai pamoja na mambo mengine, aliuomba mkutano huo wa wakuu wa nchi na serikali kuliangalia suala hilo ili kuongeza utekelezaji wa itifaki hasa katika eneo la sheria katika SADC.

“Bunge la Tanzania limekuwa mstari wa mbele kuimarisha mtangamano wa jumuiya hii kupitia Jukwaa la Wabunge wa SADC. Masuala ya utekelezaji wa itifaki za biashara, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), madini na kilimo ni maeneo muhimu yanayojadiliwa katika jukwaa hili,” alisema Ndugai.

Alisema Bunge la Tanzania linatambua mchango mkubwa wa Tanzania kuwa mstari wa mbele kutetea uwepo wa jukwaa hilo ili siku moja liwe Bunge kamili.

Aliomba nchi nyingine kutetea kuanzishwa kwa Bunge la SADC. Juni mwaka huu, Rais John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wabunge wa SADC, Veronica Dihova, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Ndugai. Dihova ni Spika wa Bunge la Msumbiji.

Wengine waliohudhuria ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro na Katibu wa Jukwaa la Wabunge wa SADC, Boemo Sekgoma.

Katika mazungumzo hayo, Dihova alieleza kuwa jukwaa hilo litashiriki kikamilifu katika Mkutano huo wa Agosti 17 na 18. Jukwaa la Wabunge wa SADC linawahusu maspika wote wa nchi wanachama wa SADC.

Aidha, Ndugai alimshukuru Rais Magufuli kufungua maonesho ya Wiki ya Viwanda, kwani yanaimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi na kuwataka Watanzania kutumia fursa ya soko la SADC lenye watu karibu milioni 350.

“Bunge linatambua juhudi za serikali katika kuweka mazingira rafiki ya biashara, kuanzishwa kwa Blue Print kuondoa vikwazo na urasimu usio wa lazima na tozo zinazobugudhi wafanyabiashara. Tunajua Bunge lijalo serikali italeta maboresho makubwa kudhibiti mtawanyo wa biashara kuondoa muingiliano wa majukumu,” alisema.

Akizungumza katika tafrija hiyo ya chakula, iliyoandaliwa kuwakaribisha wageni kutoka nje ya nchi na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa aliwashukuru waandaaji na kuhimiza washiriki katika Wiki ya Viwanda kuitumia fursa hiyo kutengeneza mtandao wa mawasiliano na kujiongezea ujuzi.

Bashungwa pia alitumia fursa hiyo, kuwakaribisha wageni wote kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kuwataka wajisikie nyumbani kwani Watanzania ni wakarimu kwa asili.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kupitia Mkurugenzi wa Masoko, Ernest Mwamwaja, ilionesha video fupi kwa waliohudhuria hafla hiyo, iliyohusu maeneo ya utalii yaliopo nchini na kuwaomba wageni kuhakikisha wanayatembelea, kwani hakuna kama hayo duniani ikiwemo Mlima Mrefu Afrika, Kilimanjaro.

WATOTO 84,625 waliokuwa na utapiamlo mkali, wametibiwa kuanzia mwanzoni mwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi