loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa kunguruma mjadala wa SADC

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania na Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Benjamin Mkapa ataongoza wasomi na Watanzania wote katika mjadala wa kuchambua historia ya jumuiya hiyo na uzoefu wake alipokuwa kiongozi.

Mkapa anatarajia kueleza anavyoifahamu SADC, kuchambua itifaki mbali mbali za jumuiya hiyo ikiwamo mafanikio ya Mkakati wa Maendeleo ya Kanda (RISDP), uliopitishwa na wakuu wa nchi na serikali mwaka 2003 wakati wa uenyekiti wake.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana, baada ya kutembelea maonesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC yanayofungwa leo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kuwa Rais mstaafu Mkapa ataongoza mjadala huo Agosti 15 wiki ijayo.

Dk Abbasi alisema kwa kutumia uzoefu wake, alipokuwa Mwenyekiti wa SADC miaka 16 iliyopita, Mkapa ataeleza historia ya jumuiya hiyo, hatua za mtangamano wa ushirikiano zilivyoanza na zinavyoendelea na kushauri nini kifanyike kwa SADC ya sasa.

“Kama mnavyojua Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kuwa mwenyekiti wa SADC, tarehe 15 ataongoza mjadala na kutoa uzoefu wake katika mtangamano wa ushirikiano wa kikanda katika ukumbi mpya wa maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),” alisema Dk Abbasi.

Katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za SADC, utakaofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Mwenyekiti mpya wa SADC anayepokea uongozi kutoka kwa Mwenyekiti wa sasa, Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob ni Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Kufuatia hatua hiyo, pia uenyekiti wa mawaziri wa SADC utakabidhiwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na maeneo mengine yanayobadilika kwa nafasi hiyo kwa mujibu wa kanuni na utaratibu wa jumuiya hiyo.

Miaka 16 iliyopita, Mkapa alikuwa Mwenyekiti wa SADC na katika uongozi wake mkakati wa RISDP ulipitishwa, ukilenga maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuipeleka jumuiya katika ustawi wa ushirikiano zaidi wa kiuchumi.

Mwaka 2011-2013 RISDP ilifanyiwa mapitio upya. Maeneo muhimu yameendeela kuwa kuimarisha ulinzi na usalama, ukuaji wa viwanda na masoko ikiweka nguvu katika ushirikiano wa mtangamano, miundombinu na uhakika wa nishati katika nchi wanachama wa SADC.

Katika hatua nyingine, Dk Abbasi amewataka wazalishaji wa bidhaa za Tanzania, kuhakikisha wanatumia vizuri fursa ya biashara kupitia Maonesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC, yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Dk Abbasi alisema pamoja na ubora wa hali ya juu aliouona katika bidhaa hizo, alipotembelea maonesho hayo jana, bado wazalishaji wa Tanzania wanapaswa kujua namna ya kupata fursa mbali mbali za kuongeza masoko ya bidhaa zao katika SADC.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi