loader
Aussems - Tumejipanga kubeba makombe yote

Aussems - Tumejipanga kubeba makombe yote

MABINGWA wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Simba wamesema msimu huu utakuwa wenye historia ya kipekee kwani wamejipanga kuhakikisha wanachukua mataji yote ya mashindano.

Kocha wa wekundu hao, Patrick Aussems amesema na ili kutimiza malengo hayo waliyojiwekea wataanza na taji la Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, Jumamosi.

Alisema wanahitaji kufanya vizuri na wanatambua kuwa wapinzani wao ni wazuri, pia wana malengo kama yao ila wanachoangalia wao ni kujipanga kupata ushindi kwa kufungua msimu na taji hilo.

“Tunahitaji kuanza msimu na kombe, tunajua utakuwa ni mchezo utakaokuwa na ushindani, lakini tunahitaji kushinda,” alisema.

Kikosi hicho cha wekundu wa Msimbazi kinaendelea na maandalizi dhidi ya mchezo huo muhimu unaozikutanisha bingwa wa ligi dhidi ya bingwa wa Kombe la Shirikisho utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco alisema “Ni mchezo utakaokuwa mgumu ila sisi tunaendelea na maandalizi yetu vizuri kwenda kupambana na kupata taji la kwanza la msimu mpya”.

Bado Simba itamkosa kipa wake namba moja, Aishi Manula ambaye ni majeruhi anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.

Daktari wa kikosi hicho, Yassin Gembe alisema mchezaji huyo amebakiza wiki moja kati ya tatu alizokuwa amepewa kupumzika kwa ajili ya kuendelea na matibabu hivyo, amemfuatilia anaendelea vizur na wiki ijayo atajiunga na timu.

“Tangu tumempa mapumziko ni wiki mbili zimeisha imebaki wiki moja na mpaka sasa maendeleo yake yanaridhisha, tunatarajia wiki ijayo atarejea aanze mazoezi mepesi,”alisema.

Nafasi ya kipa huyo kwa sasa inashikiliwa na ingizo jipya Beno Kakolanya, ambaye alianza kibarua chake katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka suluhu 0-0.

Kwa upande wa Azam FC waliokuwa Ethiopia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Fasil Kenema, wamesharejea Dar es Salaam na kuanza maandalizi dhidi ya mchezo huo wa Ngao ya Jamii.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/70458c801192282e883431da6d025704.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi