loader
Picha

Taasisi ya China kufundisha Kiswahili

BAADA ya Kiswahili kutambulishwa kuwa lugha ya nne kutumika katika nchi ya Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke ameitaka taasisi za Confucius inayofundisha lugha ya Kichina na tamaduni za Wachina, sasa kuanzisha madarasa ya Kiswahili.

Ombi hilo limelenga kuwezesha Wachina katika sehemu mbalimbali kuweza kusoma Kiswahili, lugha inayokua kwa kasi duniani, ili nao wawe na uelewe na uwezo wa kuwasiliana vema na wazungumzaji wa Kiswahili wanaozidi milioni 100 duniani.

Aidha, amesema ufadhili kutoka China kwa wanafunzi wanaosoma fani mbalimbali nchini humo umeongezeka mara mbili mwaka huu kutoka wanafunzi 120 mpaka 259 mwaka jana.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla maalumu ya kuwaaga wanafunzi 61 wa Tanzania wanaokwenda China kusomea fani mbalimbali wakiwemo 20 watakaosomea udaktari bingwa wa magonjwa ya figo na nyinginezo huku 41 wakisoma fani mbalimbali.

Balozi Wang amesema lugha ni muhimu kwa mawasiliano ambapo vyuo vikuu vinne nchini China vinafundisha Kiswahili na takribani kukiwa na wahitimu 20 wanaohitimu lugha hiyo kila mwaka.

Alisema tangu mwaka 2013 Idara za Elimu China na Tanzania ziliungana kufundisha lugha ya kichina na kuanzisha madarasa ya Confucius mawili nchini na mpaka sasa kuna shule na vyuo vikuu 50 vinavyofundisha lugha hiyo.

Alisema kwa sasa kuna wanafunzi zaidi ya 10,000 wanaosoma lugha ya kichina nchini, hivyo kwa jinsi Kiswahili kilivyo na heshima katika Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika kuwezesha mawasiliano katika biashara,utalii mikataba mbalimbali kati ya China na Afrika.

“Hivyo inahitajika zaidi ufahamu wa lugha ya Kiswahili pia; hivyo nahamasisha vyuo vya tamaduni za China hivyo na jamii ya Wachina nchini kuanza masomo ya Kiswahili kuwezesha wachina kuwasiliana vema na rafiki zao Watanzania,“ alisema.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako alisema ufadhili wa masomo mbalimbali nchini humo umekuwa ukiongezeka kila wakati wakati mwaka huu wanafunzi watakaopata ufadhili kutoka Serikali ya China na vyuo vikuu mbalimbali nchini humo wamefikia 259 kutoka 120 wa mwaka jana.

Alimuomba balozi wa China nchini, Wang Ke kusaidia kuongeza ufadhili mpaka mara tatu ya sasa ili kupata wataalamu wa miradi ya kipaumbele kwa serikali ikiwemo wahandisi wa uendeshaji mradi wa umeme mkubwa wa Rufiji na undeshaji wa reli ya kisasa SGR.

“Serikali inazidi kuomba ufadhili kwa wahandisi wa umeme mkubwa watakaosimamia mradi kuzalisha umeme wa Mwalimu Nyerere unaoendelea kujengwa katika bonde la mto Rufiji pamoja na kufadhili wahandisi wa kuendesha mradi wa reli ya SGR,” alisema Ndalichako.

Waziri amewashauri wanafunzi hao kutumia vema nafasi waliyopata kufadhiliwa na serikali na kuwa mabalozi wazuri ili kumaliza mafunzo hayo na kuwa wataalamu kwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla.

Balozi Wang Ke alisema mwaka huu wanafunzi 259 wanapata ufadhili kutoka nchini huo na mpaka sasa takribani China imetoa ufadhili kwa wanafunzi 1,900 na programu za ufundi stadi kwa zaidi ya 6,100 kutokana na ushirikiano wa kihistoria wa nchi hizo mbili.

Alisema wanafunzi wengi wa kitanzania wanachagua kusoma China kwa sasa wamedahili wanafunzi zaidi ya 5,600 wanaosoma nchini humo wakiwemo 690 wanaofadhiliwa na serikali ya China wengine wakilipa wenyewe na wengine wakifadhiliwa na kada mbalimbali.

Mwalikishi wa wanafunzi wanaokwenda kusoma China, Dk Saria Kasianju alimhakikishia waziri na balozi kuwa watakwenda kuwakilisha vema nchi kwa kufuata taratibu na sheria za nchi hiyo, hivyo kuwakilisha vema.

Kiswahili ndani ya SADC Kabla ya Wakuu wa nchi za SADC kupitisha Kiswahili kuwa lugha ya nne ndani ya jumuiya hiyo ikiungana na Kiingereza, Kifaransa na Kireno, Baraza la mawaziri wa SADC lilipitisha mapendekezo 107 ikiwamo kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya nne rasmi katika jumuiya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mkutano wa baraza hilo hivi karibuni, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema wameridhia mapendekezo hayo 107.

Profesa Kabudi akizungumza kuhusu Kiswahili, aliwashukuru wajumbe wa baraza kuona Kiswahili kinafaa kupendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC na hatua hiyo inadhihirisha kuthamini mchango Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Akifafanua, Profesa Kabudi alisema Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi kwa wapigania uhuru, lakini pia kinatumika kwenye nchi nyingi ikiwemo Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kaskazini mwa Zambia na inafundishwa kwenye vyuo vikuu 53 duniani. Afrika Kusini inaanza kukifundisha katika shule za msingi na sekondari mwakani.

Yashika kote Afrika Kwa kuingiza Kiswahili SADC, hii inakuwa lugha ya kwanza ya Afrika kuwa lugha rasmi katika jumuiya za kimataifa, ikiwemo EAC, SADC na Umoja wa Afrika (AU).

Katika moja ya mikutano ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli aliweka rekodi ya kuwa Rais wa Kwanza kuhutubia Umoja wa Afrika kwa lugha ya Kiswahili.

Hayo yalikuwa mapinduzi makubwa kuelekea katika kuitangaza lugha hiyo adhimu duniani.

Hizi ni habari njema kwa Watanzania, ambako Kiswahili lugha ya taifa na kwamba Watanzania sasa wanastahili kujivunia na kuvuna matunda ya juhudi za kukikuza Kiswahili.

MAMLAKA ya Maji ya Makonde iliyopo wilayani Newala mkoani Mtwara, ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi