loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SADC kuwa na Bunge

AZIMIO la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuielekeza Sekretarieti yake kupendekeza muundo wa Bunge la SADC, limejibu ombi la muda mrefu la Jukwaa la Wabunge wa jumuiya hiyo.

Kwa muda mrefu, Jukwaa la Wabunge wa SADC limekuwa likiomba Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo kupitisha jukwaa hilo kuwa Bunge kamili ili kutekeleza masuala ya kisheria na kurejesha chombo hicho karibu na wananchi wa nchi wanachama.

Jumuiya nyingine zenye mabunge ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU) lenye Bunge la Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lenye Bunge la Afrika Mashariki.

Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stergomena Tax, juzi akisoma maazimio zaidi ya 30 yaliyopitishwa na wakuu wa nchi na serikali katika mkutano wao wa 39 uliofanyika jijini Dar es Salaam, alitaja pendekezo la 30 ni la muundo wa kuanzisha Bunge la SADC.

“Aidha Mkutano (wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC) uliielekeza Sekretarieti na Baraza la Kibunge kupendekeza muundo wa Bunge ili kuandaa mpango wa utekelezaji wa Bunge kamili,” alisema Dk Tax akisoma maazimio ya mkutano wa marais wa SADC.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, alisema njia pekee itakayofanikisha kuipeleka jumuiya hiyo kwa watu wa chini ni kupitishwa kwa Jukwaa la Wabunge kuwa Bunge kamili.

Ndaitwah ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Namibia aliyasema hayo alipohutubia mhadhara wa wazi kuhusu mafanikio, changamoto na fursa za SADC uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani.

Mhadhara huo uliongozwa na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa. Alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wachangiaji wa mhadhara huo waliohoji kwanini SADC haina Bunge wakati jumuiya nyingine kama Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuna Bunge.

Ndaitwah alisema SADC imefanikiwa sana na inafanya vizuri katika eneo la amani kwa nchi wanachama lakini ni kweli bado haijafahamika na wananchi wa kawaida.

Awali, Rais mstaafu Mkapa akihutubia mhadhara huo, aliitaka SADC ipelekwe kwa watu wa kawaida kwani wananchi wengi wa nchi wanachama wamekuwa wakiliona kama ni chombo cha viongozi wanaokutana kwa vikao vya kila mwaka na haiwahusu wala kuwasaidia.

“Bunge ndio chombo kinachoweka ajenda karibu na wananchi wa kawaida kwa kuwa wabunge ni watu wanaotokana na wananchi hivyo huu ni wakati muafaka wa kuwa na chombo hicho,” alisema Ndaitwah.

Hivi karibuni, katika hafla ya kuwakaribisha wajumbe wa mkutano huo nchini Tanzania, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliuomba Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kulipa kipaumbele Jukwa la Wabunge wa SADC kuwa Bunge kamili.

Alisema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na Serikali za SADC ikiwamo Tanzania, kutetea jukwaa hilo kuwa bunge kamili na kuomba msukumo zaidi uwekwe katika mkutano wa viongozi hao uliofanyika Agosti 17 na 18, mwaka huu.

“Bunge la Tanzania limekuwa mstari wa mbele kuimarisha mtangamano wa jumuiya kupitia Jukwaa (Baraza) la Wabunge wa SADC. Masuala ya utekelezaji wa itifaki za biashara, teknolojia ya habari na mawasiliamo (Tehama), madini na kilimo ni maeneo muhimu yanayojadiliwa katika jukwaa hili,” alisema Ndugai.

Juni mwaka huu, Rais John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Veronica Dihova ambaye ni Spika wa Bunge la Msumbiji, Ikulu, jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Ndugai.

UZALISHAJI wa chakula umeimarika na hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi