loader
Picha

Uchaguzi serikali za mitaa Novemba 24

SASA ni rasmi, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara katika ngazi ya Mtaa, Kijiji na Kitongoji umepangwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikalki za Mitaa, Selemani Jafo alitoa tangazo hilo jana jijini hapa mbele ya wakuu wa mikoa, wakurugenzi, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya wananchi.

“Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 Ibara 4(1-3), Matangazo ya Serikali Namba 371, 372, 373 na 374 ya mwaka 2019, Waziri mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anautangazia umma wa Watanzania na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa tarehe 24 Novemba, 2019 itakuwa ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara,” alisema Jafo.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kifungu cha (1), waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa anapaswa kutoa Tangazo la Uchaguzi kwa umma si chini ya siku 90 kabla ya siku ya uchaguzi. Akifafanua zaidi, Jafo alisema tarehe hiyo imepangwa baada ya kukamilika kwa kanuni ambazo zitatumika kuendesha uchaguzi huo ambazo wadau, vyama vya siasa na asasi za kiraia zilishiriki kutoa maoni.

“Uchaguzi wa mwaka huu, utakuwa bora, kwa sababu umekuwa shirikishi wakati wa uandaaji kanuni na tumeandaa kanuni ambazo zinaodnoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwenye chaguzi zilizopita,” alisema na kuongeza kuwa siku ya uchaguzi, upigaji wa kura utaanza saa 2 asubuhi na kumalizika saa 10 jioni na watu watapiga kura kwa karatasi maalumu.

Alisema kampeni za uchaguzi huo zimepangwa kufanyika kwa siku saba kabla ya uchaguzi, ambazo zitaanza Novemba 17 hadi 23, mwaka huu.

“Kampeni za Uchaguzi zitafanyika siku saba kabla ya siku ya uchaguzi. Aidha, kanuni zinaelekeza, kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi kitawasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni,” alieleza.

Uchaguzi wa mwaka huu unaongozwa kwa Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji na Matangazo ya Serikali Namba 371, 372 373 na 374 ya Mwaka 2019.

Masharti ya uchaguzi Akielezea masharti muhimu ya kuzingatia katika huo, Jafo alisema nafasi zitakazogombewa ni Mwenyeviti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa Mtaa na wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.

Nyingine ni Mwenyekiti wa Kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.

Pia Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Miji. Jafo alisema wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi watatakiwa kuwa wanachama na kudhaminiwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Maeneo na mipaka ya uchaguzi Jafo alisema ili kuwafahamisha wananchi majina ya maeneo na mipaka ambayo itahusika katika kujiandikisha na upigaji wa kura, Msimamizi wa Uchaguzi atatangaza majina na mipaka ya vitongoji vilivyoko katika eneo la halmashauri husika siku 72 kabla ya siku ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi. Alisema pia msimamizi wa uchaguzi atatoa maelekezo ya uchaguzi siku 62 kabla ya siku ya uchaguzi, na atafanya uteuzi wa watumishi wa umma watakaoandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura siku 52 kabla ya uchaguzi.

“Uandikishaji na uandaaji wa Orodha ya Wapiga Kura utaanza siku ya arobaini na saba (47) kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku saba kwa kutumia fomu maalumu na utafanyika katika majengo ya umma na pale ambapo hakuna jengo la umma, uandikishaji utafanyika kwenye sehemu ambayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atakuwa amekubaliana na Viongozi wa Vyama vya Siasa.

Jafo aliongeza: “Vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia kura, kwa maeneo yaliyo chini ya Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo vitakuwa katika ngazi ya Kitongoji na kwa upande wa Mamlaka za Miji (Miji, Manispaa na Majiji), vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia kura vitakuwa katika ngazi ya Mtaa.: Taratibu za Uchaguzi Alisema mtu anayekusudia kugombea nafasi za uongozi, atatakiwa kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi husika siku zisizopungua 26 kabla ya siku ya uchaguzi kwa kadri itakavyoelekezwa na Msimamizi wa Uchaguzi.

“Mtu huyo pia atatakiwa kurejesha fomu husika ndani ya muda wa siku 7 tangu siku ya kwanza ya uchukuaji wa fomu iliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi. Ukomo wa walioko madarakani Jafo alisema viongozi wote walioko madarakani kwenye nafasi zote zitakazogombewa, uongozi wao utakoma siku saba kabla ya siku ya kuchukua fomu za kugombea. Jafo alisema msimamizi msaidizi wa uchaguzi atafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi zilizoainishwa katika Kanuni siku 19 kabla ya tarehe ya uchaguzi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni. Waangalizi wa ndani Alisema waangalizi wa ndani wa uchaguzi wanatakiwa kuomba kibali cha kufanya hivyo kwa Katibu Mkuu Tamisemi kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 16, mwaka huu ikiwa ni ndani ya siku 21 baada ya tangazo la uchaguzi kutolewa.

“Waangalizi wataruhusiwa kuangalia uchaguzi baada ya kupata kibali cha Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Serikali za Mitaa, maombi ya kibali cha uangalizi wa uchaguzi yatawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Serikali za Mitaa ndani ya muda wa siku 21 baada ya Tangazo la Uchaguzi kutolewa,” alieleza.

Kuhusu elimu ya mpiga kura, Jafo alisema taasisi yoyote inayotaka kutoa elimu ya mpiga kura katika uchaguzi, itatakiwa kuwasilisha maombi ya kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura.

“Kwa tangazo hili, wananchi wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kupiga kura, kugombea na kushiriki katika uchaguzi huu ili kupata viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Naye Katibu Mkuu Tamisemi, Joseph Nyamuhanga alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika katika vijiji 12, 319, mitaa 4,264 na vitongoji 64, 384. Maoni ya wadau Akizungumza baada ya kutangazwa tarehe ya uchaguzi, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Abdallah Juma Sadala alisema anaamini uchaguzi utakuwa huru na utafanyika kwa amani na utulivu.

Alisema kutokana na kuandaliwa kwa kanuni za uchaguzi kulikokuwa kwa ushirikishi zaidi, kunaonesha kukua kwa demokrasia nchini. “Kwa kiasi kikubwa maoni tuliyotoa kama vyama vya siasa yamezingatia na kuitaka serikali kutazama mawazo yaliyotolewa kuhusu wakuu wa mikoa kuondolewa kwenye usimamizi wa chaguzi ili yaendane na katiba, kanuni zilizopo na kwamba kama kuna changamoto zitatuliwe,” alisema.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

1 Comments

  • avatar
    Ramadhan I. Birolele
    31/08/2019

    Utaratibu umeandaliwa vizuri ,nadhani uchaguzi wa kipindi hiki utakuwa bora HONGELENI SANA KWA MAANDALIZI

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi