loader
Picha

Utekelezaji mradi wa SGR waikosha Benki ya Dunia

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani.

Kabagambe anayewakilisha nchi 22 za Kanda ya Afrika katika benki hiyo yenye Makao yake Makuu Washington, DC nchini Marekani, ametoa pongezi hizo kwa Rais John Magufuli baada ya kutembelea na kukagua sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.

Alisema amefurahishwa na kiwango cha kiufundi kilichotumiwa na Kampuni ya Yapi Merkez iliyopewa kandarasi ya kujenga reli hiyo na kwamba mradi huo si tu utakuwa na manufaa kwa Tanzania peke yake, bali katika ukanda wa nchi za Afrika ambazo hazipakani na bahari.

“Nimekuja kujionea hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kujenga reli hii ya kisasa na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza mradi huu mkubwa na wa kielelezo kwa kutumia fedha zake za ndani,” alisisitiza Kabagambe.

Aliahidi kuwa wakati Benki ya Dunia ikiangalia namna ya kuongeza ufadhili wa miradi kwa Tanzania, ataishawishi benki hiyo pamoja na taasisi nyingine za kimataifa zinazotoa misaada na mikopo kutoa fedha ili Tanzania itimize malengo yake ya kukamilisha ujenzi wa reli hiyo itakayofungua fursa za kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Afrika.

Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli katika Shirika la Reli Tanzania (TRC), Felix Nlalio alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya kiongozi huyo wa Benki ya Dunia pamoja na ahadi aliyotoa ya kuipigia debe serikali kwenye taasisi za kimataifa ili zitoe fedha za kukamilisha mradi huo.

Aliahidi kuwa kazi yao kubwa kama TRC na serikali kwa ujumla ni kuchapa kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa reli hiyo unaokwenda kwa kasi ukamilike kwa wakati na kuiletea faida nchi pamoja na nchi jirani.

Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa unaohusisha awamu mbili, kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro (kilometa 300) kilichoanza kujengwa Mei 2, 2017 na kitakamilika ifikapo Novemba 2, 2019 kwa gharama ya Sh trilioni 2.7.

Kipande cha pili kinachoanzia Morogoro –Makutupora (Manyoni, Singida) (kilometa 422), kilianza kujengwa Februari 26, 2018 na kitakamilika baada ya miezi 36 yaani Februari 25, 2021 kwa gharama ya Sh trilioni 4.4.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam na pia kutaimarisha biashara hususani kati ya Tanzania na nchi zinazopitiwa na Ushoroba wa Kati za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda na Rwanda.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi