loader
Picha

Waziri apigilia msumari wadaiwa sugu TPA

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesisitiza kuwa wizara kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) itaendelea kuwaondoa wadaiwa sugu wa kodi ya pango za majengo na nyumba watumishi wa umma, wabunge na baadhi ya taasisi za serikali ambao wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 20.

Amesema watafanya hivyo kwa lengo la kuimarisha wakala huo ili ujiendeshe wenyewe na hatimaye kukamilisha miradi mingine inayoitekeleza. Alisisitiza hayo katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyetaka kufahamu msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.

Kamwelwe alisema uamuzi huo wa kuwaondoa wadaiwa sugu unazingatia taratibu stahiki zinazotambulika kisheria.

“Wizara imeamua kufanya hivi kwa mujibu wa sheria kwani wakala unadai wateja wake zaidi ya shilingi bilioni 20 hivyo tukiendelea kulimbikiza madeni haya, wakala utashindwa kujiendesha na hatimaye kufa kabisa,” alifafanua.

Aidha, alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19, TBA imekusanya zaidi ya Sh bilioni 19 kutoka vyanzo vyake vya ndani vya mapato na inatarajia kukusanya zaidi ya Sh bilioni 114 katika mwaka wa fedha 2019/20. Alieleza kuwa hadi kufikia Juni, 2019, TBA imekamilisha baadhi ya miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba kwenye Mradi wa Kufufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere katika mto Rufiji uliopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

TBA imeanza kwa kuwaondoa wadaiwa sugu jijini Dar es Salaam na kisha kufuatia Dodoma ambako juzi ilizotoa familia tatu zilizokuwa zikiishi kwenye eneo la Area C. Jijini Dar es Salaam familia kadhaa zimetolewa kwenye nyumba zao huku ikibainisha kuwa uondoaji wa wadaiwa hao ni endelevu na kufanyika nchi nzima.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Miliki wa TBA, Herman Tanguye, TBA inadai fedha nyingi ambazo zikilipwa zitaiwezesha ofisi hiyo kufika mbali zaidi hasa kwa kujenga nyumba nyingine na kuwapangisha watu.

“Ifahamike kuwa TBA ni Wakala wa Majengo ambao kazi kubwa ni kuhakikisha ubora na usalama wa makazi, hivyo basi inakuwa sio sawa kwa watu kuendelea kuishi kwenye nyumba hizi na kushindwa kulipa, ili na sie tuendelee kuwaandalia makazi bora watu wengine ni lazima tulipwe kodi zetu tunazodai wananchi hao na hiyo itafanyika tu kwa kuwa kwa sasa hatutaki kubembeleza tena tumeshawapatia muda wa kutosha,” alisema.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa wakati akiwasilisha taarifa ya sekta hiyo, aliielezea kamati hiyo kuwa serikali inaendelea kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege nchini.

Kwandikwa alisema tayari Sh bilioni 5.7 zimeshapokelewa wizarani kwa ajili ya fidia ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Selemani Kakoso ameishauri wizara kupitia TBA kuhakikisha inaondoa kero na malalamiko ya wateja wake kwa kufanya maboresho ya nyumba zake.

Aliishauri serikali iangalie namna ya kuwapatia TBA mfuko wa dharura wa utekelezaji wa miradi iliyosimama hususani ile ambayo ipo katika hatua ya kuiongezea serikali gharama kubwa kwa kutoendelea kwa ujenzi huo.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi