loader
Picha

Wakili amlipia JPM deni la milioni 5/- Muhimbili

WAKILI Albert Msando amekabidhi fedha Sh milioni tano kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikiwa ni kumsaidia Rais John Magufuli kulipa deni aliloahidi kumlipia mwanamke mmoja aliyefi wa na mama yake mzazi.

Aidha, Muhimbili itamuandikia Rais Magufuli kuhusu kiwango kilichobakia cha deni hilo ambacho ni Sh 364,814. Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo wakati alipotembelea hospitalini hapo kuwaona majeruhi wa ajali ya moto uliosababishwa na kupinduka kwa lori la mafuta ya petroli iliyotokea mkoani Morogoro Agosti 10, mwaka huuu.

Akiwa hospitalini hapo, alikutana na mwanamke mmoja aliyedai ni mkazi wa Morogoro, ambaye alifiwa na mama yake aliyekuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo, na kutakiwa kulipia gharama ya Sh 5,364,814. Hata hivyo, Rais Magufuli aliagiza mwanamke huyo kuruhusiwa kuondoka na mwili, huku akiahidi fedha hiyo angeilipa yeye mwenyewe. Pia alimkabidhi mwanamke huyo Sh 500,000 kwa ajili ya matumizi.

Akizungumza hospitalini hapo jana wakati wa makabidhiano ya fedha hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Lawrence Museru alisema Rais Magufuli aliahidi kutoa fedha hizo baada ya mwanamke huyo kumlilia kuwa kafiwa na hana msaada.

“Rais aliagiza mama huyo aruhusiwe kuondoka na mwili na yeye mwenyewe (Rais) atawajibika kulipa deni hilo la hospitali,” alisema Profesa Museru na kuongeza kuwa agizo hilo lilitekelezwa ikiwa ni pamoja na mwanamke huyo kukabidhiwa mwili wa mama yake mpendwa.

Alisema baada ya ahadi hiyo, MNH ilipeleka deni la Sh 5,364,814 Ikulu na wakati wakijiandaa kulipa ndipo alipotokea mwananchi aliyeamua kumsaidia Rais Magufuli kulipa deni hilo kwa kuona majukumu mengi aliyonayo kiongozi huyo. Profesa Museru alisema amepokea fedha hizo kutoka kwa Msando na wenzake ikiwa ni kulipia gharama za matibabu kwa mwanamke ambaye alifariki.

Hata hivyo, Profesa Museru aliwatahadharisha wananchi kuwa gharama za matibabu ni ghali kutokana na kuboreshwa kwa huduma, na sio rahisi kwa Mtanzania wa kawaida kulipa kwa urahisi iwapo atakuwa hana kadi ya bima. Alisema ni muhimu kujiunga na mifuko ya bima za afya ili kupata matibabu zaidi kwani kwa mwezi hospitali hiyo inafuta gharama za matibabu Sh milioni 500 hadi 600.

Kwa upande wake, Msando alisema alichangisha fedha hizo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram akihamasisha wananchi ili kulipa deni hilo. Msando alisema alitumia mtandao huo kuonesha umma kuwa inaweza kutumika kwa njia iliyo bora, lakini pia aliuona ubinadamu wa Rais Magufuli aliouonesha na kutaka kudaiwa yeye fedha hizo za Muhimbili.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi