loader
Picha

Yanga, Azam, Simba Ni kufa au kupona michuano ya Caf

TIMU nne zinazopeperusha bendera ya nchi kimataifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho leo zinatarajiwa kuingia uwanjani kwenye michezo ya raundi ya pili ya marudio kwa hatua ya awali kuendeleza kampeni ya kusaka ushindi utakaowawezesha kusonga mbele.

Timu nne zinazoiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo zinazotarajiwa kushuka viwanjani leo na kesho ni Yanga na Simba upande wa Ligi ya Mabingwa, na Azam FC na KMC upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hizo zinaingia kwenye mechi hizo za marudiano baada ya michezo yao ya awali kwa asilimia kubwa kutawala sare isipokuwa Azam FC pekee, ambao walianza vibaya kwa kupoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Fasili Ketema ya Ethiopia.

Huku Simba wakiwa ugenini walitoka suluhu dhidi ya UD Songo ya nchini Msumbiji sawa na KMC waliotoka na matokeo kama hayo dhidi ya wenyeji wao As Kigali ya Rwanda, Yanga wakilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Township Rollers wakiwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Licha ya kwamba mchezo wa mpira huwa unadunda na kuleta matokeo ambayo hayakutarajiwa kwenye uwanja wa nyumbani, lakini wanapaswa kutumia nguvu ya mashabiki kwa kuanikiza kuwapa sapoti wachezaji kupata nguvu ya kupambana bila kuchoka ili kupata ushindi. Ukiachilia mbali mashabiki, kwa kipindi cha wiki moja kilichopita kila timu imefanya maboresho kwenye kikosi chake, ikiwemo kupata mechi za kirafiki kujiweka sawa kabla ya kuvaana na wapinzani wao.

Timu zote hizo zina kila sababu ya kupambana kusaka ushindi bila kujali watakuwa kwenye uwanja wa ugenini au nyumbani kuhakikisha wanafanya vizuri kuendelea kulinda nafasi iliyopata nchini ya kuingiza klabu nne kwenye michuano hiyo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma tulipokuwa tunaingiza timu mbili. Makala haya yanakuletea tathmini fupi kwa kila mchezo na nini kila timu inapaswa kufanya kuhakikisha hairudii tena makosa yaliyopita ili kuiwezesha kupata ushindi katika mchezo wa wiki hii na kuondoka na ushindi.

Simba v UD Songo SIMBA ambao ni mabingwa wa tetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatarajiwa kushuka kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuwakabili wapinzani wao Songo kutoka nchini Msumbiji, hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa wababe hao kukutana, kwani kwenye mechi ya awali wawili hao walitoka suluhu mechi iliyopigwa ugenini kwenye mji wa Beira.

Katika mchezo huo, Simba wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana historia waliyojijengea msimu uliopita kwa kufanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali kwenye michuano hiyo kwa faida ya kutumia vema uwanja huo na nguvu ya mashabiki wa timu hiyo ambao wanajitokeza kwa wingi kuanikiza. Ingawa wapinzani wao hao wataingia kwenye mchezo huo wakiwa wamejipanga huku wakijua wazi Simba wakiwa nyumbani wanakuwa na nguvu ya kucheza.

Kwa kutambua hilo, Simba wanahitaji kupata mabao ya mapema hali inyoweza kuwachanganya wapinzani wao na kutoka mchezoni faida ambayo inaweza kuwanufaisha na kuweza kupata ushindi wa mabao mengi kasha kutinga hatua inayofuata. Kwenye mechi iliyopita, Simba walionekana kukosa muunganiko mzuri kutoka sehemu ya katikati hadi sehemu ya kumalizia hali iliyochangia washambuliaji wa timu hiyo kama Meddie Kagere na John Bocco kukosa mipira ambayo ingeweza kuwa na manufaa na kuweza kupata ushindi ambao ungekuwa na faida kwa wekundu hao.

Kupitia maandalizi waliyoyafanya kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, kikosi hicho kimeonekana kuimarika, jambo ambalo lilipongezwa na kocha wa kikosi hicho, Patrick Aussems aliyedai kwamba hayo ni maendeleo mazuri kuelekea kwenye mchezo huo wa narudiano kesho. Yanga v Township Rollers Yanga wapo ugenini nchini Botswana na leo jioni wanatarajiwa kushuka uwanjani kuwakabili wenyeji Township Rollers.

Mchezo wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatazamiwa kuwa mgumu kwao kwa kuwa walipokuwa kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi ya awali walitoka sare ya kufungana bao 1-1, huku Rollers wakitangulia kupata bao kipindi cha kwanza na Yanga kusawazisha kipindi cha pili kwa mkwaju wa penalti. Pamoja na Yanga kuanzia nyumbani na nguvu ya mashabiki wao lakini walipambana vya kutosha kutafuta ushindi lakini wapinzani wao hao walionekana kuwa imara kwa kuzima mashambulizi yaliyokuwa yanaelekezwa langoni kwao.

Ni mechi ya kufa na kupona kwa Yanga ambao wanahitaji ushindi wa mabao kuweza kujihakikishia kupata ushindi, jambo ambalo linawezekana kwao kwa kuwa kwa kipindi cha wiki moja iliyopita walienda kuweka kambi mkoani Kilimanjaro ambako walipata michezo miwili ya kujiweka sawa kabla ya kukutana na wapinzani wao hao kwenye mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa leo kule Gaborone nchini Botswana.

Kwenye mchezo uliopita Yanga walionekana kuwa na matatizo ya kikosi hicho kwa kukosa muunganiko na umakini wa kumalizia nafasi zilizopatikana hasa kwenye sehemu ya kumalizia kufunga. Naamini kupitia michezo ya majaribio waliyokwishapata kupitia kocha wa kikosi hicho Mwinyi Zahera wana uwezo mkubwa wa kupata matokeo kwa kuwa kipindi cha maandalizi hatakuwa amefanya maboresho ya kikosi hicho.

Hiyo ni mara ya pili kwa Yanga kukutana na wapinzani wao hao, kwani mwaka juzi walikutana katika uwanja huo huo na matokeo yalikuwa sare ya kufungana bao 1-1, hali iliyowafanya wenyeji Township Rollers kufanikiwa kusonga mbele kwa faida ya ushindi walioupata ugenini. Azam Fc V Fasil Ketema Licha ya Ketema kufanikiwa kushinda ushindi kiduchu kwa bao 1-0 wakiwa kwao nchini Ethiopia, bado Azam wanapewa nafasi kubwa ya kuweza kupindua matokeo hayo na kuibuka na ushindi utakaowafanya kusonga mbele.

Kwa kuwa walipokutana kwenye mechi hiyo ya awali, wawili hao walionekana kutokupishana kwenye kiwango cha kumiliki mchezo, hivyo Azam wana kila sababu ya kupindua matokeo hayo leo jioni kwenye Uwanja wao wa Azam Complex kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kujihakikishia kusonga mbele. Hata historia yao bado Azam inawabeba wakiwa kwenye uwanja huo mara nyingi wanaibuka na ushindi kwenye kipindi chote ambacho timu hiyo ilikuwa inashiriki michuano hiyo ilikuwa na rekodi ya kutumia vema uwanja huo ambao ni machinjio yao.

KMC v As Kigali KMC walitarajiwa jana kuingia kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuwakabili wapinzani wao As Kigali kutoka nchini Rwanda, hatua hiyo inakuja baada ya timu hiyo kuanza vyema ugenini kwa kutoka suluhu ugenini. Pamoja na kwamba KMC kukosa uzoefu kwenye michuano hiyo lakini bado walipewa nafasi kubwa ya kuweza kuwatibulia wapinzani wao hao kutoka Rwanda na hiyo inaleta taswira ya mechi ya awali iliyopigwa Kigali hadi mechi hiyo inakamilika wawili hao wakitoka suluhu.

TIMU zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zinaendelea kufanya mazoezi kuimarisha ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi