loader
Picha

Ligi Kuu 2019-20 Ni kipindi cha jasho na damu

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2029/2020 linafunguliwa leo kwa viwanja vitano kuwaka moto kwa timu kadhaa kucheza zikiwania pointi tatu muhimu.

Hata hivyo, vigogo vya soka Tanzania Bara vya Simba na Yanga pamoja na Azam FC na KMC wenyewe hawatashuka dimbani kutokana na kukabiliana na mechi za kimataifa. Simba na Yanga wenyewe wanashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wakati Azam FC pamoja na KMC, wenyewe wanaliwakilisha taifa katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

TIMU SHIRIKI

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, msimu huu ligi hiyo itashirikisha jumla ya timu 20, ambazo ni Simba, Yanga, Azam FC, KMC, Lipuli FC, Ndanda, Alliance,Tanzania Prisons na Ruvu Shooting.

Timu zingine ambazo zitachuana katika msimu huu wa Ligi Kuu, ambayo itamalizika mwakani, ni pamoja na Polisi Tanzania, Mwadui FC, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Namungo FC, Mbao, Singida United, Biashara United na JKT Tanzania.

Kila timu shiriki itashuka dimbani mara 38 na kama ikishinda mechi zote, basi inatakiwa kujikusanyia jumla ya pointi 114, lakini haijawahi kutokea timu kutwaa pointi zote hizo. NGAO YA JAMII Simba, ambao ndio mabingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita, mwishoni mwa wiki iliyopita walitwaa kwa mara ya tatu mfululizo Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Azam FC kwa mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Kwa ushindi huo, Simba imeweza kuifikia rekodi ya Yanga ya kutwaa ngao hiyo mara tano, ambapo kabla ya Simba kushinda wiki iliyopita, wenyewe Yanga ndio walikuwa na rekodi ya kutwaa mara nyingi ngao hiyo. Mechi ya Ngao ya Jamii, ambayo inawakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Simba), na washindi wa Kombe la Shirikisho au Kombe la FA (Azam FC), ni ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu unaofuata.

MSIMU MPYA

Awali, mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilitakiwa kuanza kupigwa Agosti 23, lakini kutokana na mwingiliano wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, TFF wamelazimika kusogeza mbele ratiba hiyo.

Aidha, timu ambayo ilikuwa imepangwa kuanza kucheza mechi ya ufunguzi ni Simba ambayo ni mtetezi wa ligi hiyo kwa msimu uliopita, iliyopangiwa kucheza dhidi ya JKT Tanzania, lakini kutokana na mabingwa hao kukabiliwa na mchezo wa kimataifa dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji, mchezo huo wa ligi umesogezwa mbele. Sio tu Simba, hata Yanga, Azam pamoja na KMC, mechi zao zote za ufunguzi za Ligi Kuu Tanzania Bara, zimesogezwa mbele na sasa zote zitachezwa wikiendi inayofuata baada ya kukamilisha ratiba zao za raundi ya awali za michuano ya kimataifa.

TIMU ZIMEJIPANGAJE?

Timu zilianza kujipanga kwa kufanya usajili kulingana na mahitaji, huku zile za michuano ya kimataifa kama Simba, Yanga, Azam FC na KMC zikijitahidi kufanya usajili kwa kuzingatia mechi hizo. Pia, timu zilijitahidi kupiga kambi za uhakika mfano Simba walikwenda Afrika Kusini wakati watani zao Yanga, wenyewe walianzia Morogoro kabla ya kuhamishia kambi hiyo Zanzibar na baadae Moshi na Arusha, ambako pia walicheza mechi za majaribio. Kambi hizo zilikuwa kwa ajili ya michuano ya kimataifa pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuhakikisha timu zote hizo zinajiandaa vizuri tayari kwa ajili ya michuano hiyo.

Maandalizi ya timu zote shiriki kulingana na mahitaji yao, ndio kunaifanya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2019/2020 kutarajiwa kuwa moto mkali na kuwa na ushindani mkubwa tofauti na huko nyuma. Pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, jana kumtangaza mdhamini mkuu wa ligi hiyo, ambaye ni Vodacom aliyekuwa anafadhili kwa miaka ya nyuma, lakini sasa ameibuka na kitita kikubwa zaidi cha fedha, ambacho kitazifaidisha zaidi timu na TFF. Makala haya yanakuletea baadhi ya timu zinazotarajiwa kuonesha ushindani kwenye ligi hiyo kulingana na ukwasi walionao ambao utachagiza kufanya vyema na kupewa matarajio ya kushika nafasi za juu kuwania kikombe hicho.

SIMBA SPORTS CLUB

Simba ndio mabingwa watetezi na wanaingia katika ligi hiyo kama timu inayopewa nafasi tena kutetea ubingwa wake kutokana na usajili iliyofanya pamoja na maandalizi, huku ikiweka matumaini hai kwa kufanya vizuri katika mechi kadhaa, ikiwemo ile ya Ngao ya Jamii. Simba ina wadhamini kadhaa ikiwamo SportPesa, ambayo imetoa kitita cha kama Sh milioni 800 kwa mwaka, A-One Product inayozalisha kinywaji cha Mo Extra wametoa Sh milioni 250 kwa mwaka. Pia wameingia mkataba na Kampuni ya Romario Sport ya Uarabuni kwa ajili ya kutengeneza na kuziuza jezi kupitia wakala na msambazaji wao hapa nchini, Uhlsport wenyewe wanatoa kama Sh milioni 900 kwa mwaka. Kulingana na uwezo huo wa kifedha, Simba wanapewa asilimia kubwa ya kufanikiwa kutetea tena taji hilo la ligi kwa mara ya tatu mfulizo ikilinganishwa na klabu nyingine.

VIJANA WA JANGWANI

Yanga, ambao wanajulikana pia kama vijana wa Jangwani, wenyewe msimu huu wako vizuri zaidi ukilinganisha na ule uliopita, ambao walikuwa wakilialia kutokana na ukosefu wa fedha. Uwezo wa kifedha, ambao ulitokana na wanachama na wapenzi wake kuichangia, umeifanya timu hiyo kusajili wachezaji aliowahitaji kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera, hivyo wengi wanatarajia timu hii ndio itakuwa mpinzani halisi wa Simba katika mbio za ubingwa.

Yanga ndio inaongozwa kwa kutwaa mara nyingi taji hilo la Ligi Kuu, baada ya kulibeba mara 27 ikiwa ni ushindi wa kihistoria, tofauti na timu zingine. Klabu hiyo pia inadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa pamoja na kampuni nyingine kama GSM, ambayo imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza na kuzisambaza jezi za Yanga.

SportPesa kama kwa Simba, imeipa Yanga kiasi cha Sh milioni 800 huku GSM ikiweka mabilioni ya fedha pamoja na kuahidi kulikarabati jengo la klabu hiyo lililopo katika mitaa ya Twiga na Jangwani. Bado Yanga ina mtaji mkubwa wa mashabiki, ambao hawataki kuona klabu yao ikipata shida na ndio maana walikuwa tayari kuichangia timu yao mamilioni ya fedha na kuiwezesha kufanya usajili mzuri kwa kutumia fedha hizo.

VIJANA WA CHAMAZI

Azam FC ni miongoni mwa timu tajiri na zilizofanya uwekezaji mkubwa na zinatarajia msimu huu kufanya vizuri, lakini kama itarekebisha makosa madogo madogo, ambayo yamekuwa yakiisumbua klabu hiyo.

Kiuwekezaji Azam inaongoza hakuna Simba wala Yanga, kwani timu hiyo ndio pekee ambayo ina uwanja wake wenyewe, ambao inautumia kwa mechi za ligi na zile za kimataifa, tofauti na hata na vigogo vya soka hapa nchini. Pamoja na uwekezaji mkubwa, lakini Azam FC imeshindwa kabisa kudhihirisha ‘utajiri’ wake mbele ya Simba na Yanga kwa kuendelea kuwa mteja wa timu hizo mbili.

Azam kama msimu uliopita inapewa nafasi ya kushika nafasi ya tatu, lakini baada ya msimu huu kuwa na kocha Etienne Ndayiragije, ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo. Kocha huyo anajulikana uwezo wake tangu alipokuwa akizifundisha Mbao FC ya Mwanza kabla ya kutua timu ya Manispaa ya Kinondoni ya KMC na sasa Azam FC, na sasa vigogo vya Simba na Yanga vikae vizuri, la sivyo vitatolewa nishai na Azam.

TIMU NGENI YA KMC

KMC ni timu inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, wenyewe wamefanikiwa kuingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya M-bet, ambayo inaidhamini KMC kwa miaka mitano kwa thamani ya kama Sh bilioni 1, ambao ni sawa na Sh milioni 200 kwa mwaka. Fedha hizo zinaweza kuisaidia timu hiyo, lakini inatakiwa kutafuta wadhamini zaidi ili iweze kujiandaa vizuri kusajili na kumudu mahitaji mengine msimu Ligi Kuu 2019-20 Ni kipindi cha jasho na damu wa mwaka 2020 na 2021. Huu ni msimu wake wa pili tangu ipande daraja, lakini imeonesha mchezo mzuri na kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa iko chini ya Jackson Mayanja baada ya Ndayiragije kwenda Azam FC.

POLISI TANZANIA

Polisi Tanzania imepanda Ligi Kuu msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza, lakini timu hiyo inashika nafasi ya nne kwa kuwa na udhamini mnono unaodhaminiwa na Lodhia Group, ambao ndio wadhamini wa kuu, na mdhamini mwenza ni Mazao Group, wote wakiingia mkataba wa mwaka mmoja mmoja.

Maafande hao wanakadiriwa kwamba kwa mkataba huo wanavuna kitita cha milioni 400, hivyo basi wanategemea kuleta ushindani mkali kwenye ligi hiyo, na hasa ukizingatia kuwa inafundishwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Selemani Matola.

Matola ana zoefu na Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani kutokana na msimu uliopita kuwa na timu ya Lipuli ya Iringa kabla ya kuhamia Polisi Tanzania, ambayo inatarajiwa kuwa moto. Polisi Tanzania katika maandalizi yao ya Ligi Kuu hivi karibuni walicheza dhidi ya Yanga na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ushiria mjini Moshi. Polisi wamechagua Uwanja wa Ushirika Moshi kuwa nyumbani kwao.

NAIBU Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

1 Comments

  • avatar
    aron
    01/03/2020

    simba ni timu zur xan

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi