loader
Picha

Utalii wachangia 80% fedha za kigeni Z'bar

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa kujengwa kwa hoteli ya kisasa ya Madinat El Bahr ni hatua kubwa ya mafanikio katika mipango ya maendeleo kwenye sekta ya utalii ambayo inachangia asilimia 27 ya Pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.

Dk Shein aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa Hoteli ya Madinat El Bahr iliyopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara kadhaa kutoka katika sekta ya utalii.

Katika hotuba yake, Rais Shein alisema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sekta ya utalii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazoingia Zanzibar ambapo taarifa za Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar zinaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, utalii umechangia kiasi kikubwa katika upatikanaji wa ajira.

Alieleza kuwa katika medani ya biashara ya kimataifa inaeleweka kwamba utalii ndio sekta kuu miongoni mwa sekta zinazotoa huduma na ina mchango mkubwa katika uchumi wa dunia.

“Nina furaha kuona kwamba, sera na mipango yetu ya kukuza utalii inatufanya na sisi tuwe wenye kunufaika na neema za utalii kwa kadri sekta hii inavyokua duniani,” alisema Dk Shein.

Aidha, Rais Shein alisema katika mwaka 2017 sekta ya utalii ilitoa ajira takriban 28,000 za moja kwa moja ambazo ni zile ajira zinazohusu shughuli halisi za utalii na zaidi ya ajira 60,000 zisizo za moja kwa moja ambazo zinazinufaisha sekta nyengine za kiuchumi kutokana na shughuli za utalii.

Alieleza kuwa ufanisi wa mipango na sera katika kuendeleza utalii unadhihirika wazi wazi katika matokeo ya utafiti juu ya sekta ya utalii uliofanywa na UNICEF kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar mwaka 2018.

Alieleza kuwa utafiti huo umeonesha utalii umekuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar katika kukuza ajira, hali za maisha ya watu na utekelezaji wa mipango na mikakati ya kupunguza umaskini.

“Imeelezwa kwamba pato linalopatikana kutoka sekta ya utalii limekuwa likiongezeka kwa kiasi kikubwa kila mwaka kwa mfano pato hilo liliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 157.1 mwaka 2011 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 269.3 katika mwaka 2014 na katika mwaka 2017 tayari lilikuwa limeshafika Dola za Marekani milioni 489,” alisema Dk Shein.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa waliofika Zanzibar tangu mwaka 2008 hadi mwaka huu imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kizuri ambapo hadi mwaka 1985 idadi ya watalii waliofika Zanzibar ilikuwa chini ya 20,000 ambapo hadi Desemba mwaka 2018 idadi ya watalii ilifikia 520,809.

Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema serikali imefarijika na uwekezaji huo na kusisitiza serikali inajali na imekuwa ikiupa umuhimu utalii kwa kutambua mchango wake katika mapato ya nchi.

Mmiliki wa mradi huo wa hoteli, Rustamali Merali Shivji alipongeza ushirikiano mkubwa alioupata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji, na kumshukuru Dk Shein kwa kumshauri kuja kuekeza Zanzibar tokea walipokutana mwaka 2004 wakati alipokwenda kumzindulia hoteli yake ya “New Dodoma Hotel” jijini Dodoma wakati Dk Shein akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Alisema mradi huo wa hoteli ya hadhi ya nyota tano umechukua muda wa miaka minane kukamilika ambao una ukubwa wa mita za mraba 22,000 ambao umegharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 38 huku akisisitiza kuwa mradi huo utasaidia kupanua soko la ajira na Pato la Taifa.

SERIKALI imesema Tanzania inatarajia kupokea watalii wengi kutoka nchi za ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Zanzibar

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi