loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lissu akwama kortini, Ndugai kicheko

ALIYEKUWA Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amekwaa kisiki katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya maombi yake ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai wa kumvua ubunge, kutupiliwa mbali.

Aidha, bungeni jana Spika wa Bunge Job Ndugai alibainisha kuwa jeuri, ubabe na kiburi ni sababu kubwa Lissu kupoteza ubunge. Kwa upande wa Mahakama hiyo imesema kuwa Lissu hakupaswa kuleta maombi hayo na badala yake alipaswa kuleta maombi ya kupinga uchaguzi na sio kuapishwa kwa Mbunge wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu.

Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Sirilius Matupa alisema kuwa baada ya uamuzi wa Spika mambo ya kisheria yalipaswa kutokea mara moja na kwamba maombi hayo yangeletwa wakati wa uchaguzi yangekuwa na maana.

Jaji Matupa alisema ili maombi ya Lissu yatelekezeke ni lazima kuwapo kwa uvunjaji wa Katiba, kwani jinsi maombi hayo yalivyo yanataka kuwepo kwa wabunge wawili ndani ya jimbo moja.

Alisema kwa kuwa uchaguzi haujapingwa Mtaturu ataendelea kuwa Mbunge na kwamba endapo Lissu angeshinda kungekuwa na wabunge wawili kinyume na Katiba ya nchi Ibara ya 77.

Aliongeza kuwa kwa sasa Mahakama haiwezi kuelekeza mbunge aliyeapishwa kutoka kwenye kiti hicho licha ya kwamba ina uwezo wa kumvua ubunge aliyeko na kumpatia mwombaji baada ya kuwasilisha maombi ya kupinga uchaguzi.

‘’Kwenye maombi haya kuna baadhi ya watu walitakiwa kuwepo ili kesi isikilizwe vizuri lakini hawapo kwa mfano Tume ya Taifa ya Uchaguzi hivyo, ili maombi haya yatekelezeke lazima kuvunjwe Katiba,’’ alisema.

Alieleza haki anayodai mwombaji (Lissu) ipo kwenye Ibara 83 (a) na Sheria ya Uchaguzi kifungu 83 (b) kinaelekeza kufungua shauri la kudai haki mahakamani.

‘’Kesi hii ina mazingira ya aina mbili ya kikatiba na ya kisheria na nikiri wazi kwamba imenisumbua na imenipa wakati mgumu wa kuandika maamuzi kama kesi nyingi zitaletwa kwa mtindo huu,’’ alieleza Jaji Matupa.

Alisema kinachopingwa mahakamani ni uchaguzi na sio kuapishwa kwa Mtaturu kwani ili mtu awe Mbunge ni lazima kuwepo kwa matokeo ya uchaguzi, hati ya kuchaguliwa na kuapishwa hivyo kuapishwa ni haki yake.

Jaji Matupa alisema si vizuri Mahakama kuingilia uapishwaji badala yake inashughulika na uchaguzi na sio uapishwaji. Upande wa serikali katika kesi hiyo uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, George Mandepo, Alicia Mbuya na Lucas Malunde na Mawakili wa Serikali ni Jenipher Msanga na Nkama Musalama.

Mawakili wa mleta maombi ni, Peter Kibatala na Frank Kihwelo. Lissu alifungua maombi hayo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalumu kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Kwa upande wake, Spika Ndugai alieleza kuwa sababu za kiburi na jeuri ndizo pia zilizomfanya Lissu na aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) naye kupoteza ubunge.

Ndugai aliyasema hayo bungeni jana alipomtangaza rasmi mbunge mpya wa jimbo hilo Miraji Mtaturu baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa kubariki kuvuliwa ubunge kwa Lissu jana.

Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Taifa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe imesema itakata rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama.

Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai alilithibitishia Bunge kuwa Mtaturu ni Mbunge halali kutokana na uamuzi uliotolewa na Mahakama.

Alisema kilichomponza Lissu ni jeuri na kiburi kwani pamoja na kuumwa hakuweza kutoa taarifa za ugonjwa wake kwa Spika lakini alionekana akifanya shughuli nyingine katika maeneo mbalimbali.

Alisema mbali ya Mbunge mwenyewe, lakini hakukuwa na taarifa zozote kutoka kwa chama chake, kambi ya upinzani bungeni na hata Mnadhimu wa Upinzani katika shughuli za Bunge, kwa kile alichosema ni kiburi na jeuri.

Alisema jambo kama hilo lilitokea pia kwa aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Nassari.

Alisema suala la wabunge kutoa taarifa kwa Spika wanapokuwa nje ya Bunge na pia kujaza fomu za maadili ni suala la kikatiba na kwamba mbunge anayekiuka hilo anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na si kuonewa. “Mfano mzuri ni Kiongozi wa Upinzani bungeni Mheshimiwa Mbowe.

Alipokuwa magereza Segerea aliniandikia barua akanijulisha kuwa asingeweza kujaza fomu za maadili kwa vile yupo jela, lakini akaniambia nitafanya hivyo nikitoka na kweli akafanya hivyo baada ya kutoka.

“Sasa wewe unakaa kimya mwaka mzima bila kumjulisha Spika chochote mwaka mzima unapita, mwaka wa pili kimya lakini unaonekana ukiendelea na shughuli nyingine huko na mbaya zaidi unayemshambulia huko ndiye huyo ambaye hujampatia taarifa,” alisema Ndugai.

Katika hatua nyingine, akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe, alisema chama chake kitakwenda Mahakamani kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

WATOTO 84,625 waliokuwa na utapiamlo mkali, wametibiwa kuanzia mwanzoni mwa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi