loader
Picha

Mugabe kuzikwa kijijini Kutama

WAKATI Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kiongozi wa ngazi ya Taifa atakayeiwakilisha nchi katika maziko ya kitaifa ya Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, atajulikana leo, jabali huyo wa Afrika atazikwa kijijini kwake Kutama na siyo katika makaburi ya Mashujaa jijini Harare.

Aidha, imesema wizara hiyo haihusiki na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayoonesha orodha ya viongozi wa mataifa mbalimbali watakaoiwakilisha nchi kwenye maziko hayo.

Taarifa hiyo kwa upande wa Tanzania inamtaja Rais John Magufuli, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela, aliliambia gazeti hili jana kuwa, wizara bado haijatoa taarifa kuhusu kiongozi atakayeiwakilisha nchi na itaeleza hilo leo.

“Haijathibitishwa bado kiongozi gani atakwenda. Lakini natumaini mpaka kesho (leo) tutakuwa tumejua,” alisema.

Alipoulizwa kama ana taarifa yoyote kuhusu habari inayosambaa katika mitandaoni ya kijamii ikinukuu chanzo kuwa ni The Independent Observer ikiwataja viongozi wa nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania watakaokwenda kumzika Mugabe, Bohohela alisema wizara hiyo haijapokea wala kutoa taarifa yoyote kuhusu suala hilo.

Mugabe (95) alifariki Septemba 6, mwaka huu nchini Singapore alikokwenda kutibiwa. Mwili wake uliwasili nchini humo juzi tayari kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumapili kesho kutwa.

Katika hatua nyingine, mvutano ulioibuka juu ya mahali atakapozikwa Mugabe umepatiwa ufumbuzi na sasa atazikwa katika kijiji alichozaliwa wiki ijayo, huku kiongozi huyo akiacha wosia kuwa mkewe Grace asiondoke karibu na jeneza lake wakati wote wa mazishi yake.

Awali kuliibuka utata juu ya mahali atakapozikwa mwanasiasa huyo mkongwe na jabali la siasa za Zimbabwe na Afrika, baada ya kuibuka mvutano baina ya familia yake iliyotaka azikwe kijijini kwake na serikali ambayo ilitaka azikwe katika makaburi ya kumbukumbu ya mashujaa wa taifa hilo mjini Harare.

Mpwa wa Mugabe, Leo Mugabe jana aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa, mwili wa kiongozi huyo utazikwa kwa faragha kijijini kwake Kutama.

“Mwili wake utalala Kutama Jumapili usiku na kufuatiwa na mazishi ya faragha yatakayofanyika kati ya Jumatatu au Jumanne lakini si katika makaburi ya mashujaa, huu ni uamuzi wa familia nzima,” alisema Leo.

Baada ya kifo hicho, Rais Emmerson Mnangagwa alimtangaza Mugabe kuwa shujaa wa taifa hilo, hali ambayo ilimaanisha angezikwa katika makaburi ya kumbukumbu ya mashujaa wa taifa hilo mjini Harare.

Hata hivyo, familia yake imepinga wazo hilo, ikisema haikushirikishwa na kwamba machifu wa kabila lake katika kijiji chake kilichopo Jimbo la Zvimba ndiyo wanaopaswa kuamua mahali atakapozikwa kiongozi huyo.

Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa, mojawapo ya maombi ya marehemu Mugabe ilikuwa ni kutaka mkewe Grace, asiondoke karibu na jeneza lake wakati wa mazishi mpaka atakapozikwa.

Rais wa China, Xi Jinping, Rais wa zamani wa Cuba, Raul Castro na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ni miongoni mwa wanaotarajiwa kushiriki mazishi ya kitaifa ya Mugabe yatakayofanyika katika uwanja wa mpira mjini Harare Jumamosi kabla ya mazishi rasmi yatakayofanyika kijiji kwake.

MAMLAKA ya Maji ya Makonde iliyopo wilayani Newala mkoani Mtwara, ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi