loader
Kishindo mazishi Komredi Mugabe

Kishindo mazishi Komredi Mugabe

WAKUU wa nchi mbalimbali Afrika wamesema bara hilo limepoteza shujaa mkubwa wa harakati za ukombozi wa bara hilo, Robert Mugabe (pichani) na kutaka uzalendo na umoja wake uendelee kuenziwa huku Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akitumia muda huo kuomba radhi kwa vurugu walizofanyiwa wageni Waafrika nchini mwake.

Aidha, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema nchi hiyo imefunga rasmi suala la mgogoro wa ardhi akisema kamwe nchi hiyo haitafanya marekebisho ya sheria ya ardhi, na ardhi iliyopo ni ya Wazimbabwe na itatumika kwa ajili ya maendeleo yao na sio vinginevyo.

Viongozi hao wametoa kauli hizo jana kwenye Uwanja wa Mpira cha Rufaro jijini Harare kwenye shughuli ya mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Komredi Mugabe, na kutoa heshima zao kwa mwili wake.

Zaidi ya marais wa sasa 10 walishiriki wakiwamo pia marais wastaafu wa Afrika na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali ambao walimzungumzia Mugabe kama kiongozi shujaa na mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika.

Baadhi ya marais hao ni Uhuru Kenyatta wa Kenya, Edgar Lungu wa Zambia, Filipe Nyusi wa Msumbiji, Dk Hage Geingob wa Namibia, Teodoro Nguema wa Equatorial Guinea, Ramaphosa, Andy Rajoelina wa Madagascar, Peter Mutharika wa Malawi, Joao Laurenco wa Angola na Brahim Ghali wa Jamhuri ya Kiarabu ya Sarhawi.

Akitoa salamu za rambirambi, Rais Ramaphosa alilazimika kuomba radhi kutokana na mauaji na vurugu wanazofanyiwa Waafrika nchini humo, baada ya kuanza kuzomewa aliposimama kutoa salamu zake.

“Niombe radhi kwa kilichotokea Afrika Kusini dhidi ya Waafrika wenzetu, ni kweli kilichofanyika kimekwenda kinyume na makubaliano ya Umoja wa Afrika ambao waasisi wake akiwemo marehemu Mugabe alisisitiza tuwe kitu kimoja na tushikamane,” alisema Rais Ramaphosa.

Aliongeza, “Tukio lile ni baya na hata nyie mmelisema hapa kwa ujumbe wenu na mimi niko nakubaliana na nyie, tunalifanyia kazi kuhakikisha jambo hilo halitokei, sisi sio wabaguzi tunapenda wageni na tunaalika watu mbalimbali kuja kuwekeza hii ndio njia ya kumuenzi Mugabe kiongozi wetu shujaa.”

Naye Rais Uhuru Kenyatta akimzungumzia Mugabe, alisema Afrika imepoteza kiongozi aliyekuwa alama ya ukombozi na mwenye uzalendo na nchi yake lakini pia kwa bara zima.

“Tumempoteza alama ya kweli ya ukombozi wa bara letu, Mugabe alikuwa mstari wa mbele kusema matatizo ya Afrika na alipigania kupatikana kwa suluhu yake, kilichobaki ni sisi viongozi wa sasa kumuenzi mema yake kwa kuungana kuweka maslahi ya wananchi wetu na bara letu, hii ndio nje pekee ya kumuenzi,” alisema Uhuru.

Akizungumzia kifo cha Mugabe na suala la ardhi, Rais Mnangagwa alisema mti mkubwa wa Afrika umedondoka na bara zima liko kwenye majonzi na ili kumuenzi shujaa huyo, Zimbabwe itaendelea kuheshimu mabadiliko ya matumizi ya ardhi yaliyofanywa na Mugabe na kamwe nchi hiyo haitafanya marekebisho ya sheria ya ardhi.

“Zimbabwe kamwe haitafanya marekebisho ya sheria ya ardhi , ardhi yote ni ya Wazimbabwe na sio vinginevyo, na katika kumuenzi baba yetu Mugabe tutaheshimu maamuzi aliyoyafanya kuhusu umiliki wa ardhi na kamwe hatutabadilika,” alisisitiza Rais Mnangagwa aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Mugabe.

Aidha, aliitaka jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo kwani imeshasema wazi ardhi yake itatumika kwa maendeleo, na wameshachukua hatua kadhaa kufanya mapinduzi ya kiuchumi.

Pia aliishukuru Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) kwa kuwa mstari wa mbele kusimama nao na kutaka vikwazo dhidi yao viondolewe.

Akimzungumzia Mugabe, alisema Bara la Afrika lilikuwa limebakiwa na waasisi wawili wa ukombozi ambao ni Mugabe na Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda na sasa Mugabe ameondoka na amebaki mmoja.

“Kwa kweli tunasikitika kuondokewa na kiongozi wa ukombozi wa bara letu walikuwa wamebaki wawili yeye na Kaunda sasa Kaunda kabaki mwenyewe, Mugabe kaenda kuungana na waliom tangulia kama akina hayati Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela na wengine wale waasisi wa ukombozi wa Afrika,” alisema Mnangagwa.

Naye Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyemwakilisha Rais John Magufuli, alisema Tanzania inalia pamoja na Wazimbabwe, na msiba huo ni wa bara lote na Mugabe alifanya mengi yaliyoacha alama.

“Tanzania iko na nyie, tunalia pamoja marehemu Mugabe atakumbukwa daima kwa mema aliyofanya kwa nchi yake, lakini pia kwa Bara la Afrika, alikuwa kiongozi mwenye utu na uzalendo wa kweli,” alisema Samia.

Kwa upande wake, Rais Nguema alisema Mugabe alikuwa mpigania haki za binadamu na mwanaharakati wa kweli wa ukombozi hivyo mchango wake kamwe hautasahaulika.

Wakati Rais Jamhuri ya Kiarabu ya Sahrawi, Brahim Ghali alisema Mugabe atakumbukwa kwa mchango wake wa ukombozi wa Afrika alisema alikuwa kiongozi shujaa wa uhuru na mwenye utu wa kweli.

“Mugabe alikuwa kiongozi mwenye utu,alichukua jambo kama lake na hata sisi watu Sahrawi ametusaidia sana kwenye mgogoro wa mipaka, daima tutamkum buka,” alisema Ghali.

Naye Mwakilishi wa Cuba, Casa Ines- Maria alisema Mugabe alikuwa kiongozi mzuri mwenye kujenga uhusiano bora na mataifa mengine rafiki na kwamba uhusiano wake na marehemu Fidel Castro ulianza zamani na kwamba hadi leo unaendeleo baina ya nchi hizo.

Mwakilishi wa China, Hou Xi Jou alisema Rais Xi Jinping ametuma salamu za rambirambi na kusema Mugabe alitoa mchango mkubwa katika kuhimiza urafiki kati ya China na Zimbabwe na kati ya China na Afrika.

Marais wastaafu wa Afrika waliohudhuria ni Kaunda, Jerry Rawlings wa Ghana, Thabo Mbeki na Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Joseph Kabila wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Olusegun Obasanjo wa Nigeria.

Mugabe (95) aliyeitawala Zimbabwe kwa miaka 37 kati ya 1980 hadi 2017 alipoondolewa madarakani kwa msaada wa jeshi, alifariki dunia wiki iliyopita nchini Singapore alikokwenda akipatiwa matibabu.

Serikali ya Zimbabwe na familia yake imesema maziko yake yatafanyika kwenye Makaburi ya Mashujaa katika Kiwanja cha Mashujaa wa Taifa.

Aidha, tarehe rasmi ya maziko haijafahamika na sherehe za kimila za kumuaga zitafanyika kijijini kwake na hiyo ni kwa mujibu wa taafira za familia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6128f3c9296e67aaae2eb6e04fb126df.jpg

ZAIDI ya wataalamu wa afya ...

foto
Mwandishi: Na Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi