loader
Picha

Nguo za kubana; janga linalowatafuna wanaume, wanawake bila wao kujua

TAKWIMU zilizotolewa na Ofi si ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015/ 2016 zilionesha kwamba, kiwango cha kila mwanamke wa Tanzania kuzaa kimepungua kutoka wastani watoto 6.2 mwaka 1992 hadi 5.2.

Tafsiri ya hali hiyo inaweza kuelezwa kwamba ni kutokana na wanawake wengi kufuata uzazi wa mpango au kushuka kwa viwango vya uwezo wa kushika mimba miongoni mwa wanawake kutokana na sababu mbalimbali. Inawezekana kabisa utafiti mpya ukaonesha kiwango kikiwa kimezidi kushuka.

Wakati hali ikiwa hivyo, uchunguzi uliofanywa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na taarifa zake kutolewa Julai mwaka 2017 ulibaini kwamba, asilimia 33 ya wanaume mkoani Dar es Salaam wana tatizo katika kusababisha mimba.

Akitoa hadharani uchunguzi huo, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Pedro Pallangyo, alisema idadi kubwa miongoni mwa wanaume hao wanasumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu na kisukari.

Lakini daktari na mhamasisha wa damu salama wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), John Bigambalaye, anabainisha kuwa licha ya maradhi ya shinikizo la damu na kisukari kuwa sababu za kiafya zinazowafanya wanaume kutosababisha mimba, nguo za kubana ni janga lingine linalowatafuna wanaume na wanawake katika suala la uzazi.

Katika mahojiano na gazeti hili, mtaalamu huyo anasema wanaume wanaovaa nguo za ndani zisizo-bana huwa na ongezeko la asilimia 25 la uimara wa mbegu za kiume kuliko wenzao wanaovaa nguo za ndani zinazobana.

Anasema hii ni kwa sababu uzalishaji na uimara wa mbegu za kiume haupendelei joto la zaidi ya nyuzi joto 34 za sentigredi. Dk Bigambalaye anasema licha ya baadhi ya wanaume kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya mfumo hafifu wa mbegu za uzazi, wapo wanaopata tatizo hilo kwa kujitakia kutokana na kuvaa nguo za ndani zinazobana.

Anasema baadhi ya mitindo ya nguo za ndani za kubana kama nguo za waendesha farasi, baiskeli, ‘skin jens’ na kadhalika hubana viungo vyao vya uzazi na kusababisha kutokea kwa hali ya joto lisilo rafiki katika uzalishaji wa mbegu. Anasema ni vizuri wanaume wakavaa mavazi ya ndani ambayo hayabani kwani yanasaidia maumbile hayo kupata hewa ya kutosha.

“Kupata watoto ni faraja kwa wanandoa. Wakati mwingine watoto wanakosekana na ndoa kuvunjia kumbe sababu ni ya kujitakia tu kutokana na kuvaa nguo za kubana,” anasema Dk Bigambalaye Anasema suala la uzazi linahusisha vitu vingi na kwamba mwanaume anaweza kuwa na tatizo la mbegu za uzazi, vile vile mwanamke anaweza kuwa na tatizo la mayai kutorutibishwa vizuri.

“Mwanaume akitoa mbegu za uzazi zinatakiwa ziwe zimekamilika kiidadi na lazima ziwe na kichwa na mkia; zinapokuwa na kichwa na mkia tunasema mbegu imekamilika kwani hapo inaweza kufika katika mji wa mimba wa mwanamke,” anasema. Anasema ili safari hiyo ya mbegu ikamilike kunapaswa kuwa pia na ute (mucus) wa kawaida, usiozidi kipimo.

“Ute ukizidi sana unazuia zile mbegu kukimbia kwa kasi matokeo yake zinajikuta zimekaa sehemu moja zikipambana na ule ute kwa vile unakua umezidi na hivyo zinachelewa kufika na kufia njiani,” anasema.

Anasema katika njia ya mwanamke, tindikali ikizidi pia ni tatizo kwa sababu husababisha mbegu kufia njiani kwa kuwa zinakutana na tindikali iliyopitiliza na kuzidhuru kabla hazijarutubisha yai ili mwanamke apate ujauzito. Anasema kuvaa nguo za kubana husababisha mishipa inayotembeza damu mwilini hasa katika mapaja, kibofu cha mkojo na korodani kushindwa kusamba za damu katika baadhi ya maeneo kwa urahisi.

Anafafanua kwamba, mtu anapovaa nguo za kubana saa 24 mwili wake ‘haupumui’ vyema na hivyo kuleta athari katika mbegu. “Kuna mwingine anaweza kutoa mbegu za uzazi, lakini ukizipima hamna kitu ni maji maji tu ambayo hayawezi kumpa mimba mwanamke,” anasema.

Anasema wanaume wanaokwenda hospitalini kwa ajili ya masuala ya uzazi wakiwa wamevaa nguo za ndani zisizobana wanakuwa ongezeko la ubora wa mbegu kwa asilimia 17.

Dk Bigambalaye anasema mbali na nguo za kubana, pia kuna vitu kadha wa kadha vinavyoweza kuathiri mbegu za kiume ikiwemo umri na uzito wa mwili. Tabia nyingine zenye madhara hayo ni pamoja na kuvuta sigara, mazoea ya kuoga maji ya moto kwani mengine joto lake huweza kuwa chanzo cha tatizo.

Kuhusu wanawake wanaovaa nguo za kubana (skini taiti na skini jeans), Dk Bigambalaye anasema wapo hatarini pia kupata maradhi mbalimbali ikiwemo kuharibika kwa mishipa ya fahamu na fangasi sehemu za siri.

Baadhi ya maeneo ambayo huathirika zaidi ni mapaja kwa wanawake, kibofu cha mkojo kwa wanaume, nguvu za kiume na kufa ganzi kwa miguu kwa wanawake. Nguo zinazobana sana husa babisha mishipa midogomidogo inayosafirisha damu kubanwa na hivyo kuathiri usambazaji wa damu kwenye baadhi ya maeneo ya mwili.

Anasema mara nyingi madhara ya nguo hizi hujitokeza kama dalili ya miguu kufa ganzi au hisia za miguu kuwaka moto na kwamba, ni mara chache wahusika hutambua kuwa dalili hizo chanzo chake ni mavazi.

“Unapovaa suruali ya kubana sana, mishipa midogo midogo inayosafirisha damu hubanwa na y maana kuna muda ukivua nguo mwili unawasha. Hiyo ni kutokana na damu ambayo ilishindwa kutembea inavyotakiwa.”

“Kwa kawaida damu husafiri kwa kasi kama maji hivyo misuli inapobanwa, damu hushindwa kusafiri na kusababisha neva za fahamu kufa au kuharibika,” anasema Dk Bigambalaye Anatoa ushauri kwa wanawake na wanaume kuhakikisha wanavaa nguo pana ambazo zinaacha nafasi ya kutosha hasa hasa katika maeneo ya siri.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hosipitali ya Taifa Muhimbili, Cyril Massawe, anaonya wanaovutiwa na mavazi ya kubana hasa vijana, kuwa makini kwa sababu tafiti zimeonesha yana madhara mengi kiafya.

Juni 23, mwaka jana jarida linalohusiana na masuala ya upasuaji wa mfumo wa fahamu na akili (Neurosurgery and Psychiatry), lilionesha kuwa, watafiti katika Hospitali ya Royal Adelaide nchini Australia walihusisha uvaaji wa jeans za kubana na tatizo la misuli lijulikanalo kitabibu kama ‘Compartment syndrome’ lililompata mwanamke mmoja nchini humo.

“Ugonjwa wa mwanamke huyu unaonyesha madhara mapya ya uvaaji wa jeans zinazobana,” anasema Dk Thomas Kimber, mmoja wa watafiti waliotoa ripoti hiyo alipokuwa akizungumza kuhusu madhara ya mavazi ya kubana.

Mtaalamu wa mishipa ya fahamu na mwanachama wa Chama cha Madaktari wa Mishipa ya Fahamu cha Marekani (AAM), Dk John England, anasema: “Mishipa ya fahamu kwa baadhi ya watu, inaweza kukandamizwa kwa urahisi.”

Anaongeza: “Mshipa unaotoka kwenye nyonga na kuingia mapajani kwa ajili ya kuchukua hisia, unaweza kubanwa na kitu chochote kinachobana mapaja au eneo la kiuno.”

Anasema hali ya kubanwa kwa mishipa ya fahamu kama itakuwa ya kujirudiarudia, inaweza kusababisha madhara ya kudumu. Kwa msingi huu hapana budi ifahamike kwamba kwa wanawake, nguo zinazobana kupita kiasi zinaweza kusababisha damu kuganda ndani ya mishipa, uvimbe wa mishipa ya damu kwenye miguu na magonjwa ya fangasi ya ngozi yanayoambatana na muwasho.

Hii inaweza kutokea kwa sababu ya jasho linalozalishwa kwa wingi katika nguo zinazobana hufanya ngozi ikose hewa safi. Uvimbe wa mishipa ya damu miguuni maarufu kama ‘varicose veins’, ni moja ya matatizo yanayowapata mara kwa mara wanawake wajawazito na wale wanaotumia vidonge, vipandikizi na sindano za kupanga uzazi bila kufanya mazoezi ya mwili.

Tatizo lingine la nguo za kubana kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2004 katika toleo namba 117(2) la Jarida la Ejog (Europian Journal of Obstetrics & Gynaecology and Reproductive Biology) ni ongezeko la kuzaliana kwa bakteria waharibifu wanaosababisha mwanamke kutokwa na uchafu sehemu za siri. Jarida hilo linasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa wanawake wanene na watu wenye tatizo la ugonjwa wa kisukari.

Kwa wanaume, mavazi haya yanaweza kuathiri utendaji wa figo pamoja na kibofu cha mkojo sambamba na urahisi wa maambukizi katika njia ya mfumo wa mkojo. Mavazi ya kubana yanaweza pia kusababisha uvimbe wa mishipa ya korodani na kuathiri ubora wa mbegu za kiume zinazozalishwa.

Hali hii wakati mwingine huwa ni chanzo cha ugumba na upungufu wa nguvu za kiume kutokana na athari za maumbile ya kianatomi pamoja na athari za kisaikolojia.

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Na Vicky Kimaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi