loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanahabari na mchango wao kuboresha maadili

WIKI iliyopita tuliangalia namna wanaharakati wenye uzalendo wa kweli katika nchi yetu, wanavyoweza kusaidia katika kuboresha maadili ya utumishi wa umma. Tukasema wanaweza kufanya hivyo kwa kuibua mambo mbalimbali ya kweli na yenye nia njema ya kulijenga na siyo kulibomoa taifa.

Leo tunaangalia namna wanahabari wanavyoweza kusaidia katika kuboresha maadili ya utumishi wa umma kwa kuzingatia mambo mbalimbali muhimu, kwa mujibu wa taaluma zao.

Wengi wetu tukisikia nafasi ya wanahabari, katika kuboresha maadili kwenye utumishi wa umma, kitu cha kwanza tunachofikiria ni namna wanavyoweza kufichua maovu mbalimbali yanayofanyika kinyume na maadili, katika utumishi wa utumishi wa umma.

Kufichua maovu ni jambo la msingi kwa wanahabari na kuna taratibu zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika na wanachokiandika, kuangalia kama hatua yao ya kuandika italeta manufaa pamoja na kusikiliza pande zote ili kutoa taarifa ambayo inajitosheleza (balanced story).

Ni katika muktadha huo, wanahabari wana nafasi kubwa kwenye kuboresha maadili ya watumishi wa umma na kwa maana hiyo wana mambo mengi zaidi ya kufichua ukiukwaji wa maadili katika utumishi wa umma.

Kwa mfano, waandishi wa habari wanaweza kutumia nafasi yao, katika kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu, wanapongezwa kwa namna mbalimbali zinazoweza kuwafanya watambulike na umma na hata kuwafanya wawe mfano kwa wengine.

Bila shaka tumeshawahi kusikia Rais John Magufuli, akitaja baadhi ya watumishi ambao wamefanya mambo makubwa yenye kuashiria uadilifu wa hali ya juu.

Kutajwa huku kunaweza kukawa ni namna mojawapo kwa wanahabari kufuatilia na kumwelezea vizuri mtu kama huyu ili awe mfano kwa watumishi wengine.

Jumatatu wiki hii wakati akizindua rada nne za kisasa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam alimsifia hadharani Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari, kwa utendaji mzuri uliotukuka.

Vilevile, wanahabari wanaweza kufuatilia kesi mbalimbali zilizomalizika katika siku za nyuma na za hivi karibuni, ambazo ziliwatia hatiani watumishi wa umma waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya jinai, ambayo yanahusisha ukiukwaji wa maadili na kuzielezea kesi hizo kinagaubaga kwa umma.

Vilevile, waandishi wa habari wanaweza kufuatilia na kuzifanyia uchambuzi wa mara kwa mara ripoti za mkaguzi mkuu wa mahesabu ya serikali na kuuweka uchambuzi huo bayana na kwa lugha inayoeleweka kwa wananchi wote na wadau mbalimbali, wakilenga kufichua viashiria vya ukosefu wa maadili, ili viweze kufanyiwa kazi.

Katika kufuatilia masuala mbalimbali kuhusu maadili ya watumishi wa umma, wanahabari wanapaswa kuangalia kwa karibu utendaji wa watendaji katika utumishi wa umma, badala ya kutumia muda mwingi kuangalia watumishi wa kisiasa peke yao.

Vilevile, wanahabari wanatakiwa kuhakikisha kuwa macho yao yanaelekezwa siyo tu kwa serikali kuu, bali pia katika serikali za mitaa pamoja na taasisi zingine za umma kwa kuandika mazuri yanayofanyika ili yaimarishwe na yanayoonekana kuwa mabaya yasitishwe.

Pia, wanahabari makini wanatakiwa kuhakikisha siyo tu wanamulika mambo makubwa yenye kuleta kashfa kubwa kwa watumishi wa umma, bali pia waangalie mambo madogo madogo ambayo licha ya madhara yake kutoweza kuonekana kwa haraka, kesho yanaweza kuwa makubwa na kuleta athari mbaya kwa taifa.

Wanahabari vilevile, baada ya kupata taarifa mbalimbali, wanaweza kujenga utamaduni wa kushauriana na taasisi husika, kabla ya kurusha mambo kwenye vyombo vya habari.

Ili wanahabari waweze kuwa na uhalali wa kufuatilia ukiukwaji wa maadili kwingineko inabidi waanze kwa kujijengea uadilifu wao wenyewe kwa kutekeleza kazi zao kulingana na maadili ya taaluma zao, hali itakayowawezesha kuwa na haki sahihi (moral authority) ya kufuatilia ukiukwaji wa maadili katika sekta zingine za utumishi wa umma.

Vilevile, wanahabari lazima wawe na hamu na jitihada za kujifunza vizuri juu ya mambo yanayohusu taasisi wanazozishughulikia katika kufuatilia maadili ili waweze kutenda haki kwa mujibu wa sheria pale wanapofanya ufuatiliaji kuhusu maadili ya watumishi.

Kwa kuhitimisha, ni vizuri wanahabari wakajijengea uwezo wa kuhamasisha wasomaji na wasikilizaji wao kwa namna mbalimbali ili waweze kuchagua na kusoma au kusikiliza habari zinazohusu maadili na hasa kwa kukizingatia kuwa, katika makala yake ya mwaka 1995, Warren Francke alipata kusema, ni vigumu sana kutabiri kile ambacho wasikilizaji au watazamaji wa vyombo vya habari watakichagua wanapoletewa habari mbalimbali.

foto
Mwandishi: Na Dk Alfred Nchimbi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi