loader
Picha

Mkoa wa Katavi na vivutio lukuki vya utalii

MKOA wa Katavi ni mojawapo kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Mkoa huu ulianzishwa rasmi Machi 2012 kwa kuumega kutoka Mkoa wa Rukwa, una wilaya nne za Mpanda Mjini, Mpanda Vijijini, Mlele na Tanganyika.

Mkoa huu unafahamika zaidi kutokana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ambayo ni mojawapo ya hifadhi za taifa 16, ikiwa inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa kati ya hifadhi zote Tanzania baada ya Ruaha na Serengeti.

Kwa mujibu wa wenyeji, jina la mkoa huo limetokana na jina la asili la mwindaji maarufu wa kienyeji aliyeishi katika maeneo ya hifadhi akijulikana kama “Katabi”.

Wenyeji hao wanaamini Katabi ni mzimu wa kabila la Wabende ambapo mpaka leo wanafika katika eneo hilo, kwenye mti ujulikanao kama ‘Mti wa mzimu wa Katabi’ wakiamini mzimu huo uliishi hapo kabla ya hifadhi.

Inaaminika kuwa mzimu wa Katabi una uwezo wa kufanya miujiza mbalimbali, ndiyo maana vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo vimekuwa vikiutumia kuomba mahitaji mbalimbali kwa mujibu wa imani zao.

Mila na desturi za wenyeji wanaoizunguka hifadhi ya Katavi haziruhusu uharibifu wa mazingira, wanaamini katika yale yaliyokatazwa na mizimu yao, kama kukojoa kwenye msitu na nyika yao ya matambiko, kukata na kung’oa miti.

Kutokana na utii huo kwa mizimu yao, inasemwa kuwa hifadhi ya Katavi ndiyo pekee nchini ambayo bado ina mazingira yake ya asili.

Mila na desturi za wenyeji, zinapochanganywa na vivutio vingine vilivyomo kwenye hifadhi hiyo, kwa pamoja vinaipa hifadhi ya Katavi mvuto wa kipekee kwa utalii.

Vivutio Hifadhi ya Katavi Katavi ni hifadhi yenye vivutio vingi, baadhi vikiwa havipatikani sehemu yoyote duniani. Ina vyanzo vitatu vya maji ikiwemo Ziwa Katavi, Mto Katuma na maeneo mengine.

Uwepo wa vyanzo hivyo vya maji umefanya eneo hilo kuonekana kuwa ni nyumbani kwa viboko na mamba, kwani kuna idadi kubwa ya viboko na mamba.

Katika eneo hili ni kawaida kushuhudia mapigano kati ya viboko na mamba. Pia eneo la Ziwa Katavi kuna nyati, tembo, swala, chui, simba, pundamilia wengi na zaidi ya aina 400 za ndege.

Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Katavi ilitangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa mwa- ka 1974 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 2,253 na ilipofika 1996 iliongezwa eneo na kufikia kilometa za mraba 4,471.

Kama ukifika katika Hifadhi ya Katavi utapata fursa ya kujionea wanyama pori wengi yakiwemo makundi makubwa ya tembo, nyati, simba, pundamilia, mbwa mwitu, kongoni, swala pala na nyemela.

Eneo la Mto Stalike na Iku ni kivutio kingine kikubwa cha utalii kutokana na mapi- gano ya makundi ya viboko na mamba, pia kuna idadi kubwa ya vipepeo na ndege wa aina mbalimbali na mandhari pana ya uwanda tambarare wa nyasi katika mkondo wa bonde la ufa la Rukwa.

Uoto huo wa asili una aina 226 za miti, mito na vijito vinavyoingia na kutoka katika eneo la hifadhi. Kwenye uwanda huo wa nyika, wenyeji hufanya matambiko yao, watalii huburudika kwa kujionea nyika hiyo kubwa kuliko zote nchini, makundi makubwa ya wanyama wakubwa kama vile nyati, tembo, twiga, pundamilia na viboko.

Ukiwa katika hifadhi hiyo unaweza kutazama wanyama kwa kutumia gari, hasa nyakati za asubuhi ambapo wanyama wanakuwa wamepumzika.

Pia matembezi mafupi yanayojulikana kama “Sitalike walking Trail” kuanzia kilomita moja hadi hadi tisa. Kwa wanaopenda kutembea, yapo matembezi marefu (Chorangwa Hiking Trail) ya kilomita 10 na kuendelea ambapo mtalii ana uwezo kutembea kwa saa 10.

Pia ndani ya hifadhi ya Katavi, mtalii anaweza kufanya utalii wakati wa usiku kumwezesha kuona wanyama ambao mchana hawaonekani kirahisi, akiwa kwenye gari la wazi na lenye taa maalumu. Kwa mujibu wa tovuti za utalii, Hifadhi ya Katavi ndiyo makazi ya makundi makubwa ya nyati hapa duniani na pepo ya asili, ikiwa imehifadhi mazingira yake ya asili, kwa kutoathiriwa na shughuli za binadamu.

Utalii ikolojia Nkondwe Mwaka 2013 mkoa wa Katavi kupitia halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ulifikiria kuwepo kwa ukanda wa utalii ikolojia.

Hivyo ulitenga eneo lenye ukubwa wa hekta 5,036 kwa ajili ya utalii ikolojia. Hali hii ilikuja baada ya kuona watalii wengi wanaofika katika hifadhi ya Katavi mkoani Katavi, na hifadhi za Gombe na Mahale mkoani Kigoma wanakosa namna ya kuunganisha usafiri kwa ajili ya utalii kati ya hifadhi hizo tatu.

Hivyo hatua hiyo ili- chukuliwa kufuatia eneo la Nkondwe lililo katikati ku- onekana kuwa ni eneo pana na lenye vivutio vingi sana vya utalii na vinavyoweza kumfanya mtalii akaendeleza utalii katika maeneo hayo.

Eneo hilo tengwa la ukan- da wa utalii ikolojia linavyo vivutio vingi ambavyo ni pamoja na eneo la majimoto, maporomoko ya Nkondwe, chemchem ya asili ya maji ya Mto Sabaga, mto wenye miamba mikubwa mwanzo- mwisho, safu za milima ya ikolojia ya Kalutwe, wanyama aina ya sokwe mtu, ambao ni adimu kupatikana duniani n.k.

Kimsingi utalii ikolojia umelenga kufungua vivutio katika maeneo yanayozun- guka hifadhi hizo tatu, na malengo ya utalii ikolojia ni kuhamasisha uhifadhi pamoja na kupunguza madhara yaletwayo na utalii, na unahusisha watu wachache tofauti na ule utalii tuliouzoea wa asili.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga, mwaka 2017 alieleza kuwa Mkoa wa Katavi una ukanda mzuri wa Ziwa Tanganyika, unaofaa kujenga hoteli za kitalii, na kuna eneo la majimoto linaloweza kutembelewa kitalii.

“Pia tunayo maporomoko ya maji ya Nkondwe, ambapo muda wote kwa mwaka mzima maji hut- iririka, na halmashauri yetu ya Mpanda iko kwenye mchakato wa kuingia makubaliano na Taasisi ya Jane Goodall iliyoko Kigoma kuja kuwafundisha sokwe mtu ili waweze kuwazoea binadamu waliopo katika maporomoko ya Nkondwe,” anasema Muhuga na kuongeza, “Mkoa wa Katavi unao sokwe mtu wengi wanaokisiwa kuwa 1,000 ukilinganisha na Kigoma ambao wana sokwe 342, lakini utaona kuwa Kigoma wananufaika nao, sisi ambao tunao wengi hatunufaiki nao, hivyo sasa tumeshachukua hatua na tunaishukuru Taasisi ya Jane Goodall kukubali kuja kuwafundisha (sokwe mtu) ili kuboresha utalii katika mkoa wetu,” anasisitiza Muhuga.

Mkuu huyo wa mkoa ambaye alistaafu mwezi Julai 2018, anasema kuwa pia lipo eneo jingine la utalii wa ikolojia lenye chemchem ya maji yanayosukumwa juu la Sabaga, na ipo mikakati ya kutaka watalii wengi watembelee na kujionea vivutio hivyo.

Pia Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imekuwa na mikakati mingi kuhakikisha eneo hilo linavutia na kuweza kupokea wageni kwa ajili ya kufanya utalii katika maeneo yote ya hifadhi zote tatu.

Mchakato wote unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Jane Goodall ambayo imekuwa ikifanya kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda katika uhifadhi ili kutengeneza miundombinu na kuhakikisha ukanda wa utalii ikolojia unahifadhiwa.

Matarajio makubwa ya mkoa wa Katavi yalikuwa utalii katika ukanda huo utafunguka kimiundombinu, kwa maana ya barabara za kutoka Kigoma kwenda Katavi, Katavi Tabora na Katavi kwenda Rukwa, ambazo baadhi zimekwisha boreshwa ili ziweze kufikika kiurahisi.

Vile vile mkoa huo unategemea kuunganisha ukanda wa pwani ya Ziwa Tanganyika, kwenye vijiji vya Kalema na Ikola, ili mtalii akimaliza kutalii katika eneo la utalii ikolojia pamoja na kuangalia vitu vya kiasili katika kijiji cha Vikonge bado anaweza akasafiri kwenye pwani ya Ziwa Tanganyika.

Wakati Maonesho ya Utalii yakianza leo, ni vyema sasa ukaanza kufikiria kutembelea eneo hili la utalii kuliko dhana iliyozoeleka ya kudhani kwamba vivutio vingi vya utalii viko mikoa ya Kaskazini. 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

1 Comments

  • avatar
    FINEHAS MUKANGARA BWIRE
    20/09/2019

    Gazeti la Serikali linapaswa kuandika na kuonyesha picha zilizo sahihi.Hawa wanyamapori mnaowaonyesha siyo SOKWE MTU-chimpanzee bali ni GORILLA.Nchini Tanzania hatuna SOKWE-GORILLA bali tunao SOKWE MTU-Chimpanzee.Pia siyo kweli kwamba sokwe mtu ni adimu kupatikana duniani.Wametapakaa kwenye maeneo mbalimbali ndani ya miinuko/milima yenye misitu magharibi mwa Africa kusini ya jangwa la Sahara!

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi