loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera RPC Dodoma kuzuia usafirishaji holela wa mafuta

MOJA ya janga kubwa ambalo Tanzania haitasahau ni ajali ya moto, uliotokana na mlipuko wa mafuta mkoani Morogoro hivi karibuni, ulioua jumla ya zaidi ya watu 100.

Mlipuko huo ulisababishwa na watu wengi, kutojua hatari inayowakabili na pia kutokuwepo na hadhari miongoni mwa wahusika na wananchi kwa ujumla wao.

Somo lililopatikana katika ajali hiyo ni kubwa mno kwa watanzania, hasa wanaopenda kuishi kwa amani na usalama.

Ndio maana tunasema hatua iliyochukuliwa na Polisi mkoa wa Dodoma, ya kupiga marufuku usafirishaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwenye mabasi ya abiria yaendayo vijijini, ni ya kutia moyo na kuonesha utimamu wa ulinzi na usalama kwa upande wa jeshi hilo mkoani hapo.

Pamoja na kuwasifu kwa hatua waliyoichukua, tunapongeza na kauli yake thabiti ya kutaka mamlaka zinazohusika, kutafuta utaratibu mwingine wa kusafirisha mafuta hayo.

Ukiangalia takwimu za jumla ya mabasi matano ya abiria, kunaswa na lita 1,277 za petroli na lita 850 za dizeli, unaweza kuona ni kiasi gani mabasi hayo yalikuwa ni mabomu halisi ya kuteketeza maisha ya mamia ya wananchi wanaosafiri na jirani zao, kama ajali itatokea. Ipo historia katika usafiri wa nchi hii, ukiachia janga la Morogoro, basi la Kampuni ya Mabasi ya Taifa (KAMATA) lililokuwa linakwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, liliteketea baada ya kupata ajali eneo ambalo watu walikuwa wamechoma moto msitu.

Hivyo ni dhahiri kutembea na mafuta katika mabasi ya abiria, siyo salama hata kidogo. Hatua aliyoichukua Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Dodoma, Gilles Muroto kufanya msako katika mabasi yaendayo vijijini eneo la Kikuyu katika jiji la Dodoma, inastahili kuigwa na makamanda wengine kwa kuwa tabia hiyo imezoeleka na ni ya hatari.

Ukamataji wa magari ya abiria matano, yakisafirisha mafuta ya petroli na dizeli pamoja na abiria na mizigo mingine katika hali ya hatari, ndio unatufanya tuone nia njema ya kamanda katika kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama.

Katika hesabu za kawaida, basi la abiria kuwa na madumu 55 kwenye buti, likisafiri katika barabara yenye mashimo na tabia za watu katika maeneo ya ‘kuchimba dawa’ kuvuta sigara, hakika tulikuwa tunasubiri janga jingine.

Pamoja na kupongeza kamanda huyo kwa hatua zake na kushauri wengine kuiga, tunaiomba Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Maji na Nishati (Ewura), kuangalia namna ya kusaidia wananchi wa vijijini jinsi ya kupata nishati kwa njia salama zaidi.

Ni kweli kama alivyosema Kamanda Muroto ni lazima utaratibu utafutwe wa jinsi ya kufikisha mafuta ya petroli na dizeli vijijini, lakini si kwa stahili hiyo ya kuyasafirisha kwenye mabasi ya abiria.

Nao wawekezaji wanatakiwa kuangalia ni kwa namna gani, wanaweza kuyatoa mafuta mijini hadi vijijini kwa usalama zaidi, ili taifa hili lisiendeleee kusubiri majanga na kuwajibika katika kuyahudumia.

KUANZIA leo hadi Jumapili wiki hii jijini Dodoma, Chama Cha ...

foto
Mwandishi: TAHARIRI

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi