loader
Picha

Jamii ya Kimasai na janga la ukeketaji

KATIKA vipindi vya likizo, baadhi ya jamii nchini huendesha shughuli za kimila zikiwamo za ukeketaji unaoaminika na jamii nyingi kuwa, ni moja ya mambo muhimu kufanyiwa wasichana na wavulana waliofi kia umri ili wakubalike na kuingizwa katika rika la utu uzima.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, mwanamke mmoja kati ya 10 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 amekeketwa na kati yao, asilimia 35 wamekeketwa kabla ya umri wa mwaka mmoja.

Uchunguzi wa muda mrefu katika maeneo mbalimbali nchini umebaini kuwa, katika jamii hizo, vipindi hivyo huwa na sherehe mbalimbali hadharani kuwapongeza na kuwatuza mabinti waliokeketwa huku damu zikiwachuruzika miguuni kutokana na kujeruhiwa huko kupitia ukeketaji.

Mmoja kati ya ngariba 169 walioachana na kazi hiyo baada ya kuona madhara yake na kupata elimu kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwamo taasisi ya HIMD, Esther Kallanga anashuhudia katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mradi wa Paza Sauti unaodhaminiwa na Internews jijini Dar es Salaam, athari za kazi hiyo mbele ya wanahabari.

Anasema: “Kwa kawaida, unapokeketwa unatakiwa kujikaza, usipige kelele, pale unavumilia ukishakatwa kama hujatoa chozi, au kujitingisha hata jicho tu, tunapiga ndulu; ile ni ishara kuwa binti amekua na sasa ameingia kwenye utu uzima, ni kitendo cha kishujaa na heshima kwake.” Anasema:

“Huwa tunawafanyia wengi, hata 100 kwa mwezi, boma moja unaweza kukuta mabinti 10 hadi 20, hiyo ni familia ya mtu mmoja tu, yaani watoto wa baba mmoja mama tofauti,” anasema Ngariba huyo ambaye, hata hivyo ameamua kutupa zana zake baada ya kupata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji.

Anasema msimu wa ukeketaji katika maeneo yake ya jamii ya Kimasai ni mwezi wa sita na mwisho wa mwaka shule zinapofungwa na kwamba, imebainika kuwa katika msimu huu huwapo wimbi kubwa la watoto wa kike kutimka (kutoroka) kwenda kuelekea maeneo mbali mbali ya miji kuepuka kukeketwa na familia zao.

NGARIBA WENGINE WAMFANYIA VURUGU BAADA YA KUSTAAFU Anasema: “Unajua kupitia ungariba unapata utajiri mkubwa, unapewa mifugo mingi, unapewa hela, unaheshimika katika jamii, sasa kuna baadhi hawataki kuacha kazi hii, hata nilipowaelimisha madhara ya kuacha, walichonifanyia ni vurugu, walienda kukusanyana wakawa wengi wakaja nyumbani kwangu kunivuruga na kutaka kunipiga, hata sasa wapo ambao hawaongei na mimi; ni kama wamenitenga.”

“Wanaamini ukifanya ukeketeaji huu unapoteza hamasa na hisia zaidi za kutaka wanaume, kumbe siyo kweli na ukiangalia wengi waliokeketwa ndio inawaongezea spidi ya kutembea na mwanaume huyu, na yule na mwingine,” anasema.

Tapwaa ni mmoja wa wasichana wa jamii ya Kimasai aliyeamua kukimbia makazi yao na kukimbilia Ngarenaro Arusha kwenye kituo cha Health Integrated Development (HIMD) kupata hifadhi ili kujinusuru na kadhia hiyo ya kukeketwa.

Alilazimika kutoroka kwao majira ya saa tisa usiku kukwepa kitendo hicho. Tapwaa anasema: “Nilikuwa nalazimishwa kukeketwa na kuolewa, sikuwa tayari, nilishaona dada zangu na majirani zangu, ambao wengine wamepoteza maisha kwa kupoteza damu nyingi, sikutaka hayo mambo yanikute.”

“Nashukuru nilibahatika kwenda shule, na shule niliyokuwa nasoma tulitembelewa na waelimishaji rika waliotufundisha madhara ya ukeketaji; nikachukua namba zao za simu.”

“Nilipomaliza kidato cha nne mwaka jana 2018, baba akaniambia ni lazima nikeketwe na niolewe, hakutaka hata kusubiri matokeo ya kidato cha nne, nilikaa na mama yangu nikamueleza kuwa nisingependa kukeketwa na kuolewa kwa sasa, mama akaniuliza sasa tunafanyaje?” anasema Tapwaa na kuendelea.

“Nilikuwa na wazo la kutoroka lakini nitatorokaje bila ya kukamatwa, kwa vile mama alinielewa akaniambia niende kwa mama yangu mdogo, nikamwambie huko pia hakupo salama, ni rahisi mimi kufuatwa na kukeketwa, nikamwambia mama kuna waelimishaji rika nawafahamu nitaenda huko.

”Anasema mama yake alimwelewa na kumsaidia kupanga mipango ya namna ya kumwezesha binti huyo kuondoka kijini kwao Engaruka wilayani Monduli katika mkoa wa Manyara, bila kukamatwa.

“Mama alinielewa, akanichorea ramani yote ya namna nitakavyoweza kutoroka kijijini kwetu hadi nifike mjini bila tatizo…” anasema Tapwaa.

SAFARI YA USIKU WA MANANE Tapwaa anasimulia namna alivyokimbia mila hiyo hatari kimwili, kiafya na kisaikolojia akisema aliamka kwa kunyata saa tisa za usiku na kuanza safari ya kwenda kijijini Selela kwa miguu.

“Siku hiyo kulikuwa na giza sana; nilikuwa naogopa sana, na nilichomwa na miba njiani maana nililazimika kutembea msituni kwa kuhofia kuwa, nikipita barabarani, nitaonekana na nikionekana basi nitakamatwa na kurudishwa nyumbani.”

Anasema: “Kutoka kijiji chetu cha Engaruka kwenda Selela kuna wanyama wakali kama simba, chui na wanyama wengine, nilikuwa naogopa kweli na ilifika wakati machozi ya uchungu yakanitoka.”

“Nilikuwa naomba Mungu wanyama wasinidhuru na pia nisikamatwe na kurudishwa kijijini Selela na kadri nilivyokuwa natembea, ndivyo kulivyozidi kupambazuka, nashukuru Mungu nikafika kijijini Selela saa nne asubuhi siku iliyofuata.”

Anasema kutoka pale, alipanda basi hadi Mto wa Mbu alipowasiliana na mwelimishaji rika mmoja aliyemwelekeza mahali wanapopaswa kukutana. “Alinipeleka kwake nikalala, akanisaidia kunifikisha Arusha na kunipeleka kituoni….. na hivyo ndivyo ikawa namna nilivyoweza kuepuka kukeketwa,” anasema Tapwaa.

“Nilikuwa nahofu ya kudhuriwa na wanyama, lakini niliona ni bora niliwe na simba au kuliwa na wanyama wengine, lakini siyo kudhuriwa na binadamu ambao wangenikeketa.

“Kuna wenzangu niliwashuhudia wakikeketwa na kupoteza maisha katika maumivu makali, sikutaka hali hiyo inikute,”anasisitiza.

‘MAMA AMEPATA KIPIGO KWA AJILI YANGU’ Tapwaa anasema baada ya kubainika ametoroka, kwa vile baba yake alishamwambia mama yake amwandae binti yake tayari kwa kukeketwa na kuolewa siku mbili zijazo, kitendo cha kutoroka kilimweka matatani mama yake.

“Nilikuja kupata mawasiliano ya mama nilivyofika kituoni, mama akanielezea mateso aliyopata kwa ajili yangu, alivyopigwa na kunyanyaswa kwa ajili yangu kwa kuwa baba alisema mama ndiye sababu ya kutoroka kwangu, na inakuaje ajichukulie majukumu ya watoto, hayo madaraka ameyapata wapi.” FAMILIA INAMTENGA TAPWAA Binti huyo anayelelewa katika kituo cha HIMD anasema:

“Familia yetu imenitenga, lakini mimi naona ni sawa tu ni bora wanitenge, lakini siyo kunifanyia ukatili…” “Ninajitaidi niweze kutimiza ndoto zangu ili nitakaporudi nyumbani, niwe ninajiweza kiuchumi na asiwepo mtu wa kunibabaisha maana nitakuwa na maamuzi yangu mwenyewe.”

Anasema kwa sasa hana mawasiliano na familia yao, na kwamba hataki kujua kinachoendelea huko kwani azma yake ilikuwa kujiokoa, hivyo anapambana na maisha yake.

“Kwa sasa napigania ndoto yangu; kituoni nimejikita kwenye mradi wa kilimo cha mboga mboga na ufugaji kuku, lakini hata hivyo nipo kwenye mchakato wa kujiunga na chuo cha hotelia.

“Nikimaliza kusoma nikawa na kazi yangu nitarudi nyumbani, nitarudi nikiwa na kipato changu, najua hakuna atakayenilazimisha kukeketwa maana nitakuwa simtegemei mtu, nitakuwa na kipato changu mwenyewe na hivyo ni rahisi kufanya maamuzi yangu,” anasema.

MKASA YA MAJONZI Manusura huyo wa ukeketaji anasema amewahi kuwashuhudia wasichana wa jirani wakipoteza maisha na hata watoto, lakini kuna msichana mmoja alikuwa hataki kukeketwa wakawa wanamshurutisha akawasukuma ngariba na kukimbia.

“Wakatumwa vijana wa kiume kumkamata, kwa hiyo alivyokamatwa alikeketwa visivyo na mpaka sasa amekuwa mlemavu….”

LEIGWANANI ATAKA SHERIA KALI Mwenyekiti wa Kitaifa wa Leigwanani wa Jamii ya Wamasai Tanzania, Isack Leksongomeijo anasema kwa kawaida mtoto akitoroka kwao, hutengwa na jamii hawezi kurudi tena, kwani akirudi atadhuriwa kwa kuwa kitendo alichofanya kinatafsiriwa kuwa ni uasi katika jamii.

Anapingana na wanaosema tohara kwa jamii ya kimasai imepungua akisisitiza kuwa, wapo wanawake wengi wanaojifungulia kwa wakunga wa jadi na wengine kukeketwa huko kama wametoka katika jamii zisizokeketa sambamba na watoto wadogo, hivyo takwimu sahihi hazipatikani.

“Mkisema tohara imepungua, siyo sawa; haijapungua, inatakiwa tufike mwisho tuseme ukweli, tusifanye siasa, mimi kama kiongozi wa jamii ya Kimasai nimeshuhudia watoto wengi wanapoteza maisha, tunakatisha maisha ya watu.

Serikali itunge sheria kali kuhusu ukeketaji ikiwemo wahusika kufungwa na isimamiwe kwelikweli,” anasema Leksongomeijo. Anasema elimu zaidi inapaswa kutolewa kwa jamii hiyo ili iachane na ukeketaji kwani hauna faida zaidi ya madhara kwa watoto vikiwamo vifo na ulemavu.

“Tuache siasa; anayebainika kushiriki kitendo cha kumkeketa mtoto awe baba, mama au ngariba wote wafunguliwe mashtaka na wafungwe…. Watoto wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya kukeketwa, na kuna watu wananufaika kwa ajili ya ukeketaji, mfano ngariba anapokeketa, anapewa mbuzi moja kwa kila mtoto anayemkeketa na Sh 100,000,” anasema.

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Na Vicky Kimaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi