loader
Picha

Rushwa ya ngono ni mchwa unaotafuna wanawake wengi katika duru za siasa

“KWELI kuna minong’ono ya kuwapo madai ya rushwa ya ngono katika baadhi ya vyama ili wanawake wapate uteuzi katika nafasi mbalimbali au majina yao yapitishwe kugombea uongozi, hasa udiwani na ubunge.”

Anasema Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika Mkoa wa Temeke, Donasian Kessy, anapozungumza na mwandishi wa makala haya ofisini kwake hivi karibuni, mintarafu madai ya kuwapo rushwa ya ngono katika vyama vya siasa hususan katika msimu wa uchaguzi wa kisiasa.

Anaongeza: “Tunapoelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24, mwaka huu na Uchaguzi Mkuu ujao wa mwakani, mwanamke atakayeombwa rushwa ya ngono atoe taarifa Takukuru kupitia namba ya simu 113 ambayo ni bure au katika ofisi ya Takukuru iliyo jirani, tutafika na kufanya kazi; wala wasiogope mazingira ni salama.”

Rushwa ya ngono ni moja ya matendo ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yanayowaathiri zaidi wanawake kazini na hata walio masomoni katika taasisi za elimu ya juu kama vyuo japo hayasemwi hadharani.

Kwa mujibu wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), takriban asilimia 89 ya wanawake katika sekta ya umma, wamepata bughudha za kingono wakati wakitafuta kazi, cheo au huduma.

Hivi karibuni katika siku ya pili ya kongamano la Kamati ya Viongozi wa Dini Mbalimbali kuhusu Nafasi ya Mwanamke Katika Uongozi wa Kuchaguliwa lililowashirikisha wanawake 100 kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), TEC na wawakilishi wa serikali na asasi za kiraia katika ukumbi wa AMECEA Kurasini Dar es Salaam, baadhi ya washiriki walisema katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa kuna madai ya rushwa ya ngono katika baadhi ya vyama hali inayowaogopesha wanawake wengi kugombea.

Katika kongamano hilo, Mwanasheria na Ofisa Programu katika Dawati la Wanawake na Watoto katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Renatha Selemani, anasema: “Katika baadhi ya vyama mpaka mwanamke achaguliwe kugombea, kuna changamoto nyingi ndiyo maana wengine wanasema kuna rushwa ya ngono inayodaiwa kwa wanawake wengi ili wateuliwe kugombea na hali hiyo inawafanya wengine wajitoe kwa kuwa hawezi kujidhalilisha na kudhalilisha familia zao.”

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Idara ya Uinjilishi wa Kanisa la Menonnite Tanzania, Dayosisi ya Mashariki lililopo Upanga, Dar es Salaam, Mchungaji Maira Migire, anasema: “Rushwa ya ngono katika siasa ipo sana…”

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, vyanzo vikubwa vya rushwa ya ngono katika siasa, kazini au katika taasisi za elimu kama shule na vyuo ni mmomonyoko wa maadili, tamaa ya mwili, watu kutokujua haki na wajibu, kutojiamini kutokana na kukosa sifa pamoja na tamaa ya kupata au kujihakikishia upendeleo na huduma kwa haraka.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) kutoka Mkoa wa Singida, Jesca Kishoa amenukuliwa akitaja sababu za baadhi ya wanawake kutoa rushwa ya ngono katika siasa kuwa ni hasa tamaa ya kupata nafasi za uongozi kiurahisi bila ya kupambana.

“Baadhi ya wanawake wanatoa rushwa ya ngono ili wapate uongozi kwa sababu hawana sifa na hawajiamini, kwamba wanaweza kushinda kwenye nafasi hizo” anasema Kishoa na kuongeza: “Ajabu katika maeneo mengine, licha ya mwanamke kutoa rushwa ya ngono ili kupata fursa, bado wanazikosa kwa sababu kiongozi hapimwi kwa ngono, bali kwa uadilifu, utendaji na uwajibikaji wake.”

Anataka wanawake wajiamini, waendelee kuwa waadilifu na watafute nafasi za uongozi kutokana na uwezo wao na asiwepo wa kutaka uongozi wa huruma au zawadi.

Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, waathirika wakubwa wa rushwa ya ngono katika siasa, kazi na taasisi za elimu ni wanawake, hasa wanafunzi na watumishi wa ngazi za chini.

Kutokana na kuwapo minong’ono na vilio vingi vya kuwapo madai ya rushwa ya ngono japo hayasemwi hadharani, hivi karibuni Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kiliendesha mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam kujadili namna ya kuvunja ukimya huo. Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben akasema: “Rushwa ya ngono ipo, lakini haizungumzwi kwa kuwa inachukuliwa kama jambo la kawaida na lisilozungumzwa hadharani jambo ambalo siyo sahihi.”

Mratibu wa Mradi wa Boresha Habari Zuia Ukatili unaofadhiliwa na Internews, Florence Majani analiambia gazeti hili kuwa, vyombo vya habari vinapaswa kushirikiana na jamii kukomesha rushwa ya ngono katika siasa ili kupata viongozi wengi wanawake wanaotokana na kuchaguliwa wakiwa na sifa stahiki na waadilifu.

Akijibu swali la mwandishi katika eneo lake (Takukuru- Mkoa wa Temeke) kama amekwishapata taarifa za matukio ya wanaume kuripoti kuombwa rushwa ya ngono na wanawake walio katika mamlaka, Kessy anasema wanaume wengi inapotokea wameombwa rushwa ya ngono, hufurahia tofauti na hali ilivyo kwa wanawake ambao huumizwa na hali hiyo.

Amesema: “Katika uzoefu wangu, sijawahi kukutana na tukio la mwanaume kuripoti kudaiwa rushwa ya ngono. Na siyo siri kwa wanaume wengi licha ya madhara ya rushwa hiyo; ni vigumu mwanaume aliyeombwa rushwa ya ngono kukataa na mara nyingi hufurahia kama bahati.”

Kessy anasema katika Mkoa wa Temeke, kumekuwa na taarifa mbili za matukio ya kuomba rushwa ya ngono kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kwamba, zipo sababu kadhaa za idadi hiyo kuwa ndogo.

Kwa mujibu wa chapisho moja la Takukuru kuhusu rushwa ya ngono, miongoni mwa athari za rushwa hiyo katika jamii ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, sheria na taratibu za kazi, kuajiri watu au kupata viongozi wasio na sifa, kuzorotesha utendaji wa kazi wa taasisi vikiwamo vyama vya siasa, kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi na kuongezeka kwa mimba zisizotarajiwa hali inayochangia ongezeko la watoto wa mitaani.

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu anasema: “Jamii ijengwe katika kufichua uovu wa rushwa ya ngono unaochangia ongezeko la utoaji mimba katika vyuo na jamii kwa jumla…” Kwa mujibu wa Kessy, changamoto iliyopo katika vita dhidi ya rushwa ya ngono ni hasa watu wengi kukosa ufahamu na ujasiri wa kuripoti wanapodaiwa rushwa hiyo.

“Mwanamke mwingine akiombwa rushwa hiyo kama ni jasiri, anakataa kisha anakaa kimya hatoi taarifa popote, lakini akiwa ni dhaifu, anakubali kisha anakaa kimya, inakuwa siri yao,” anasema Kessy.

Mmoja wa wahadhiri katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) iliyopo Kijitonyama Dar es Salaam, Maiso Nyakogholo (siyo jina halisi), anasema: “Kwa kuwa suala hili ni la kimaadili, lina usiri mkubwa hivyo, ni vigumu mtu kuthibitisha kama kweli lipo ingawa linaweza kuwapo endapo mamlaka husika ina upungufu wa kimbinu katika kushirikisha jumuiya za wanafunzi na walimu au wanachama na viongozi wa chama katika siasa.”

Dk Alfred Nchimbi aliyewahi kufundisha katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Dar es Salaam na sasa ni Mkutubi Msaidizi Mkuu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, anasema, ni vigumu kuthibitisha kuwa rushwa ya ngono ipo vyuoni au katika vyama vya siasa kwa kuwa watu hawaisemi wazi labda kwa kuhofia hatima yao.

“Rushwa hii ni tofauti na ile ya pesa ambayo mtoaji anaweza kuwaambia watu kuwa imebidi nitoe pesa nipate huduma hii, lakini siyo rahisi mwanamke kusema nimefanya ngono ili nipate kitu fulani ndiyo maana rushwa hii haisikiki kama ilivyo rushwa ya pesa na ni vigumu kuithibitisha,” anasema.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007, mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku anaomba au kutoa upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kama kigezo cha kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria, atakuwa ametemda kosa chini ya kifungu hiki.

Adhabu ya mtu huyu faini isiyozidi Sh milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zate mbili kwa pamoja. Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Beatrice Mpembo anataja vikwazo katika vita dhidi ya rushwa ya ngono kuwa ni pamoja na waathirika kutokutoa taarifa kwa wakati, huku wengine wakificha ushahidi, uelewa mdogo wa jamii na tafsiri ya sheria kuhusu rushwa ya ngono.

Anasema kutokana na hali hiyo, hata watuhumiwa wachache wanaofikishwa mahakamani wengi hawatiwi hatiani kutokana na kukosekana kwa ushahidi hali inayofanya kesi zao kufutwa au kutofikishwa mahakamani kabisa.

Anaitaka jamii kutofumbia macho wanaofanya vitendo hivyo na kuwahimiza wanajamii kuwa tayari kutoa taarifa na ushahidi ili kuwatia hatiani wahusika. Uchunguzi umebaini kuwa, mara nyingi katika jamii mwanamke anapomvuta mwanaume katika dhambi ya uzinzi au uasherati na mwanaume kukataa, mwanaume huyo huingia katika hatari ya kupata kejeli kuwa “hajakamilika” jambo ambalo siyo kweli.

Mkuu huyo wa Takukuru Temeke anasema: “Hii ndiyo sababu huwezi kusikia kuna malalamiko ya mwanaume kudhalilishwa kwa kuombwa rushwa ya ngono katika sekta yoyote.”

Ili kumaliza rushwa ya ngono vyuoni, Dk Nchimbi anashauri elimu ya maadili ifundishwe kuanzia katika familia, shule za msingi, sekondari, vyuoni na kazini. “Watu wakubali kuwa tatizo lipo, hivyo lisemwe bila aibu wala woga,” anasema.

Mmoja wa wahadhiri wa kike wa ISW aliyekataa jina lake lisitajwe anasema manufaa ya kukataa rushwa ya ngono ni pamoja na hasa, kulinda heshima na utu, kuwajengea ujasiri wanawake wengine wasiendelee kukubali kudhalilika, haki kutolewa kwa usawa na kuvunja ukimya na kuondoa dhana kuwa, masuala ya rushwa ya ngono hayazungumziki.

WAKULIMA wa Kijiji cha Manda Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ...

foto
Mwandishi: Na Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi