loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chanjo ya surua, rubella na polio ni zawadi ya maisha

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikijizatiti katika kujenga taifa lenye watu wenye siha njema kwa kuboresha huduma za afya nchini kote, mkoa wa Mara kwa upande wake umepanga kutoa chanjo za surua, rubella na polio kwa watoto zaidi ya 390,000.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Chanjo wa Mkoa wa Mara, Beatus Lukona, kampeni hiyo ya chanjo kitaifa ya siku tano itafanyika Septemba 26 hadi 30 mwaka huu katika halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara kwa watoto wenye umri wa kati ya miezi 0 hadi 59.

Kampeni hiyo inayofanyika kila baada ya miaka mitatu, inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa kama siyo kutokomeza kabisa magonjwa ya surua, rubella na polio ambayo yanapopuuzwa husababisha ulemavu wa kudumu na hata vifo kwa waathirika.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, kampeni ya chanjo ya surua, rubella na polio mwaka huu kwa mkoa wa Mara inalenga kuwafikia watoto 394,553 huku Halimashauri za Wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda zikilengwa zaidi kwa sababu ya kuwa chini kiufanisi kutokana na changamoto mbalimbali.

Hata hivyo nia hii njema ya serikali ya kujenga taifa imara na lenye watu wenye afya, wakati fulani imekuwa ikitatizwa na baadhi ya watu wachache wanaozua uongo kadha wa kadha unaosababisha baadhi ya wazazi pia kupata hofu na kushindwa kuwatoa watoto wao kupata chanjo hizo muhimu kwa uhai na usalama wa watoto wao.

Hilo linamwibua Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye mbali na kufungua kampeni hiyo kwa ngazi ya mkoa, anaonya na kusisitiza kuwachukulia hatua kali wazazi watakaoacha kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya na maeneo tengefu ili kupatiwa chanjo hizo muhimu.

“Kwa kuwa kampeni hii ya chanjo ni haki ya msingi kwa watoto wetu, wanastahili kuipata kwa asilimia mia…sitokuwa na msamaha kwa yeyote atakayetatiza zoezi hili kwa namna yoyote na naziagiza kamati zangu zote za ulinzi na usalama za wilaya kusimamia zoezi hili kikamilifu,” anasisitiza Malima.

Anatanabaisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitenga fedha nyingi zaidi katika masuala ya afya kuliko wakati mwingine wowote, hivyo hataacha jitihada hizo za Rais John Magufuri na serikali yake zitatizwe kuwafikia walengwa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, surua ni ugonjwa unaosababishwa na virus aina ya ‘morbillivurus paramyxvirus’ vinavyoenea kwa haraka. Ugonjwa huu huathiri watu wa rika zote, lakini zaidi ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Ugonjwa huu huambukiza kwa njia ya hewa kupitia kukohoa ama kupiga chafya kwenye mkusanyiko na dalili zake ni pamoja na siku chache za mwanzo mgonjwa kuwa na homa kali, mafua, kikohozi na macho kuwa mekundu na kutoa majimaji.

Dalili nyingine ni pamoja na kuanza kutokewa na vipele vidogo vidogo kwenye ngozi hasa ya uso, nyuma ya masikio na hatimaye kusambaa mwili mzima. Madhara yake ni pamoja na masikio kutoa usaha ingawa hauwezi kumzuia mgonjwa kusikia, vidonda vya macho vinavyoweza kusababisha upofu; kupata nimonia, utapiamlo, kuvimba ubongo na hatimaye kifo.

Kuhusu ugonjwa wa rubbela ambao dalili zake zinashabihiana kwa karibu na surua. Ugonjwa huu husababishwa na virus vya rubella na huenezwa kwa njia ya hewa ingawa pia hata mama mjamzito huweza kumuambukiza mtoto tumboni kwa njia hiyo. Ugonjwa huu kama surua, pia huweza kuwapata watu wazima ingawa watoto ndio zaidi.

Dalili zake pia ni pamoja na vipele vidogo vidogo kwenye ngozi, homa na macho kuwa mekundu. Nyingine ni uchovu wa mwili, vidonda kooni, uvimbe kwenye matezi na mafua.

Athari zake hasa pale mama mjamzito anapoambukizwa ni pamoja na kichanga chake kuzaliwa na matatizo yaitwayo kitaalamu (congenital rubella syndrome) ambayo ni pamoja na tatazo la macho na matatizo ya moyo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kitaalamu, madhara mengine ni pamoja na kuzaa mtoto mwenye matatizo ya kutokusikia vizuri, mtindio wa ubongo, matatizo ya ukuaji wa mwili na kuharibika kwa ini na bandama.

Kwa mtu mzima, madhara yake ni pamoja na maumivu ya mwili yasiyo ya kawaida (arthritis), upungufu wa chembe hai nyeupe, maambukizi kwenye ubongo na mishipa ya fahamu (encephalitis & neuritis), kuzaa njiti au kifo.

Aidha, ugonjwa wa polio nao huambukizwa na virusi vijulikanavyo kitaalamu kama polio virus na huweza kumpata mtu wa umri wowote, lakini hasa zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka 15.

Dalili zake ni homa, kuumwa kichwa na mwili, kuharisha na kutapika wakati mwingine kukaza kwa shingo na mgongo; kutoweza kutulia na kuumwa na miguu au mikono na baadhi ya watoto hupooza na hata kufa.

Kinga yake ni chanjo ya matone (OPV) inayotolewa mtoto anapozaliwa na katika wiki ya sita, 10 na 14, wakati chanjo ya sindano (IPV) hutolewa anapotimiza wiki 14.

Hivyo basi kwa kutambua madhara ya magonjwa haya bila shaka hakuna mzazi anayeweza kupuuza kumpatia mwanaye kinga dhidi ya maradhi hayo hatarishi sambaba na chanjo ya matone dhidi ya polio ambazo zote hutolewa bure katika vituo vyote vya afya nchini na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa minajili hiyo.

Watu mbalimbali wakiwamo wataalamu wanakiri kuwa, magonjwa haya huzuilika kwa kinga ya chanjo kwa watoto ambapo mtoto huchomwa sindano mbili za kumkinga zinazotolewa kwenye bega la kushoto mtoto anapotimiza miezi 9 na marudio yake ni pale mtoto anapotimiza miezi 18.

Iwapo kuna mlipuko wa surua, watoto wenye umri wa miezi 6 na kuendelea wanapaswa kupatiwa chanjo hata kabla ya kutimiza miezi 9, ingawa pia ni lazima chanjo hiyo irudiwe pale mtoto anapokamilisha umri wa miezi tisa. Inaelezwa kuwa, magonjwa ya surua, rubella na polio hayana tiba, bali matibabu hutolewa kwa ajili ya kutibu dalili.

Kumbuka kinga ni bora na nafuu maradufu zaidi ya gharama za kuponya.

foto
Mwandishi: Na Fazel Janja

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi