loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Neema zilizopo Pwani zinavyoipaisha Tanzania

BILA Pwani, hakuna maji Dar es Salaam. Huo ndiyo ukweli. Huduma za usambazaji maji zinayofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Taka Dar es Salaam, haziwezi kukamilika bila kutaja jina Pwani.

Haziwezi kukamilika bila kutaja mto Ruvu ambao ni chanzo kikuu cha maji yanayosambazwa na Dawasa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Pwani. Ndiyo maana Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo anasema: “Huu ndiyo uzuri na umuhimu wa mkoa wa Pwani.

Uko kimkakati.” Umuhimu wa mkoa huu kwa mikoa mingine nchini haumulikwi katika eneo la huduma za maji pakee kwa maana ya chanzo na mtambo wa Ruvu Juu na Chini unaosambaza maji katika mikoa hiyo miwili, bali pia umeme wa maji unaotarajiwa kuzalishwa katika bonde la Mto Rufiji. Ndiyo maana mkuu wa mkoa anasema mkoa wa Pwani una majawabu ya masuala mengi muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Yote haya yatazungumzwa siku ya maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji,” anasema Ndikilo wakati akizungumza na wadau mbalimbali juu ya matukio hayo yatakayofanyika kongamano hilo mwezi ujao.

VYANZO VYA MAJI

Wakati mkoa wa Dar es Salaam ukitegemea maji ya Ruvu Juu na Chini, Dawasa ipo kwenye mchakato wa kutumia maji ya mto Rufiji kama chanzo kingine kitakachowezesha maji yanayotosheleza mahitaji. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja anathibitisha hayo akisema kamati imeshaundwa kushughulikia suala hilo.

“Tumetumia fursa ya bwawa la Rufiji linalojengwa na sisi tutajenga mtambo mkubwa wa maji kutoka Rufiji… Tumeshawasiliana na wadau wetu Tanesco ambao ndio wenye bwawa,” anasema Luhemeja katika taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Pwani.

Luhemeja anasema wamewasiliana pia na mkandarasi rasilimali wa bwaw na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhusu mpango huo wa kujenga mtambo wa maji.

Mwakani watawasilisha hoja kwenye Bodi ya Dawasa kwa ajili ya kupata kibali kisha upembuzi yakinifu ufanyike na kazi ianze. Anasema mtambo utajengwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni 200 ambazo ni fedha za ndani. Mradi utaanza Julai mwakani na utatumia miaka mitatu kukamilika.

Anasema: “Tutakuwa na maji ya uhakika kutoka Ruvu Juu, Ruvu Chini na Rufiji.” Uamuzi wa kuongeza chanzo cha maji unatokana na ongezeko la mahitaji katika mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka juzi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo alishauri Dawasa kutafuta vyanzo vingine hususani mto Rufiji, ushauri ambao umetekelezwa.

UMEME BWAWA LA NYERERE

Mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji ni eneo lingine la kujivunia katika mkoa wa Pwani. Huu ni mradi mkubwa ambao jiwe la msingi liliwekwa na Rais John Magufuli Julai 26 mwaka huu.

Ni mradi ambao baada ya kukamilika, Juni 2022, utazalisha megawati 2,115 zitakazoipaisha nchi katika sekta ya nishati. Inaelezwa kuwa mradi huu utagharimu Sh trilioni 6.5 na bwawa litakalojengwa litakuwa la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na la nne kwa Afrika.

Siku ya kuweka jiwe la msingi ndipo Rais Magufuli alipendekeza bwawa hilo liitwe Bwawa la Nyerere. Uamuzi huo unalenga kutambua na kuenzi maono ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliyetaka lijengwe wakati wa uongozi wake.

Serikali imechukua hatua za kujenga bwawa hilo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kutoka megawati 1,601 zinazozalishwa sasa hadi kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025. KILIMO Bonde la mto Rufiji licha ya kuwa chanzo cha umeme wa maji kupitia mradi huo mkubwa, vile vile linatarajiwa kuwa muhimu zaidi kwa kilimo cha mazao mbalimbali.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, nchi ya Kuwait imeonesha nia ya kuwekeza katika kilimo cha miwa ili kuanzisha kiwanda cha sukari. Anasema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Julius Nyerere katika Mto Rufiji, kutakuwa na takribani hekta 150,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kutoka kwenye bwawa hadi kwenye delta.

“Bwawa likishakamilika tutawaambia wawekezaji kutoka Kuwait waje. Uwekezaji utapunguza pengo la upatikanaji wa sukari nchini,” anasema. Anasema eneo hilo linafaa pia kwa kilimo cha michikichi, mpunga, alizeti na mahindi jambo ambalo mkoa unaendelea kukaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa.

Upo pia mradi wa umwagiliaji unaotarajiwa kuanzishwa kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika bonde hilo hatua itakayowezesha nchi kuzalisha mpunga na kusafirisha mchele mwingi kwenda nje.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine anasema mradi huo ni fursa ya kuonesha mabadiliko ya kimiradi yanayoweza kufanyika kuongeza uzalishaji wa mazao na kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.

Ingawa anasema mchele umekuwa ukiuzwa nje ya nchi, anasisitiza kwamba kinachotakiwa ni kuhakikisha soko la nje la bidhaa hiyo linashikiliwa kwa kutumia fursa ya bonde la Rufiji.

Akijibu maswali bungeni hivi karibuni, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba anasema Tume ya Umwagiliaji imeagizwa kuangalia matumizi bora ya ardhi zilizotengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika bonde la mto Rufiji. Tume inatakiwa kuainisha namna gani bonde linaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa (CCM) aliyetaka kufahamu ni kwa namna gani ekari zilizobakia kwenye bonde hilo zitatumika. Mchengerwa alisema katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017, serikali iliahidi kujenga kiwanda cha sukari katika jimbo la Rufiji.

VIWANDA

Sekta ya viwanda ni eneo lingine ambalo mkoa wa Pwani unajivunia kuchangia uchumi wake na nchi kwa jumla. Vipo viwanda 1,192 ambavyo kati yake, 56 ni vikubwa, 85 vya kati, 350 ni vidogo na 704 ni vidogo zaidi. Mkuu wa mkoa anataja bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vikubwa ni za ujenzi; kusindika matunda, kukausha matunda na viwanda vya sabuni.

Anataja pia kiwanda kikubwa cha matofali chenye uwezo wa kuzalisha matofali 15,000 kwa siku kilichopo Mkuranga. Anasema kimepata zabuni ya kuuza matofali kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa umeme katika mto Rufiji.

Taarifa ya mkuu wa mkoa inaonesha viwanda vimezalisha ajira 30,000 za moja kwa moja na 60,000 zisizo za moja moja. Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) inasema upo mpango wa kuanzisha kiwanda cha kusaga mahindi kitakachojengwa wilayani Kibaha.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB anasema benki imeona fursa katika mkoa wa Pwani na itahakikisha inakuwa sehemu ya mabadiliko makubwa. Kiwanda kitajengwa Kibaha na bodi imeshapitisha kwa ajili ya utekelezaji.

Anahimiza wakulima kuona mahindi kama fursa ya biashara ambayo benki inaifungua mkoani Pwani kwa manufaa ya nchi. Ingawa anasema mkoa haujafanya vizuri eneo la viwanda vya usindikaji wa mazao ya shambani na uwekezaji katika kilimo, ufugaji na uvuvi, mkoa unaende lea kuhimiza wawekezaji.

“Tukihamasisha uwekezaji katika kilimo, tutakuwa na mchango mkubwa kwenye kupunguza umasikini,” anasema Ndikilo akisisitiza kuwa wanatarajia maonesho na kongamano kusaidia kuuelezea mkoa na fursa zake kwa ajili ya wawekezaji.

KIWANDA KIKUBWA AFRIKA

Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu chaTanzania Biotech Production Limited (TBPL) kilichopo eneo la TAMCO ni uwekezaji mwingine katika mkoa wa Pwani unaopaisha nchi kitaifa na kimataifa. Hiki ni kiwanda kinachotegemewa siyo tu nchini, bali pia katika Afrika kutokana na kuzalisha dawa za kuua viluilui vya mbu ikiwa ni mkakati wa kukomesha ugonjwa wa malaria.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni kwa ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliotembelea TBPL, inaonesha dawa hizo zinategemewa katika nchi mbalimbali barani. Kiwanda hicho ni pekee katika Afrika kilichojengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya LABIOFAM ya Cuba.

Kilizinduliwa Julai, 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. Lengo la kujengwa ni kutafuta suluhisho la kudumu la mapambano dhidi ya malaria kwa kuua viluwiluwi badala ya kusubiri kuangamiza mbu (waliokomaa). Kilianza uzalishaji mwaka juzi (2017) kwa thamani ya uwekezaji wa takribani Sh bilioni 50.6 kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba.

Kwa jumla, Ndikilo anasema maonesho na kongamano litakuwa jukwaa muhimu na sahihi kumulika ‘neema’ mbalimbali zilizopo Pwani kwa maendeleo ya taifa. Pia, kongamano litaainisha fursa mbalimbali za uwekezaji mkoani Pwani.

Matukio hayo yatakayohudhuriwa na watu wapatao 100,000 yanatarajiwa kuanisha fursa za uwekezaji. Maonesho yataanza Oktoba Mosi hadi Oktoba 7. Upande wa kongamano la fursa za uwekezaji litafunguliwa Oktoba 3.

Kampuni ya Magazeti ya Serikali (Tanzania Standard News Papers- TSN) kwa Kushirikiana na Mamlaka ya Biashara ya Nje (TanTrade) ni waandaaji wa matukio hayo.

foto
Mwandishi: Na Stella Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi