loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kila la heri Yanga, Azam michuano ya Afrika leo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya soka ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga na Azam FC leo zinashuka kwenye viwanja tofauti kucheza mechi zao.

Yanga leo watakuwa Uwanja wa Ravy Mwanawasa wakiwa wageni wa Zesco United ya Zambia katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Wenzao Azam FC wako ugenini Zimbabwe kucheza dhidi ya Triangle mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika wakijaribu kupindua matokeo ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam.

Tukianza na Yanga, katika mchezo wao wa mwanzo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, hivyo katika mchezo wa leo wanahitaji sare ya kuanzia 2-2 na kuendelea au ushindi wowote ili itinge hatua ya makundi.

Yanga endapo watavuka leo, basi watakuwa wametinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kama hawatapenya, basi timu hiyo yenye maskani yake Twiga na Jangwani, wataangukia mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Wawakilishi wetu hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika wanacheza na timu yenye uwezo mkubwa na tayari kocha wake, George Lwandamina ambaye aliwahi kuifundisha Yanga kwa muda mfupi, ametoa tahadhari kwa kusema, timu yao haijawahi kupoteza mchezo wa kimataifa kwenye uwanja huo wa Levy Mwanawasa.

Yanga wasitishike na mkwara huo wa kocha Lwandamina, kwani katika soka hakuna lisilowezekana, hivyo wanaweza kuitoa Zesco katika uwanja wao, kinachotakiwa ni kujituma wakati wote wa mchezo, dakika zote 90.

Wachezaji wa Yanga wajue kuwa wana dhamana kubwa ya kuipeperusha bendera yetu ya taifa, baada ya kutolewa kwa mabingwa watetezi wa Tanzania Bara, Simba, ambao awali walipewa nafasi kubwa ya kufika mbali katika michuano hiyo.

Walitolewa mapema na timu ya Msumbiji ya UD Songo. Simba walitoka suluhu ugenini kabla ya kutoka sare ya 1-1 na wapinzani wao hao katika mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuondoshwa kwa faida ya bao la ugenini.

Kwa upande wa Azam, nao wana jukumu kubwa la kuibeba nchi yetu baada ya wawakilishi wengine wa Kombe la Shirikisho Afrika, KMC kutolewa mapema na AS Kigali ya Rwanda.

Hivyo tunawatakia kila la heri wawakilishi hao wa Tanzania Bara ili waweze kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa kwa klabu barani Afrika.

KUANZIA leo hadi Jumapili wiki hii jijini Dodoma, Chama Cha ...

foto
Mwandishi: Tahariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi