loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM atema cheche viboko vya RC, ebola

RAIS John Magufuli amesema mbinu za kibeberu zinatumika, ikiwemo kuzusha kuwepo kwa magonjwa hatari ya ebola na zika hapa nchini ili kudhoofi - sha juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Pia, Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kuwacharaza viboko wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiwanja iliyopo wilayani Chunya, kwa kuwakuta na simu za mkononi na kuongeza kuwa viboko alivyowachapa vilikuwa vichache.

Alitoa kauli hiyo jana mkoani Songwe katika ziara yake ya kikazi, ambako aliweka jiwe la msingi la Mradi wa upanuzi wa huduma za maji katika Kijiji cha Mantengu unaogharimu Sh bilioni 1.6 na utawahudumia watu 44,000.

Lakini, pia alizindua Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha GDM ambacho kinamilikiwa na kijana wa Kitanzania. Magufuli alisema taifa linapoamua kufanya mambo ya kimaendeleo, huzushiwa kila aina ya jambo, ikiwemo magonjwa hatari ya zika na ebola.

Aliongeza kuwa hizo ni mbinu za kibeberu, kwa kuwa taifa linapozushiwa kuwa na magonjwa hayo, huwafanya wageni kutoka nje kuogopa kuja hapa nchini, lakini pia wawekezaji nao hawawezi kuja.

Alisema mbinu kama hizo, zilitumika kupitia kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela aliyetangaza kuwepo kwa ugonjwa wa zika hapa nchini katika mikoa ya Morogoro na Geita mwaka 2016.

Baada ya Dk Malecela kutangaza jambo hilo, Rais Magufuli alisema aliamua kutengua uteuzi wa Dk Malecela saa 7:30 usiku na kisha kumteua Profesa Yunus Mgaya kukaimu nafasi hiyo kisha kumthibitisha rasmi hivi karibuni.

“Waliyemtuma kutangaza kuwepo kwa ugonjwa wa zika hapa nchini nilimfukuza kazi saa 7:30 usiku na wiki moja baadaye walimteua kuwa bosi wao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuna ugonjwa wa ebola kwa zaidi ya miaka 10 sasa, mbona kila siku wanaendelea kuchimba madini, hizi ni mbinu za kibeberu kwa sababu wakisha kuzushia kama kuna haya magonjwa maana yake wageni na wawekezaji hawawezi kuja hapa nchini,”alieleza Rais Magufuli.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa taifa hili lilipata Uhuru Desemba 9, 1961, lakini siyo uhuru wa kiuchumi, kwa sababu liliendelea kunyonywa kwa namna mbalimbali, ikiwemo kupitia mikopo ya miradi ya maendeleo au misaada yenye kudhalilisha ikiwemo ujenzi wa vyoo.

Viboko shuleni, ampongeza RC Mbeya Wakati huo huo, kutokana na baadhi ya wananchi kumlaumu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kuwacharaza viboko wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiwanja iliyopo wilayani Chunya, kwa kuwakuta na simu za mkononi, Rais Magufuli amempongeza Chalamila kwa uamuzi huo na kuongeza kuwa viboko alivyowachapa vilikuwa vichache.

“Nakupongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuwacharaza viboko wale wanafunzi, haiwezekani serikali itoe fedha nyingi za kujenga madarasa na mabweni halafu wanafunzi wafanye vitu vya ajabu shuleni, niliagiza wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita wafukuzwe shule na Bodi ya Shule ivunjwe, tuache mambo ya mchezo katika mambo ya maendeleo,” alisema Rais.

Alisema taifa lilikosea kuondoa adhabu ya viboko shuleni, hivyo alitamani sheria ifanyiwe marekebisho ili adhabu ya viboko iendelee kutumika. Alisema kuwa ili wanafunzi waliofukuzwa warudi shuleni hapo, lazima wazazi wao watoe fedha kwa ajili ya kujenga bweni lililoungua.

Ujenzi wa maboma, soko, stendi Baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela kumuomba Rais Magufuli Sh bilioni mbili zilizobaki kwenye ujenzi wa Makao Makuu ya Mkoa ili zitumike kujenga kiwanja cha michezo, Rais aliagiza fedha hizo zikamalizie ujenzi wa maboma ya shule. Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Sh bilioni 4.5 tu ndiyo zilitumika katika kujenga Makao Makuu ya Mkoa na kubaki Sh bilioni mbili. Awali, Mwangela alimueleza Rais kuwa mkoa huo umefanikiwa kujenga maboma 1,000 ya watoto.

Magufuli aliutaka uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na wabunge wao na halmashauri zote, kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza ekari 50 zimegwe kutoka katika eneo la Kituo cha Utafiti cha Uyole kilicho chini ya Wizara ya Kilimo ili zitumike kwa ajili ya ujenzi wa soko kuu la mazao na stendi kuu ya mkoa.

Vijana Kwa kuwa Mtanzania anayemiliki Kiwanda cha Kukoboa kahawa cha GDM mkoani Songwe ni kijana, Rais Magufuli aliwataka vijana wengine wa Kitanzania kuiga mfano huo wa kujenga viwanda hata kama ni vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani mazao kama vile korosho, alizeti, pamba na mengine mengi. Katika ziara hiyo, Rais Magufuli ameongozana na Mkewe, Mama Janeth na mawaziri kadhaa.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi