loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete- Kumuenzi Nyerere si hisani

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema si hisani kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwani amefanya mema mengi na kutaja mambo manane yanayomfanya kustahili kukumbukwa kila mwaka.

Aliyasema hayo kwenye Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam jana.

Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1961 ili kutoa mafunzo ya uongozi ikiwemo kujengwa kimaadili, kiuongozi, kimsimamo na kimwelekeo ili waweze kujibaini na kujirekebisha au kurekebishwa pale wanapokosea kama viongozi.

Kutokana na hilo, aliupongeza uongozi na menejimenti nzima ya chuo hicho chini ya Mkuu wa Chuo, Profesa Shadrack Mwakalilo kwa kuchagua kaulimbiu isemayo ‘Urithi wa Mwalimu Nyerere Katika Uongozi, Maadili, Umoja na Amani Katika Ujenzi wa Taifa’ ambayo inaakisi uhalisia wa yale ambayo Mwalimu aliyaamini na kuyasimamia.

Kwa mujibu wa Kikwete, kumbukumbu anayofanyiwa Baba wa Taifa kila mwaka siyo hisani bali anastahili kutokana na mambo makuu manane aliyoishi na kuyafanya ikiwemo ukombozi wa Watanzania dhidi ya ukoloni.

Alisema Mwalimu Nyerere baada ya kuona kila walipokuwa wakikutana katika Chama cha Tanganyika African Association (TAA) kilichoanzishwa mwaka 1929 ambacho kilikuwa kinajadili maslahi ya wanachama, lakini wakati huo huo hoja za kisiasa kujitokeza, aliamua kuanzisha Chama cha TANU mwaka 1954 ambacho kiliwasaidia kujikita katika harakati za kisiasa za kudai uhuru na hatimaye uhuru huo ulipatikana mwaka 1961.

Kwa mujibu wa Kikwete serikali ya kikoloni ilimweleza Mwalimu ama achague kuendelea na kazi ya ualimu au aache ualimu ajiunge na siasa, katika hilo Mwalimu aliamua kuacha kazi ya ualimu na kujiunga na siasa ili kuendeleza harakati za kudai uhuru.

“Sababu zingine zinazomfanya Baba wa Taifa kustahili kukumbukwa kila mwaka ni karama aliyokuwa nayo ya kudai uhuru kwa njia ya amani.

Alitumia maarifa tu, yakatosha kufanikisha uhuru wetu, lakini pia alikuwa na imani katika umoja. Alishirikiana na Mzee Karume katika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Muungano huu umedumu ukilinganisha na nchi zingine kama vile Sene-Gambia ambazo ziliungana lakini muungano wao ukafa,”alieleza Kikwete.

Mambo mengine aliyoyataja ambayo yanampa sifa Baba wa Taifa kuenziwa kila mwaka ni uwezo wake wa kulijenga taifa hili.

Alisema si jambo rahisi kwa nchi yenye makabila zaidi ya 120 kuijenga kuwa taifa imara.

Alisema hilo liliwezekana kutokana na Mwalimu kuamini katika umoja, amani na mshikamano.

Kikwete alisema kazi hiyo iliyofanywa na Baba wa Taifa ndiyo imeifanya Tanzania yenye watu wa rika mbalimbali, dini mbalimbali, makabila mbalimbali, wasomi na wasiyo wasomi kuendelea kuwa wamoja.

Alisema nchi zingine zina makabila mawili tu lakini umoja na amani hakuna. Rais huyo mstaafu alimwelezea Mwalimu kama kiongozi aliyeheshimu utu wa mtu kwa maana kwamba alikuwa mtu wa kawaida, alihusiana na watu wote, hakuwajengea watu hofu ya urais wake, alijishusha, dhamana ya uongozi haikumfanya ajione kuwa yeye ndo mtu zaidi ya wengine au mwenye haki zaidi ya wengine.

Aliongeza kuwa Baba wa Taifa pia alijali uhuru wa mataifa mengine na kudiriki kusema kuwa uhuru wa Tanzania hauna maana kama nchi zingine bado zinatawaliwa na wakoloni. “Baba wa Taifa pia aliwapenda na kuwajenga vijana taratibu kisiasa.

Aliona umuhimu wa kuwalea vijana na kuwa na nafasi ya vijana katika Halmashauri Kuu ya Taifa. Lengo la Mwalimu kufanya hivyo ilikuwa kuwasaidia vijana kujifunza kusema, kupanga mawazo na kujifunza namna nchi inayoendeshwa,”alisema na kuongeza:

“Pia Mwalimu alikuwa anaamini katika majadiliano kama njia muhimu ya kufikia mwafaka, alikuwa hamkatishi mtu akiongea, hakutishwa na hoja, aliamini kuwa mawazo hayapigwi rungu bali yanashindana na mawazo yaliyo bora zaidi.”

Watoa mada Baadhi ya watoa mada katika Kongamano hilo walieleza umuhimu wa kuendelea kumuenzi Mwalimu na kuishi yale aliyoyaacha.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Joseph Butiku ambaye aliwahi kufanya kazi na Baba wa Taifa, alisema Mwalimu aliamini katika Ujamaa kwa kuwa Ujamaa ni watu walio sawa katika utu wao na kuwa na haki sawa bila ubaguzi.

Butiku alisema Mwalimu aliamini katika Azimio la Arusha na kabla ya kifo chake aliomba siku moja Watanzania warudi katika Azimio hilo pamoja na kujitegemea kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

“Baba wa Taifa alisema hakuna nchi duniani inayoendeshwa bila miiko ya maadili, hivyo alipinga rushwa kwa nguvu zake zote na aliamini bila watu kulipa kodi siyo rahisi kuendesha nchi, hivyo Kongamano hili linatukumbusha tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi,”alieleza aliyewahi kuwa Kaitbu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama.

Dk Haruni Kondo alisema katika miaka ya hivi karibuni taifa lilitoka katika lengo na kushindwa kupiga vita rushwa, ufisadi na kujikuta likibinafsisha mashirika ya umma, kutokea kwa mmomonyoko wa utaifa na uzalendo mambo ambayo yalichangiwa na kuvunjwa kwa Azimio la Arusha lililoanzishwa na Baba wa Taifa.

Katibu Mkuu CCM Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alisema miongoni mwa mambo ambayo taifa linapaswa kumkumbuka Baba wa Taifa ni Lugha ya Kiswahili.

Alisema alikitumia Kiswahili kabla na baada ya uhuru na alikifanya kuwa Lugha ya Taifa, hivyo Watanzania hawanabudi kuidumisha na kuitumia katika kuimarisha umoja na kujenga maendeleo.

Alisema Mwalimu pia aliamini katika Azimio la Arusha ambalo lilijenga misingi ya heshima ya taifa hili. “Utanzania wetu, uafrika wetu, utaifa wetu una chimbuko katika Azimio la Arusha,”alieleza.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, Mwalimu Nyerere pia alikuwa mtu aliyekuwa tayari kukiri makosa aliyokuwa anayafanya kama kiongozi.

Aliyataja baadhi ya makosa ambayo Baba wa Taifa alikiri kuyafanya kuwa ni kushindwa kuimarisha Serikali za Mitaa lakini pia kushindwa kuimarisha vyama vya ushirika.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi